The House of Favourite Newspapers

Mwigulu Aagiza Watu Hawa Wakamatwe, Wasiachiwe! – Video

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Mwigulu Nchemba ameliagiza Jeshi la Polisi kuwatoza faini, kuwaweka ndani madereva wanaovunja sheria za barabarani na kusababisha ajali kizembe na wasiachiwe mpaka watakapofikishwa Mahakamani.

 

Mwigulu ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Aprili 5, 2018 bungeni Mjini Dodoma wakati akitoa taarifa ya ajali iliyotokea wilayani Igunga usiku wa kuamkia leo, ajali iliyohusisha lori aina ya fuso na basi la abiria la Kampuni ya City Boys na kuua watu 12 huku wengine 46 wakijeruhiwa.

 

“Taarifa za awali tulizopewa zilieleza chanzo cha ya ajali hiyo sio mashimo ya barabarani pekee yake bali ni mwendokasi wa dereva wa fuso ambaye aliligonga basi hilo. Wengine walipita mchana kutwa kwenye hayo mashimo yeye akaja kusababisha ajali usiku. Naliagiza Jeshi la Polisi popote pale watakapomkamata dereva anatembea mwendokasi pamoja na hiyo ya kutoza faini, wamuweke ndani wasimuachie mpaka pale watakapompeleka Mahakamani ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa”, amesema Mwigulu.

 

Pamoja na hayo, Mwigulu ameendelea kwa kusema “endapo dereva huyo akitoka Mahakamani na kama rekodi zake ni mwendokasi basi anyang’anywe leseni yake ili asiweze kuendelea kuendesha magari yanayosababisha ajali na kupoteza maisha ya watu kama hivi jana ilivyotokea”.

 

Aidha, Rais Magufuli amewataka viongozi wote wanaohusika na usimamizi wa usalama wa barabarani kutafakari kwa nini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali.

VIDEO: MSIKILIZE MWIGULU AKIFUNGUKA

Comments are closed.