The House of Favourite Newspapers

Mzungu Awapa Rungu Okwi Na Chama

STRAIKA Mganda Emmanuel Okwi na Kiungo machachari Claytous Chama, wamepewa rungu na kocha wao Patrick Aussems ili wawamalize Nkana mapema tu leo Jumapili.

 

Kwenye mazoezi ya mwisho ya Simba, yaliyofanyika Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam juzi jioni, Spoti Xtra lilimshuhudia Aussems akiwapatia maelekezo Okwi na Chama namna wanavyotakiwa kushirikiana kwa ukaribu ili kumaliza mchezo huo mapema.

“Nimefanya mazoezi mazuri na wachezaji wangu kikubwa nilikuwa najaribu kuwapa mbinu zaidi za kumiliki mpira kwani ili tuumudu mchezo huo hakuna namna nyingine tunavyoweza kucheza zaidi ya kumiliki na kufunga mapema iwezekanavyo.

 

“Hilo ndiyo jukumu pekee ambalo nimewapatia wachezaji wangu wote, niwaombe tu mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi ili watupe hamasa ya kutosha kwani bila wao hatuwezi kuwa na hamasa maana Nkana kwao waliweza kufanikisha hilo na ndiyo maana wakapata matokeo mazuri kwenye mchezo, ila hapa kwetu sisi tuna nafasi kubwa sana ya kuwafunga,” alisema Aussems.

 

DILI LA BOCCO

Imebainika kwamba Mohammed Dewji ‘Mo’ ametibua dili la mshambuliaji John Bocco kutimkia nchini Misri katika klabu ya Al Masry ambayo ilishafikia sehemu nzuri ya maelewano na Simba.

 

Pande hizo mbili zilikuwa tayari zilishakubaliana juu ya mauzo ya mshambuliaji huyo ambapo alitarajiwa kutua hivi karibuni lakini Mo ametibua baada ya kutaka abakie klabuni hapo.

 

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Spoti Xtra kuwa, Mo amezuia dili hilo la Bocco kwa sababu hakukuwa na mchezaji mbadala ambaye anaweza kusajiliwa kuziba nafasi yake kwa sasa lakini pia ishu ya kutotaka kupoteza straika mwingine baada ya Emmanuel Okwi kuomba kutimka.

Comments are closed.