The House of Favourite Newspapers

Niyonzima: Msihofu, Narudi Yanga SC

0

Wilbert Molandi| CHAMPIONI| Dar es Salaam

KIUNGO mchezeshaji wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, amewaambia maneno mazuri mashabiki wa timu hiyo, akitamka kuwa bado anaipenda klabu yake huku akiahidi kuongeza mkataba mwingine.

Niyonzima ni kati ya wachezaji 13 ambao mikataba yao inamalizika mwezi ujao, wengine baadhi ni Vincent Bossou, Deogratius Munishi ‘Dida’, Thabani Kamusoko, Anthony Matheo na Malimi Busungu.

Kiungo huyo, hivi karibuni alitajwa kuwepo kwenye orodha ya wachezaji wanaowaniwa kusajiliwa na Simba kwa dau la shilingi milioni 35 ambalo amelikataa.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Niyonzima alisema amekaa kwa amani muda mrefu ndani ya klabu hiyo, hivyo ni ngumu kwake kuondoka vibaya.

Niyonzima alisema, tayari yupo kwenye mazungumzo ya mwisho na Yanga kwa ajili ya kuongeza mkataba mwingine wa miaka miwili na wakati wowote atasaini.

“Nikwambie kitu, sidhani kama kuna mchezaji wa kimataifa kutoka nje ya nchi alidumu kuichezea klabu yake kwa muda wa miaka mitano mfululizo bila kuihama timu yake kama mimi.

“Mimi nimekaa kwa amani na kuvumilia hali zote za shida na raha, hivyo sidhani kama ni sahihi mimi kuondoka vibaya Yanga, nitaondoka lakini siyo kama inavyoelezwa.

“Bado mchezaji halali wa Yanga ninayemaliza mkataba wangu mwezi ujao, hivyo Wanayanga wasiogopeshwe na taarifa mbalimbali zinazohusiana na mimi kwenda Simba,” alisema Niyonzima.

 

Leave A Reply