The House of Favourite Newspapers

Nay unatamba una bilioni moja, so what?

0

MR NAYEMANUEL Elibariki ‘Nay wa Mitego’ ni mmoja kati ya wasanii wa Hip Hop ninaowakubali. Ni vile tu ametokea kipindi ambacho siwezi kwenda kwenye shoo na kuburudika pamoja naye. Zipo sababu nyingi zinazosababisha hali hii, lakini kubwa ni wakati.

Huwezi kuwa ulicheza disco la kina Lady Madonna, Michael Jackson, Lionel Richie, Shaba Ranks na wenzao wa kizazi hicho, halafu leo ukaenda Dar Live kujirusha ngoma za kina Ommy Dimpoz, Jux na Vanessa Mdee, labda kama utakuwa na sababu maalum.

Ingawa wakati unanitaka nitulie niwaache vijana, masikio hayaachi kupokea vitu vinavyozungumzwa katika nyimbo za Bongo Fleva. Mimi ni shabiki mzuri wa muziki unaobeba mashairi yenye kuakisi kile mwimbaji anachokiamini.

Ndiyo maana ninawakubali wasanii ambao wakati mwingine muziki wao hauchezeki, ingawa pia ninahusudu ngoma ambazo hata sielewi kinachozungumzwa, lakini zina beats nzuri ukiwa pale ‘dancing floor’.

Nina orodha ndefu ya wana Hip Hop wa Bongo ninaowakubali na kama nilivyosema mwanzo, Nay wa Mitego ni miongoni mwao. Kwangu ninamuona anafanya vizuri, anaitumia sanaa kuelezea hisia zake zinazowakilisha jamii inayomzunguka, vitu ambavyo vilimpa jina na heshima 2 Proud wakati ule alipofanya kazi zilizoonekana kama ni za hatari!

Na katika kumkubali huko, simaanishi kila anachokifanya kinanipendeza, kwa sababu katika hulka ya binadamu, haiwezekani kumridhisha kila mtu, hata awe mzazi wako. Hata hivyo, kutofautiana kimawazo, kimtazamo au hata kiitikadi, haijawahi kuwa kosa, kwani hili ndilo lililozaa msemo tunaouheshimu, kukubaliana kutokukubaliana!

Juzikati Nay alifanya mahojiano na kituo kimoja cha redio na miongoni mwa mengi aliyozungumza ni pamoja na kutaja thamani ya vitu anavyovimiliki. Majumuisho yake yakaonesha kuwa mkali huyo wa Kibao cha Shika Adamu Yako, ana mali zenye thamani ya shilingi milioni elfu moja, au kwa lugha rahisi, bilioni moja!

Kauli yake imepokewa kwa mitazamo tofauti sana, hasa kwenye mitandao ya kijamii. Kuna wanaokubali na kukataa, kila mmoja kwa vigezo vyake. Kwangu siwezi kubisha kama Nay hana vitu hivyo, kwa sababu kwa kipato anachokipata ni rahisi kuzifikia.

Tatizo langu ni sababu na haja ya Nay wa Mitego kusema kuhusu hicho anachomiliki. Na hii siyo kwa sababu nyingine zaidi ya usalama wake. Kibongobongo, shilingi bilioni moja ni fedha ndefu sana, hata kama tunajua siyo taslimu.

Wabongo wengi ni watu wa ajabu, kwani licha ya uvivu wao katika kuhangaika kuboresha maisha yao, pia ni wenye kupenda njia za mkato kufikia mafanikio. Kijana mdogo kama Nay ana magari matano katika maegesho yake, watu hawaoni hatari kuvamia ili kuyachukua, bila kujali kama mwenye nyumba ana silaha, au magari yote ni mabovu!

Vijana wa sasa wa Muziki wa Kizazi Kipya wengi wamejaa majivuno yanayotokana na ushamba wao. Mtu ana Krismasi mbili au tatu mjini, ametoa wimbo mmoja ume-hit, pesa inaingia kwa wingi, anaanza dharau na kujiona yeye ndiyo yeye. Wabongo hawapendi!

Ni hapa ndipo kauli za Nay zinapoweza kumuathiri, maana kama una mali za bilioni moja na magari matano ni wazi pia kuwa huwezi kosa laki tano katika dash board ya gari yako. Watu watakuvizia na kukudhuru bure wakati huenda hata mafuta uliyoweka, kesho hayalitoi gari kwenye maegesho!

Ni jambo jema kwamba maneno yake yanaweza kuwapa watu wengine usongo wa kuzidisha bidii, lakini mara zote tunapaswa kuwa waangalifu na aina ya maneno ya kuongea, kwa sababu sote ni mashahidi kuwa tunao ‘mabilionea’ wa kutosha hapa mjini, lakini wako kimya kama hawapo!

Leave A Reply