
MNUFAIKA wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Deus Anthony, ameushukuru Mfuko huo kwa kumuwezesha kuyamudu maisha licha ya kupata Ulemavu wa Kudumu uliotokana na Kazi.
Mnufaika huyo mkazi wa Morogoro ameyasema hayo leo Aprili 27, 2023 kwenye Maonesho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwenye viwanja vya Tumbaku mjini humo.
“Nilikatika mguu wa kushoto wakati nikiwa kazini mwaka 2017, WCF wamekuwa na mimi katika matibabu hadi kupona.”
Alisema hawakuishia hapo, “Nilipata Ulemavu wa Kudumu, wameninunulia mguu wa bandia naweza kutembea vizuri bila ya shida yoyote,” amefafanua.
Bw. Deus ambaye wakati anaumia kazi yake ilikuwa ni udereva amesema pensheni ya kila mwezi anayolipwa na WCF ameweza kudunduliza na kununua bajaji.

“Nawashukuru WCF kwa kuniwezesha kuyamudu maisha, hivi sasa nafikiria kukodi shamba ili nilime maaharage huko Mikumi.” Amesema
Kuhusu ushiriki wa WCF kwenye Maonesho hayo yanayofanyika Kitaifa mjini humo, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar amesema pamoja na kulipa fidia Mfuko unalo jukumu la kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi lakini pia kutoa elimu kwa Umma;
“Na hapa ndio mahala pake, hapa tunakutana na wananchi, tunakutana na wafanyakazi lakini pia tunakutana na waajiri, hivyo hii ni fursa nzuri kwetu na kwa wadau wetu pia.” Alisema Dkt. Omar.
Alisema katika banda la WCF wanatoa Elimu ya Fidia kwa njia mbalimbali ikiwemo michoro inayoonyesha tofauti ya viwango vya Ulemavu vinavyotumika kulipa fidia.
Aidha Meneja Tathmini na Usalama mahali pa Kazi WCF, Bi. Naanjela Msangi amesema katika kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi wanatoa Elimu kwa nadharia lakini pia kuna vifaa mbalimbali vya kujihami dhidi ya majanga kazini.
“Tunaonyesha vifaa sahihi vya kujihami kama vile mask (N95) kuzuia vumbi (normal dust), mask za kuzuia vumbi lenye kemikali, full face, Kifaa cha kupima viwango vya kelele maeneo ya kazi, kupima viwango vya mitetemo mwili mzima na mikono, kifaa cha kukinga kelele (ear muff), safety boots, reflectors na overall, hand gloves.” alifafanua.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi hufanyika Aprili 28 kila mwaka ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuiadhimisha siku hii, lengo kubwa ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu katika sehemu za kazi ambapo kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwakam huu ni “Mazingira salama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.”.
