The House of Favourite Newspapers

Ndoa na Shetani 30

0

ILIPOISHIA:
“Jamani mbona mmekuwa na maneno mazito hivyo au hamkupenda niwe hivi, basi ili kuonesha sipo kwa ajili ya utumwa wa pesa. Nitarudisha kila kitu cha Papaa ili tuendelee na kazi yetu,” nilisema vile kuwapima lakini hata siku moja hakuna anayeingia peponi akarudi duniani kwenye shida zisizoisha kila kukicha afadhali ya jana.
“Hapana Konso hatuna maana hiyo!” alisema Sipe.
SASA ENDELEA…

Kwa kweli furaha niliyokuja nayo yote imeyeyuka kama bonge la barafu kwenye kikaango cha moto,” nilisema kwa sauti ya unyonge baada ya kuona shoga zangu walivyokosa raha baada ya mimi kuonekana maisha nimeyakatia denge (njia ya  mkato).
“Jamani kwanza tumefanya makosa badala ya kumkaribisha tumefikia kumshangaa, Konso tusamehe si unajua maisha yetu yalivyo ni watu tuliokata tamaa. Tulichokiona leo sawa na kuona meli ikipita barabarani badala ya majini, japo kila kitu chini ya jua kinawezekana kwani hao waliopata wana nini na sisi tuna nini.
“Narudia tena shoga tusamehe sana, inawezekana kauli zetu tumezisema vibaya ila hatuna kitu chochote kibaya, siku zote tumekuwa tukikuombea upate. Konso hujawahi kutuacha kila ulichokipata ulikitoa kwetu. Tuna imani wewe huenda ukawa mkombozi wetu,” Sipe alisema kwa uchungu huku machozi yakimtoka.

Nilijikuta naingiwa huruma na kwenda kumkumbatia huku nikimfuta machozi.
“Basi da’ Sipe yameisha, nimekuelewa sana, jamani ninyi ni zaidi ya ndugu zangu kwa muda mfupi tumeonesha mapenzi mazito zaidi ya ndugu, kila jambo lilipomkuta mmoja wetu lilikuwa letu sote. Kama nilivyosema kuwa mafanikio yangu ninyi mna sehemu kubwa sana. Nafikiri hamkutakiwa kunishangaa zaidi ya kuniuliza safari yangu ya jana iliyoambatana na dua zenu imekwendaje? ”
“Basi tuingie ndani,” Doi alisema.
Nilifunga gari langu kwa rimoti na kufanya Bahati aseme:
“Mambo ya Wazungu hayo!”
“Bahati haya mambo kwangu si mageni, Doi anajua.”
Tuliongozana hadi ndani kila mtu akiwa na shauku kutaka kujua nimekuja na habari gani. Baada ya kila mmoja kutulia niliwaeleza wito wao kwa Papaa japokuwa sikutaka kuwaeleza kitu kutokana na masharti mazito niliyopewa ambayo yaliutikisa moyo wangu.  Niliwagusia tu kuna kazi wanataka kupewa huku nikiwapa matumaini.
“Jamani Papaa amesema kazi ikienda vizuri basi nasi tutasahau biashara ya kuuza mwili.”
“Mmh! Anataka kutupa biashara gani?” aliuliza Doi.

“Kwa kweli biashara hiyo mimi siijui.”
“Ushindwe kuijua wewe mhusika kama tunakwenda kuchunwa ngozi je?” Bahati alihoji.

“Jamani mimi nimetumwa na kupewa ahadi hiyo, hakuna kitu kibaya.”
“Kwa hiyo tunatakiwa lini?” Sipe aliuliza.
“Yaani nikitoka hapa mguu wangu mguu wenu mpaka kwa Papaa.”
“Makubwa, haya ngoja tukaoge tuje tutafute nguo ya sikukuu ili tukukaribie,” alisema Bahati.
“Mimi naona nitamwaga nguo zote mnisaidie kuchagua moja kali maana leo tunakwenda kivingine tofauti na siku za nyuma ambapo tungekwenda hata na nguo za ndani tu hakuna wa kutushangaa wala kutuuliza. Lakini leo inatakiwa tuwaoneshe kazi ya kuuza utamu wetu ni dhiki lakini wenyewe tunafaa kwa kazi za maana,” alisema Sipe.
“Na kweli leo lazima tuwaoneshe sisi ni watu wengine, tuvae nguo nzuuuri za heshima,” alimalizia Doi.

Kila mmoja alimaliza yake, mimi nilikaa kimya nikiwasikiliza sikutaka kuongeza neno.  Baada ya kila mtu kuoga na kuvaa nguo nzuri ya heshima, hakika niliamini mtu unavyojiweka ndivyo utakavyokuwa. Mashoga zangu walipendeza kuliko siku zote zilizowahi kuwaona.
“Waaaooo jamaniii mmependezaje?”
“Asante, lakini hatukushindi wewe.”
“Wasiwasi wenu tu.”
“Hakika leo tumependeza kama tunakwenda kuonana na mkuu wa nchi,” Sipe alisema huku akitengeneza nywele zake mbele ya kioo kikubwa. Kila mmoja alirudia zaidi ya mara mbili kujitazama kwenye kioo kikubwa kupata uhakika kama kapendeza.
Baada ya zoezi lile tuliongozana na kuondoka zetu. Tulipofika walipokelewa kwa heshima zote, ilikuwa tofauti na tulipokwenda kibiashara. Kwa vile mimi ndiye niliyekuwa mwenyewe wao niliwakaribisha sebuleni:
“Jamani karibuni sana wageni wangu.”
“Asante mother house,” walijibu kwa pamoja.
“Jamani nakuja,” niliwaacha na kwenda chumbani nilipokuwa nimemuacha Papaa nikamjulishe watu wake wamefika.
Nilimkuta akiwa bize na mtandao, nilipoingia aliacha na kunigeukia.
Usikose mwendelezo wake katika gazeti la risasi jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply