The House of Favourite Newspapers

NAMKUMBUKA RUGEMALIRA YULE; NAMSIKITIKIA HUYU!

James Rugemalira.

KAMPUNI ya Mabibo Beer Wines and Spirits Limited nilikuwa naisikia tangu miaka ya 90 mwishoni, lakini James Rugemalira sikuwa namfahamu kabisa.

 

Baadaye skendo ya Tegeta Escrow ilipofukuta mwaka 2014, nikaambiwa Rugemalira ambaye ni Mshauri wa Kimataifa wa Kujitegemea wa Kampuni ya Mabibo naye katajwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa waliochota fedha kwenye akaunti hiyo; nikasema ALAAAH!

 

Yaliposemwasemwa ikabainika kuwa Rugemalira niliyekuwa namfahamu kama wakala wa bia nyepesi na wine kutoka nje ya nchi pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya VIP Engineering ambayo inahusishwa na wizi wa fedha za Escrow; nikasema Duh!

 

Nakumbuka enzi hizo watu waliokuwa wanatamba kwa fedha waliitwa Mapedeshee; hawa walikuwa wanamwaga fedha kwenye kumbi za burudani na kufutia magari yao noti za elfu kumi huku wakishangiliwa lakini Rugemalira waliyesema ana fedha kama ‘njugu’ sikuwahi kumuona akifanya hivyo.

 

Kwa msingi huo sikuwa nimeamini kuwa mfanyabiashara huyo ana fedha hadi pale Juni 2014 alipofanya sherehe ya kihistoria ya ndoa ya mwanaye aitwaye Eve. Nakumbuka sherehe hiyo ilifanyika ndani ya Ukumbi wa Mlimani City, mapambo, vyakula na vikorombwezo vilivyofanywa kwenye sherehe hiyo ilitosha kuwafanya watu waseme haijawahi kutokea.

Hata wale ambao hawakwenda kwenye sherehe hiyo walisambaza picha za tukio hilo huku wengi wakiambananisha na maneno: Rugemalira aonesha jeuri ya fedha. Nakumbuka tulipopata picha na habari za sherehe hiyo tuliandika kwenye gazeti la Risasi kama sijasahau; mauzo ya gazeti hilo yalikuwa mazuri; hapo ndipo nikaamini kumbe Rugemalira watu wanamfahamu na wangependa kusoma habari zake.

 

Wakati nikimwamini hivyo, mwaka 2015 tuliambiwa kuwa mfanyabiashara huyo anafanya sherehe ya kutimiza miaka 70 ya uwepo wake duniani, kama waandishi tukasema, huko nyumbani kwake Makongo Juu, Dar hakutakuwa na mambo ya kitoto, ni vema tukajisogeza.

 

Picha ya historia ya yale aliyofanya kwenye sherehe ya mwanaye haikutofautiana sana, tuliyoyaona nyumbani kwa mzee huyo siku hiyo ya sherehe yalikuwa ya kipekee, itoshe kusema shughuli ilifana sana watu walisaza nyama, wali na pombe.

Baada ya kutoka huko na kunusanusa gharama iliyotumika kwenye sherehe hiyo tuliambiwa ni zaidi ya milioni 100 ambazo hatukuzipatia ushahidi lakini upepo wa habari kwenye magazeti na mitandaoni ulivumisha taarifa kwamba mzee Rugemalira alitumia kiasi kikubwa cha fedha.

 

Kwa kuwa wakati huo skendo ya Escrow ilikuwa imeanza kumkaba koo, mwanaye Eve akajitokeza na kusema kuwa watu wasipotoshe; baba yake hakutumia kiasi kikubwa cha fedha bali zilikuwa za kawaida na kwamba yeye ndiye aliyemwandalia baba yake shughuli hiyo.

 

Hata hivyo ‘safisha nyayo’ hiyo iligonga mwamba kwa vile wakati huo ilikuwa shida kumtenga Rugemalira na utajiri wa kutisha ambao wengi waliuhusisha na fedha chafu, jambo ambalo mimi sitaki kuliamini kwa sababu mahakama iko kazini kutafsiri sheria. Cha msingi nilichotaka kuandika katika makala haya ni kwamba huyu ndiye Rugemalira wa mwaka 2013-2014 niliyekuwa namfahamu; alikuwa mwenye afya ya mwili ni pochi nene!

 

Leo nipomtama Rugemalira ambaye mwanaye Eve amewahi kumsifia kuwa anajivunia kupata baba bora na kumshukuru Mungu kwa kumuweka hai hadi kipindi hicho cha harusi yake, anaonekana kuchoka afya na pengine mfuko mfukoni.

Huyu ndiye Rugemalira anayeniliza, ananifikirisha kuwa kumbe maisha ni safari na kwamba hujafa hujaumbika. Leo hii tajiri na mfanyabiashara mkubwa kama yeye anaweza kuwa kama mtu anayesumbuliwa na utapiamlo; ni jambo la kuogofya na kujifunza.

 

Lakini pia ni jambo linalotoa nafasi ya kumfanya kila mtu kuifikiria kesho yake, kuishi kwa fikra kuwa kuna kupanda na kushuka na kwamba Mungu kaumba vitu viwiliviwili. Kuna mchana na usiku, kulia na kucheka, kushiba na kuona njaa, wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna, wakati wa joto na wakati wa baridi; yote haya ni maisha yetu.

 

Nisingependa kuzungumzia mambo yanayoendelea mahakamani juu ya kesi ya utatishaji fedha inayomkabili mzee Rugemalira na mwenzake Harbinder Seth kwa kuwa kanuni zinakataza lakini vyema nikawaombea heri wazee hawa katika safari yao ya kutafuta haki.

GLOBAL HABARI NOV 26: Rais Dkt. Magufuli Aungana na Wakatoliki kuaga mwili wa Askofu Evaristo

Comments are closed.