The House of Favourite Newspapers

Namba 7 Pigo kwa Mama Kanumba – Video

0

DAR: Kama ni kumbukumbu mbaya, hakika namba 7 itabaki kuwa pigo kila atakapokuwa anaikumbuka mama mzazi wa marehemu Steven Charles Kanumba, Flora Mtegoa, kufuatia kuwapoteza wanawe wawili kwa nyakati tofauti katika siku inayofanana, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lina stori hii ya kuhuzunisha.

 

NAMBA 7 NI PIGO…

Kanumba ambaye ni mwanaye wa kumzaa, alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka 2012 huku mwanaye, mtoto wa mdogo wake mama Kanumba, Seth Bosco akifariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 7, mwaka huu na vifo vyao vikiwa vimetofautiana miaka saba (7).

 

“Hili ni pigo kwa kweli, mama Kanumba kila atakapokuwa anaikumbuka namba 7 kwake itakuwa ni kilio mara mbili. Anamlilia mwanaye Kanumba, lakini pia anamlilia Seth ambaye ndiye mtoto pekee aliyekuwa anaishi naye baada ya Kanumba kufariki dunia,” alisema mwigizaji mkongwe, Blandina Chagula ‘Johari’.

 

MAMA KANUMBA ANENA

Akizungumza kwa uchungu akiwa msibani nyumbani kwake, Kimara-Temboni jijini Dar, mama Kanumba ambaye ndiye aliyemlea Seth tangu akiwa mdogo, alionesha kuumizwa na kifo hicho na kwamba amebaki mpweke.

 

“Ni pigo zito kwangu kwa kweli, sijui hata nielezeeje. Kanumba aliondoka siku kama hii aliyoondoka Seth, jamani wanangu wameniacha peke yangu,” alizungumza kwa uchungu mama Kanumba huku akitokwa machozi.

 

SIKU YA TUKIO

Akizungumzia siku ya tukio, mama Kanumba alisema kuwa hali ya Seth ilianza kubadilika ghafla kuanzia asubuhi ya Desemba 6, mwaka huu kabla ya kufariki dunia usiku wa saa 6:30.

 

“Hali yake ilianza kubadilika ghafla tangu jana (Desemba 6), alisema mgongo unamuuma, kwa hiyo anahitaji kwenda Muhimbili (Hospitali ya Taifa), kweli tukampeleka, akafanya mazoezi kisha akarudi nyumbani.

“Tulipotoka Muhimbili, tukapika chakula cha mchana tukala. Baada ya hapo akasema anaenda kulala ila ikifika saa 12:00 jioni, tumuamshe ili aangalie Muvi ya Kanumba maana kuna chaneli walitangaza kuwa wataionesha.

 

“Kweli ulipofika huo muda ndiyo akaanza kutetemeka sana, ikabidi tumuite dokta. Dokta alipofika, baada ya kumuangalia, akamwambia aende kupumzika, lakini ilipofika saa 6:30 usiku mwanangu akafariki dunia,” alisema mama Kanumba.

 

MZAZI MWENZA WA MAREHEMU ANENA

Kwa upande wake, Doris ambaye ni mzazi mwenza wa Seth, alielezea jinsi alivyozipokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa.

 

“Jana (Desemba 6) asubuhi niliongea naye vizuri tu, ghafla baadaye usiku akanipigia wifi yangu Abela (dada wa Kanumba), akanipa taarifa za msiba, ila kwa kuwa nilikuwa kazini sikuweza kufika kwa wakati ule ndipo nikaja asubuhi msibani.

 

“Kwa kweli nimeumia mno, ameniachia mtoto mdogo. Naumia sana, naomba Mungu ampumzishe mahali pema peponi, amina,” alisema Doris.

 

JOHARI ANENA

Johari ambaye amekuwa karibu na familia ya Kanumba kwa muda mrefu, naye alielezea kwa masikitiko jinsi alivyopokea taarifa za msiba huo.

 

“Nilipigiwa simu na mama Kanumba usiku kuwa, Seth amefariki dunia, ikabidi nije kushirikiana nao. Nimeumia kweli, Seth amenifanya nizidi kuamini kuwa kifo kipo. Sisi kama wasanii wenzake kuna mikakati tunaipanga ili tuweze kumsindikiza mwenzetu salama kwenye nyumba yake ya milele,” alisema Johari.

MANENO YA MWISHO YAHUZUNISHA

Miongoni mwa maneno ya mwishomwisho ambayo Seth alizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, yanahuzunisha kutokana na jinsi alivyoonesha kuguswa na mateso ya kuumwa kwake.

 

MAHOJIANO YALIKUWA HIVI;

Ijumaa Wikienda: Pole sana Seth kwa ugonjwa unaokusumbua.

Seth: Shukrani sana, nipo hapa tu, nimelala sijui nitatembea lini.

Ijumaa Wikienda: Nini zaidi?

 

Seth: Tatizo langu kubwa wameniambia kuwa nina uvimbe kwenye uti wa mgongo, lakini zaidi ya hapo sina tatizo lingine.

Ijumaa Wikienda: Na kuhusu miguu kutotembea kabisa, ilikuwaje?

Seth: Kutokana na hilo tatizo ndiyo imesababisha hivyo, maana nilishtukia tu miguu haina nguvu, mwisho nikashindwa kabisa kutembea.

 

Ijumaa Wikienda: Lakini nimeona kwenye grupu moja la wasanii, wameanza kukuchangia…

Seth: (Mshangao) wameanza kunichangia mimi? Mimi sijui hilo kwani sasa hivi kuna hivyo vitu tena kwa upande wa wasanii, haya ngoja tuone.

Ijumaa Wikienda: Kwa nini umeshangaa?

 

Seth: Yaani sitaki kukuficha, nikisikia nachanganyikiwa, naumia sana roho yangu, natamani Mungu atende miujiza niinuke hapa kitandani.

Ijumaa Wikienda: Mungu atakusaidia, utapona…

Seth: Lakini naumia sana juu ya mama yangu.

Ijumaa Wikienda: Kwa nini unasema hivyo?

 

Seth: Namuonea huruma kwa sababu mama analia kila wakati juu ya kaka Kanumba, lakini sasa analia juu yangu nilivyo kwenye hali hii, ndiyo maana natamani nipone haraka mama asiendelee kuumia. Namuomba tu Mungu niinuke ili na mimi nisije kumuachia huzuni kubwa mama yangu.

 

Ijumaa Wikienda: Pole sana, Mungu atakutendea uombavyo, unawaambia nini wasanii wenzako kuhusiana na tatizo lako?

Seth: Kitu kikubwa ni kuwa na upendo tu, hata ushirikiano maana kwa pamoja tunaweza kufanya mambo mengi hasa kwenye ugonjwa na tukasaidia kwa haraka.

 

Ijumaa Wikienda: Asante sana na pole sana.

Seth: Asante sana, salamu zangu zifike kwa watu wa ofisini kwenu.

 

TUJIKUMBUSHE

Seth amefanya kazi kwa karibu na marehemu Kanumba enzi za uhai wake kupitia Kampuni ya Kanumba The Great Film Productions. Baada ya kifo cha Kanumba, kampuni hiyo ilitetereka na kushindwa kuendelea kuzalisha filamu na kufikia hatua baadhi ya mali za marehemu kuuzwa.

Kifo chake kimemkuta baada ya kusumbuliwa na maradhi ya mgongo ambayo yalimsababishia apooze mwili.

 

KUZIKWA

Mwili wa marehemu umezikwa jana jijini katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar. Marehemu ameacha mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka nane.

Stori: Imelda Mtema na Memorise Richard.

 

TAZAMA MAZISHI YA SETH

Leave A Reply