The House of Favourite Newspapers

Mzee Mwinyi: Kijana Wetu Magufuli Ametutendea Makubwa

0

RAIS Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amewataka Watanzania kumuenzi Dk John Magufuli kwa vitendo katika mambo aliyokuwa akisisitiza kuondoa umasikini na kuleta ustawi kwa wananchi wote.

 

 

Akitoa salamu za rambirambi katika Misa Takatifu ya maziko ya Magufuli iliyofanyika jana Chato mkoani Geita, Mwinyi alisema kutokana na upendo wake kwa Watanzania, kiongozi huyo aliamua kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania masikini kwa kusisitiza kila mtu kufanya kazi huku akiwa na usimamizi makini wa rasilimali za nchi.

 

 

“Safari za ndege zimerudi katika nchi, tena siyo za London na Dubai bali ni ndege zetu wenyewe ambazo zinakwenda kila mahala, kijana wetu huyu ametutendea makubwa,” alisema Mwinyi.

 

 

Alisema kutokana na upendo na huruma aliyokuwa nayo kwa wananchi masikini, aliamua kuwasaidia wafanyabiashara wamachinga kwa kuwaondolea fedheha kwa kuwapa ruhusa na kinga.

 

 

Mwinyi alisema Magufuli aliwapenda na kuwahurumia wanyonge kwa kuwainua baada ya kuwajengea mahali mahususi pa kufanyia biashara huku wakiwa na kinga ya kutosumbuliwa na vyombo vya usalama na mamlaka ya mapato.

 

“Kwa hilo siyo machinga pekee, hata akina sisi na watu wengi tumeingia katika huruma hiyo ya hayati Rais Magufuli. Tukawa tumepata mtu wa kutusemea, kututhamini na kutufanya watu wa maana kama walivyo Watanzania wengine, huyo ndio Magufuli,” alisema Mzee Mwinyi.

 

 

Mzee Mwinyi aliwavunja mbavu watu baada ya kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote wasimchoke kumsikiliza kutokana na kutokuwa na kasi ya kusoma hotuba yake hiyo.

 

 

Alisema katika kipindi kifupi cha miaka mitano alichoongoza Magufuli, nchi imepiga hatua kubwa na kuushangaza ulimwengu kwa namna alivyoiletea maendeleo ya haraka nchi yake kwa jinsi alivyokuwa mfuatiliaji asiyechoka wala kukata tamaa.

 

 

Mzee Mwinyi alisema Magufuli alifanikiwa kwa haraka katika kipindi kifupi kwa kuwa alikuwa mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno na mfuatiliaji mkubwa wa kile anachotaka kifanyike.

 

 

“Hayati Magufuli sio tu kwamba aliunganisha nchi kwa barabara, bali hata masoko makubwa ya kisasa yalianza kuchipuka kama uyoga nchini Tanzania,” alisema.

Leave A Reply