Kartra

Nabi Amvuta Yanga Mrithi wa Metacha

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amemjumuisha kikosini kipa wa timu ya vijana, Geofrey Magaigwa ili kuchukua nafasi ya Metacha Mnata ambaye amesimamishwa kutokana na suala la utovu wa nidhamu.

 

Yanga U20, ilifanikiwa kufanya vizuri kwenye Ligi ya Vijana ambapo ilishika nafasi ya pili baada ya kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Mtibwa kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.

 

Geofrey Magaigwa ni mmoja kati ya vijana ambao wamepata nafasi ya kusafiri na timu ya wakubwa ambayo ilicheza jana dhidi ya Biashara United kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mkurugenzi wa Mashindano wa Klabu ya Yanga, Thabit Kandoro alisema kuwa: “Kwanza tumefarijika sana na timu ya vijana ambayo imefanya vizuri katika mashindano pamoja na vipaji vikubwa walivyovionyesha.

 

“Tunaweka mikakati mizuri ya kufanya kitu kikubwa zaidi kwa vijana kwa ajili ya msimu ujao ili kuhakikisha tunalichukua kombe la vijana.

 

“Kocha Nabi na benchi zima la ufundi lilikuwa linashuhudia mashindano ya vijana yaliyofanyika Chamazi na wamevutiwa sana na vipaji vyao, hivyo ameanza kumjumuisha Geofrey kwenye timu kubwa badala ya Metacha ambaye amesimamishwa kwa sasa,” alisema Kandoro.

Stori: Leen Essau, Dar es Salaam


Toa comment