The House of Favourite Newspapers

Mzee Kipara Atoa Fundisho Kubwa kwa Wasanii Bongo

Fundi Saidi ‘Mzee Kipara’

MANYUNYU ya mvua yananipiga, hali ya hewa ni baridi kali, nipo kwenye mlima mrefu na kwa mbali naona wanyama mbalimbali wakiwa wamejikunyata chini ya miti.

Najaribu kuvuta picha ya sehemu nilipo, akili yangu inashindwa kung’amua eneo hilo ni wapi.

 

Wakati nikiendelea kutafakari, ghafla anatokea mtu mzee mwenye mvi, anatumia bakora yake kutembelea.

Nami picha imekuja, ni mzee wangu muigizaji Fundi Saidi ‘Mzee Kipara’. Haraka naanza kukumbuka michezo yake aliyoshiriki iliyokuwa inarushwa kwenye Luninga ya ITV ikiwemo Fukuto, Jahazi na Baragumu. Namsalimia na kuanza kuzungumza naye:

 

MIMI: Mzee wangu shikamoo na habari za siku nyingi.

MZEE KIPARA: Daah! Wewe kijana kama nakukumbuka, si ulikuwa unakuja mara kwa mara pale nyumbani kwangu, Kigogo Round About kunihoji.

MIMI: Ni kweli kabisa hujakosea, mimi naitwa Erick Evarist najua jina langu ulikuwa umeshalisahau.

MZEE KIPARA: (anacheka kidogo) Ni kweli sura ilikuwa inakuja lakini jina kwa kweli lilinitoka. Enhe vipi huko utokako, wanasemaje wasanii wenzangu?

 

MIMI: Wapo wanaendelea kupambana, kidogo mambo yanakwenda si kwa kasi ile ya zamani.

MZEE KIPARA: (Anahamaki) Nini shida? Mbona niliwaacha wasanii wanafanya vizuri wakiongozwa na Kanumba japo naye baadaye alinifuata huku. Au alipoondoka Kanumba ndiyo nao wakaanza kusuasua?

MIMI: Nafikiri ni ule ushindani tu ulipungua kidogo hasa kwa mpinzani wake Vincent Kigosi ‘Ray’ lakini pamoja na hilo nafikiri kuna sababu nyingine za kimfumo ambazo zimechangia kushusha muamko wa sanaa nchini.

 

MZEE KIPARA: (anatikisa kichwa kulia na kushoto) Kijana sijaridhika na majibu yako lakini, mfumo kivipi?

MIMI: Mfumo namaanisha serikali iliyopo madarakani kwa sasa, imedhibiti mafisadi, imezuia biashara ya madawa ya kulevya na kuzuia kabisa mianya ya fedha za haramu sasa hali kidogo imekuwa ngumu mfukoni.

Iko hivi, wale mafisadi walikuwa wanamwaga fedha haramu ambazo zilikuwa zinazunguka kwa watu kwa namna mbalimbali sasa kwa sasa hakuna hiyo kitu hivyo fedha zimekuwa ngumu hususan kwa wale waliokuwa wanategemea fedha hizo haramu.

 

MZEE KIPARA: Ooh hapo nimekupata bila shaka kama serikali iliyopo madarakani imefanya hivyo nafikiri ni jambo jema, watu wataumia kwa muda lakini baadaye watakaa sawa na wale waliozoea kupiga dili, watajifunza kujishughulisha na uchumi utajiseti wenyewe.

MIMI: (Huku nikimtolea macho kwa umakini) Ni kweli japo kwa wengine wanashindwa kuwa wavumilivu hasa wale waliozoea mteremko…

 

MZEE KIPARA: Kujenga uchumi wa kweli siku zote kuna gharama, lazima watu wajifunze kulipa gharama. Vipi Bi Chau, bado anaendelea kuigiza?

MIMI: (Nikajiweka sawa kisha nikamwambia) yupo! Ila kwa sasa amejikita zaidi katika utangazaji na kutoa mada mbalimbali za wanawake katika magazeti. Muda mrefu sana sijamuona akiwa lokesheni.

 

MZEE KIPARA: Daah kweli mambo yanabadilika, sasa wale wakongwe wenzangu wanaishije sasa hivi? Nakumbuka tulikuwa tunasuasua sana kuhusu kipato, wasanii sasa hivi wanapata wapi fedha?

MIMI: Siku hizi wengi wamerudi kwenye enzi zile mlizoanzia lakini angalau kuna makampuni ya luninga yanawalipa kidogo hela nzuri kwa kuandaa tamthiliya ambazo zinakuwa mali ya makampuni husika.

Wao wanalipwa, wanaingia lokesheni kushuti na kisha hiyo tamthiliya inaoneshwa katika luninga husika.

 

MZEE KIPARA: Nimemkumbuka Mzee Majuto, na yeye ameweza kwenda na kasi ya vijana?

MIMI: Mzee Majuto bwana yupo, yeye siku hizi amekuwa akidaka fedha nyingi sana kwenye matangazo. Amekuwa msanii anayeongoza kwa kuwa na matangazo mengi sana ya bidhaa mbalimbali. Naye ni muda mrefu sijamuona lokesheni.

Hata hivyo hivi karibuni alikuwa amelazwa, alifanyiwa upasuaji. Lakini kwa sasa anaendelea vizuri.

MZEE KIPARA: (kwa huzuni) mpe pole sana najua naye umri umeenda kidogo, maradhi ni jambo la kawaida.

Niwasihi tu wasanii wenzangu kupambana kuhakikisha sanaa ya uigizaji inaheshimika, yasije kutokea kama yale yaliyonitokea mimi wakati niko hai. Umri unakuwa umekutupa mkono lakini hujanufaika na kitu.

 

Kuigiza tena unakuwa huwezi, unaishia kuwa mtu wa kusaidiwa kila siku na wenzako. Si jambo jema. Ni vyema pia wakawa na bima za afya ili ziweze kuwasaidia, mambo ya kuombaomba msaada si mazuri pale umri utakapokuwa umeenda.

Wakati akizungumza hayo, ghafla napigiwa simu na mchumba wangu ambaye huwa ana hawaida ya kuniamsha kila alfajiri nijiandae kwenda kazini. Nagundua mazungumzo yangu na Mzee Kipara ilikuwa ni ndoto tu na si halisi.

Na Erick Evarist

Comments are closed.