WANANCHI wa Shinyanga wamejitokeza kwa wingi kuuaga mwili wa baba mzazi wa aliyekuwa msaani wa Bongo Movies, marehemu Stephen Kanumba, mzee Charles Kanumba (71), kabla ya kusafirishwa kwenda katika Kijiji cha Nyakaboja, Busega mkoani Simiyu kumpumzisha kwenye makazi yake ya milele leo, Jumatano, Machi 11, 2020.
Zoezi la kuuaga mwili huo limefanyika jana Jumanne Machi 10, 2020, nyumbani kwake Mtaa wa Magadula, Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, huku ibada ya kumuaga ikiongozwa na mchungaji Benjamin Makaranga wa Kanisa la AICT Ngokolo.
Akisoma historia ya marehemu kwa niaba ya familia, Rubeni Zakayo, ambaye ni ndugu wa karibu na familia ya marehemu, alisema marehemu alizaliwa mwaka 1949 huko Busega mkoani Simiyu.
Mara baada ya kustaafu kazi serikalini mwaka 2015, alianza kusumbuliwa na maradhi ya nyonga, tumbo, magoti, na kibofu cha mkojo, hadi umauti ulipomkuta Machi 8, mwaka huu.
Aliongeza kuwa marehemu ameacha mjane na watoto saba, ambapo alifanikiwa kuzaa watoto tisa, lakini wawili wameshatangulia mbele za haki, watoto wa kiume watano na wa kike wanne.
Naye Mchungaji Zabroni Mang’wenghula kutoka Kanisa la AICT Ndala, aliwataka wananchi kumtumaini Mungu katika enzi za uhai wao, ili kujiweka tayari pindi watakapotwaliwa Naye.