The House of Favourite Newspapers

Nani kauona mwaka 2019? Soma Hapa Ujifunze Jambo

SHANGWE za kumaliza mwaka 2018 na kuingia 2019 zilisikika kila kona ya nchi jana (Jumanne).

“Nashukuru tumeuona mwaka mpya,” zilikuwa nyingi huku wimbo wa DDC Mlimani Park Orchester uitwao Huma Kwa Wagonjwa ukitawala kupigwa kwenye kumbi za starehe, majumbani na kwenye mitandao ya kijamii.

Hakika ni jambo la heri kufunga mwaka na kuingia mwaka mpya ukiwa hai, lakini nimeona vyema niyarejee mashairi ya wimbo nilioutaja ili tuutafakari pamoja katika mwaka huu mpya tuliouanza.

 

Wimbo huo umetungwa na mwanamuziki Shabani Dede unaanza na mashairi haya:

Vifo vingi hutokea kwa kukosa msaada na kutomudu gharama za matibabu eeee, yatupasa tusaidiane.

Mtunzi anatuambia kuwa vifo vingi hutokea kwa kukosa misaada; hebu tujiulize mwaka uliopita ni watu wangapi wenye uhitaji tuliwakunjulia mikono yetu?

Tumejitoa mara ngapi kuwasaidia wagonjwa katika kuokoa maisha yao au tuliwaacha wafe na leo sisi tunashangilia bila wenzetu.

 

Mwaka 2019 tuache ubinafsi, tusaidiane ndugu zangu.

Dede anatukumbusha kitu kingine kuhusu suala la ajali kwa kuweka mashairi haya:

Uonapo barabarani, ajali imetokea na watu kujeruhiwa,

Wanahitaji msaada wenu wa hali na mali.

 

TUBADILIKE NA TUJENGE TABIA YA KUPENDA KUSAIDIA WENGINE YATUPASA TUSAIDIANE

Ndugu yangu mwaka 2019, tubadilike na kupenda kuwajali wenzetu, ile hali ya ajali kutokea na kukimbilia kupiga picha za kuposti mitandaoni na kuwaacha majeruhi wakitapatapa kutafuta msaada tuiache.

Maana kuna watu bila huruma ajali inapotokea wanakimbilia kupora maiti fedha na kuwanyang’anya majeruhi mali zao. Tuache tabia hizi mbaya sisi sote ni binadamu ndugu zangu.

Tunaendelea kukumbushwa jambo jingine:

Siku hizi maradhi mengi yamezuka ambayo husababisha vifooo na wagonjwa huteseka, basi tujenge tabia ya huruma kwa wagonjwa yoyooo.

 

HURUMA EE HURUMA JAMAA TUSAIDIANE WANADAMU.

Wakati wewe na mimi tunasherehekea jana kuuona mwaka mpya kuna ndugu zetu wako mahospitalini wamelazwa, wengine wamekata kauli wanasubiri watu wa kuwasaidia watoke katika lindi la umauti; halafu sisi tumekesha tukimwaga fedha baa na kwenye majengo ya starehe.

Mwaka 2019 tumeambiwa na mtunzi tujenge tabia ya kujali wagonjwa.

 

Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa mwaka 2018 vyombo vyetu vya habari vya Global viliwafikia wagonjwa wengi wasiokuwa na uwezo wa kujitibia na kuendesha kampeni nyingi ambazo zilisaidia kuhamasisha jamii kuwachangia na wagonjwa wengi walisaidika.

Shukrani ziwaendee wote waliojitokeza kwa msaada wa aina yoyote mwaka 2018 kuwasaidia wagonjwa waliokuwa wakiteseka mahospitalini nchi nzima, moyo huo wa kujitoa unapaswa kuendelezwa mwaka 2019 kwa nguvu zote ili tuweze kupewa neema na Mungu ya kuumaliza mwaka huu kama ilivyotokea mwaka jana.

 

Pamoja na hayo Dede anatukumbusha jambo muhimu sana katika maisha yetu mwaka huu, hebu sikiliza mashairi haya halafu nitarejea kuyafafanua:

Ingawa kuishi ni bahati na kufa ni lazima kwetu sote.

Ndugu yangu mpendwa shangwe tulizozifanya kuukaribisha mwaka mpya hazikutokana na ujanja wetu, ni bahati aliyotutunuku Mwenyezi Mungu.

Wapo watu wengi waliokuwa wema ambao wamefariki mwaka 2018 na tumebaki sisi ambao hatuwazidi kwa kitu chochote hao waliokufa.

 

Wamekufa mashehe, wachungaji, mapadri ambao wangesalia dunia mwaka huu 2019 pengine wangefanya kazi kubwa ya kulinusuru taifa letu na maovu.

Tunapotafakari haya tukumbuke kuwa tunaishi kwa huruma ya Mungu na kwamba siku moja tusiyoijua tutakufa kwa sababu tumeambiwa na mtunzi kuwa kufa ni lazima na ndivyo ilivyo!

Baada ya kuona hilo suala la kuishi kwa huruma, mashairi ya wimbo wa Huruma kwa Wagonjwa yanatukumbusha hili pia:

Ni vizuri wana ndugu kupanga mikakati, kuchangia kuokoa maisha yao,

Ili kuokoa vifo, vifo kwa jamii , visitokee

 

HURUMA…

NANI KAUONA MWAKA, KAMALIZA MWAKA NI MAJALIWA YAKE MUNGU EE KUUONA MWAKA

Ni vizuri ndugu kuweka vikao na kujadili gharama za matibabu kuliko kuwatelekeza bila msaada wowote yatupaswa kutetea maisha yao, wanapokuwa wanaumwa.

 

NANI KAUONAMWAKA…

Badala yake mnaonyesha ufahari msibani na makamera ya video mazishini

NI MAJALIWA YAKE…

Tabia hiyo jamani kibinadamu, haifai

NI MAJALIWA YAKE…

Ni kweli kabisa siku hizi ukiona ndugu wamekusanyika mahali basi wanachangishana habari ya harusi au msiba, mambo ambayo si ya msingi sana kama kuokoa maisha ya watu.

Nadra sana kuwakuta ndugu wanajitolea kumhudumia mgonjwa, wengi wanapopata mgonjwa ndiyo wanazidisha ubize.

 

Wanakosa nafasi ya kuwatembelea wagonjwa na kuwafariji, ila wakisikia: “Mgonjwa wetu amefariki leo asubuhi.”

Utashangaa kuyaona magari ya kifahari yamekusanyika nyumbani kwa marehemu.

Hapo sasa ‘vigogo’ utawaona wanaingia kwenye mashindano ya kutoa michango.

Unabaki unashangaa, huyu mgonjwa kumbe ndugu zake ni matajiri namna hii, mbona hawakujichangisha wampatie matibabu bora zaidi?

 

Dede anatuambia mwaka 2019 tuache tabia hiyo ya kuonesha ufahari misibani, tujenge tabia ya kuokoa maisha ya watu kuliko kuwatelekeza mahospitalini.

Tumeaswa kuachana na kuufanya msiba kuwa na mbwembwe nyingi badala yake mbwembwe hizo zigeukie kwenye kusaidia wagonjwa waweze kupona.

Tuiache misiba iwe sehemu ya utukufu wa Mungu na si mashindano ya kiuwezo!

Comments are closed.