Namshauri rais wetu Magufuli  haya muhimu kwa taifa

Namshukuru Mungu kwa kutuweka hai leo.

Leo nimeamua kumshauri Rais Dk. John Pombe Magufuli kutekeleza mambo nane ili kuweka misingi ya mabadiliko nchini, ikiwemo serikali yake kuweka wazi mikataba yote ya rasilimali za nchi.

Mikataba hiyo ni pamoja na ile ya mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji na ya madini. Ili Serikali ya awamu ya tano ifanye mabadiliko ya msingi, ni vyema Dk. Magufuli akahakikisha kuwa pamoja na kuweka wazi mikataba, pili, anafuta posho za vikao katika mfumo mzima wa serikali kama Mpango wa Maendeleo unavyotaka. Fedha hizo zitasaidia kuendeleza mambo pale panapohitajika kama watakavyoona inafaa.

Tatu ni vyema pia Dk. Magufuli akafuta matumizi ya mashangingi ambapo tayari Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeanza kuonesha mfano, wote tunajua jinsi magari hayo yanavyotumia mafuta mengi yanayogharimu fedha nyingi za walipa kodi.

Suala la nne ambalo Rais Magufuli anaweza kulifanya ni kufuta taratibu uagizaji wa sukari kutoka nje na kuanzisha miradi ya miwa ili Tanzania nayo iuze sukari yake nje ya nchi na kutupatia fedha za kigeni.

Suala la tano, nasisitiza kwa serikali ya awamu ya tano ni kuweka wazi taarifa ya serikali kuhusu tuhuma za utoroshaji wa fedha na kama zipo basi serikali ifungue mashtaka kwa wahusika mara moja ikiwezekana fedha hizo zirejeshwe zije kufanya kazi za maendeleo.

Sita, ni vyema akaipatia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), mamlaka ya kukamata na kushtaki mtu atakayebainika na kuthibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa badala ya kuwa na mzunguko mkubwa wa kupeleka suala hilo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hata kwa jambo lililo wazi.

Saba,  serikali ihakikishe kila Mtanzania mwenye mali, ahakikishe anathibitisha namna alivyoipata na kuhakikisha mali na madeni ya viongozi yanawekwa wazi kwa umma na wananchi waruhusiwe kuhoji.

Nane, kutokana na hali ya uchaguzi ilivyo Zanzibar, namshauri Dk. Magufuli, kuruhusu uchaguzi kufanyika katika majimbo ambayo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliona yana kasoro kutokana na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi lakini yale ambayo waliona hayana kasoro na tume kutoa vyeti kwa walioshinda, wasirudie uchaguzi.

Tusipochukua tahadhari suala la Zanzibar litatutia doa kama lilivyowahi kutuaibisha mwaka 2001 ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania tulizalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni, Mombasa Kenya. Ilikuwa ni aibu kubwa kwa nchi yetu!

Tisa,  nimshauri Rais Magufuli, kuanza mchakato wa Katiba mpya kwa kuanzia alipoishia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kuachana na Katiba Pendekezwa kwani ilituletea mgogoro mkubwa wa hatari. Yote haya yakifanyika nchi yetu itazidi kudumu katika mshikamano na amani itadumu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Loading...

Toa comment