The House of Favourite Newspapers

chongo -31

0

Ilipoishia wiki iliyopita:
“Hapana, mimi naona tukutane na wadau wetu Jully na Mwani tupange namna ya kuifanya hii kazi haraka, maana naona kama tunaweza kuwahiwa, sina amani kabisa aisee,” Bata alimweleza mpenzi wake.
Sasa endelea

Simu zikapigwa na baada ya saa moja, vijana hao wanne walikuwa wamekaa kwenye mojawapo ya vibaa vidogo vinavyozunguka eneo la Leaders Club jijini Dar es Salaam, meza yao wakiwa wameisogeza mbali na wateja wengine wa kawaida.
“Huu mpango inabidi ukamilike haraka jamani, maana nimemuona Sule akiingia kwa Jerry, nina wasiwasi huenda nao wakawa wanatutafuta, huwezi jua,” Bata aliwaambia wenzake baada ya kila mmoja wao kuagiza kinywaji chake, huku kuku akiendelea kubanikwa jikoni.
“Ni kweli jamani, hii kazi lazima ifanyike haraka, maana kama kuwajua tumeshawajua na bahati mbaya nao wameshatujua, kwani tayari Mwani wewe ni mwenzao, wakishakuona na sisi, halafu wakajua ndiyo adui zao, rahisi kweli kutufikia,” Jully naye aliunga mkono maelezo ya Bata na kuwafanya wote waliobakia kutingisha vichwa vyao kuunga mkono.

Mjadala ukaendelea kila mmoja akitoa namna nzuri ya kuweza kuutekeleza mpango ule, ingawa wote walikubaliana kuwa jambo lile lazima lifanyike ndani ya wiki hiyo. Baada ya majadiliano marefu, mwishoni wakakubaliana kuwa Jully akalale kwa akina Mwani, akijifanya ni rafiki yake waliosoma wote zamani, ambaye hivi sasa anaishi mkoani, ili wapate muda wa kuingia ndani ya ile chemba ili kusoma mchezo.
Haikuwa tabu kwa wazazi wake Mwani kumpokea Jully, kwani licha ya kuwa walimuamini sana mtoto wao, lakini pia kwa umri wake, alikuwa anajitambua, hivyo kama atajiingiza katika mambo yanayoweza kumletea matatizo, angekabiliana nayo mwenyewe.
“Mammy, huyu ni rafiki yangu Jully, nilisoma naye primary Olimpio, lakini alihama na wazazi wake wakaenda Mwanza, yaani hatujaonana siku nyingi kweli, amekuja Dar kwa ajili ya usajili chuo kikuu, atakaa kwetu kama wiki moja hivi,” Mwani alimtambulisha Jully kwa mama yake, kitu kilichowafanya wote watatu wawe na tabasamu pana midomoni mwao.
Mama yake Mwani, ambaye kwa sababu ya elimu na ufanisi katika biashara zake hakuwa mtu wa kujali sana, alimkaribisha na kumtakia kila la kheri, ajisikie nyumbani wakati wowote. Jully alifurahi sana na muda mchache baadaye wasichana hao wawili wakaingia chumbani kwa Mwani.
**
Sule alishuka katika lifti akili yake ikiwa imeshabadilika, harufu ya damu ilikuwa ikisikika katika pua yake. Hali hii ilimtokea kila mara alipotaka kutoa uhai wa mtu na inapotokea hivi, huwa haiishi hadi awe ametimiza lengo lake.
Alipotoka nje ya jengo hilo akaenda garini kwake huku akiangaza eneo lote lakini hakuweza kumuona Bata. Hata hivyo, hakukata tamaa, aliamua kuipoteza siku hiyo akizunguka katika maeneo ya jirani akiamini atatokea, lakini haikuwa hivyo hadi ilipotimia saa kumi na mbili, alipompigia simu Twaha, akimfahamisha kuwa alikuwa njiani kuelekea Sinza, wakakubaliana.
“Ile stori ya yule dogo imenivutia sana, nawapenda watu kama wale wenye misukosuko ambao hawakubali kushindwa, natamani nimsikie nijue anavyojisikia baada ya kupona,” Sule alimwambia Twaha, walipokutana mnamo saa mbili usiku katika pub moja iliyo pembeni ya Barabara ya Shekilango huko Sinza.

“Yule dogo anapatikana, mimi kuna mshkaji mmoja ndiyo alinionesha, anafanya biashara ya kuuza viatu na nguo katika mitaa ile ya Samora na pale ndipo maskani yake kubwa, kama kesho ukikaa pale huwezi kumkosa, utamuona tu,” alisema Twaha, kichwani mwake akiwa hana lile wala hili.

Wakaendelea na vinywaji na mazungumzo yakahamia sehemu zingine, wakazungumzia kuhusu pambano kubwa la soka lilikuwa linafanyika mwishoni mwa wiki hiyo baina ya Simba na Yanga, kwani wote walikuwa wapenzi wa mpira wa miguu, Sule akimshabikia Mnyama na Twaha Kandambili.

Saa sita kamili za usiku, wawili hao wakaagana, Sule akaingia katika gari lake ili arejee nyumbani na Twaha naye akitafuta usafiri wa kumfikisha kwake, wote wakiwa wameburudika kiasi cha kutosha.
**
Saa mbili za usiku, Mwani na Jully walitoka, wote wakiwa wamevaa kaptura za jinsi na fulana zinazobana, nyeusi, wakazunguka nyumba mbili tatu, wakatokezea nyuma, sehemu ilipo chemba inayotokezea nyumba wanayoishi akina Jerry na mkewe!
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua inayoelekea ukingoni katika toleo lijalo.

Leave A Reply