The House of Favourite Newspapers

Ndoa ni chachu ya mafanikio, ukibugi imekula kwako!

0

700lovecouplerelationshipkisspassionsexmarriagedate.jpg

Leo nitazungumzia suala la mafanikio na namna mwenza wako uliyeamua kuingia naye kwenye maisha ya ndoa anavyoweza kusababisha aidha ukafikia malengo yako au akazima ndoto zako za mafanikio.

Nalazimika kuandika juu ya mada hii kutokana na yale ambayo nimekuwa nikiyashuhudia huko mtaani na kusikia pia kutoka kwa wasomaji wangu.

Yupo mfuatiliaji mmoja wa safu hii mkazi wa Arusha ambaye alijitambulisha kwangu kama Mama John. Huyu aliwahi kunipa kisa chake ambacho kimenisukuma kuandika juu ya mada hii.

Alisema: “Nilipohitimu kidato cha nne sikufanikiwa kuendelea na masomo. Mama yangu alinipatia mtaji na nikafungua duka la ‘cosmetics’. Niliamua kufanikiwa kupitia biashara hiyo, nikaifanya kwa nidhamu ya hali ya juu.

“Nilikuwa makini katika kila shilingi niliyoipata. Kutokana na mambo kuniendea vizuri, nikafungua na saluni kisha nikanunua gari na kiwanja. Mpaka naolewa, nilikuwa na mafanikio makubwa.

“Mwanaume aliyenioa alikuwa akifanya kazi benki. Nikakubali kuwa naye nikijua atanisaidia kwenye kusimamia biashara zangu. Tofauti na matarajio yangu, baada ya kuolewa nikagundua ni mume malaya na mfujaji wa pesa ile mbaya.

“Kumbe hata mshahara wake alikuwa akiutumia kwa mambo ya anasa na hata nilipompa lile jukumu la kusimamia biashara zangu, akawa anatumia pesa nyingi kuhonga wanawake na kunywea pombe.

“Sasa hivi biashara zangu zimekufa na nimekuwa tegemezi kwake, gari alipata nalo ajali akiwa kwenye starehe zake. Mbaya zaidi nikaja kugundua kuwa alikuwa na mpango wa kuuza hata kile kiwanja changu. Naichukia ndoa kwa kuwa nimechagua mume ambaye siyo sahihi na matokeo yake ndoto zangu za mafanikio zimeyeyuka.”

Nini umejifunza kupitia kisa hiki? Kwa kifupi ni kwamba usipokuwa makini mweza wako anaweza kukurudisha nyuma kimafanikio lakini pia ukibahatika, unaweza kushangaa ubavu wako unakuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yenu.

Kwa mfano, wapo wanawake ambao wao na starehe, starehe na wao, wao si watu wa kuwaza mafanikio. Mwanamke kama huyo akiolewa na mwanaume mwenye ndoto za mafanikio, atayumba.

Pesa zitaishia kwenye kununulia viwalo, kujichana na kujirusha kila wikiendi. Kwa mfumo huo wa maisha, mafanikio hayawezi kupiga hodi.

Lakini pia mwanamke anaweza kuingia kwenye ndoa na mwanaume asiye na malengo na mpenda anasa. Huyo naye hawezi kufanikiwa. Anaweza kuwa mtafutaji lakini pesa zake zikiingia ndani mume anachukua na kufanyia mambo yasiyo ya kimaendeleo.

Wapo wanaume wenye mawazo butu, wala hawawazi kuhusu mafanikio. Wewe mwanamke ukiolewa na mwanaume huyo, hata kama unawaza mafanikio, utashangaa na wewe unaishi ilimradi siku zinakwenda.

Ukifuatilia sana utabaini wapo wanawake ambao walikuwa na mafanikio yao lakini wenza wao wakawarudisha nyuma.

Leave A Reply