The House of Favourite Newspapers

Kilimanjaro Challenge Yazinduliwa; GGM, Tacaids Zapata Bil 1.5 Kudhibiti Ukimwi

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Faustine Ndugulile akizungumza katika uzinduzi wa zoezi la upandaji wa Mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019), na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka 2019 kwa ajili ya kudhibiti UKIMWI nchini.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile jana 4, Juni 2019, amezindua zoezi la upandaji wa Mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019), na kuendesha harambee iliyowezesha kupatikana zaidi ya Sh bilioni 1.5,  fedha zilizochangwa kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini.

 

Katika hafla hiyo alisema serikali inatarajiwa kupeleka bungeni muswada wa sheria wa kushusha umri wa kuridhia vijana kupata huduma za UKIMWI kutoka miaka 18 hadi miaka 15 ili kupunguza wimbi la maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI (VVU) hususani kwa vijana.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya Taifa ya Kuthibiti UKIMWI nchini (TACAIDS), kubainisha kuwa zaidi ya watu 200 hupata maambukizi mapya ya VVU kwa siku, huku kati yao vijana 80 wenye umri wa miaka 15 hadi 24 pia huambukizwa kwa siku.

Meneja wa Kili Challenge, Manace Ndoroma (wa kwanza kushoto) katika picha ya pamoja na Dkt. Ndugulile (wa tano kushoto), Mkurugenzi wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko (wa nne kushoto), Makamu wa Rais Miradi Endelevu wa Kampuni ya Anglo Gold Ashanti, Simon Shayo (watatu kulia) pamoja na viongozi wengi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa zoezi HILO.

Kilimanjaro Challenge ni mfuko muhimu unaoratibiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Tume ya kuthibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikisha taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/ UKIMWI.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Ndugulile alisema tatizo la UKIMWI linabadilika kila mara hivyo kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya vijana kuathiriwa huku asilimia 80 ya vijana hao wakiwa ni vijana wa kike.

 

“Serikali tumeanza kuliona hilo na kuchukua hatua, hatua ya kwanza kushusha umri wa kuridhia kwani ni kweli wanaanza kujamiiana wakiwa umri wadogo, takwimu zinaonesha kuanzia wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19, asilimia 27 ni wajawazito au wana watoto.

 

“Kwa hali hii ya maambukizi tumeamua kupeleka muswada bungeni kushusha umri wa ridhaa hadi miaka 15. Ili sasa iweze kuruhusu kijana kuweza kupata huduma, kwa sababu kwa sasa inabidi apate ridhaa ya mzazi au mlezi,” alisema Dk. Ndugulile.

 

Aidha, alisema wizara italeta mpango wa kuruhusu watu kujipima wenyewe ili kutoa motisha kwa akina baba kupima VVU. “Kama ilivyo kwa wanawake wanavyojipima ujauzito na kina baba watahamasika kujipima na naamini litawapa motisha,” alisema.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, DkT. Leonard Maboko alisema muswada huo ukipitishwa na kuwa sheria utasaidia vijana kupata huduma za UKIMWIkwa haraka bila ridhaa ya mzazi au mlezi kama ilivyo sasa. Alisema hadi sasa Tanzania inao watu milioni 1.5 wenye VVU ambao ni sawa na asilimia 4.7.

Mkurugenzi wa Makao ya Watoto Moyo wa Huruma – Geita, Sr. Adalbera Mukure akielezea namna kampeni hiyo, ilivyonufaisha kituo hicho na kuwezesha watoto zaidi ya 137 wanaolelewa katika kituo hicho kupata huduma mbalimbali ikiwamo elimu. Kulia kwake ni George Emanuel na kushoto ni Rosemarry Emanuel ambao ni baadhi ya watoto waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Kili Challenge jijini Dar es Salaam.

“Lakini maambukizo mapya yamepungua kutoka 80,000 miaka mine iliyopita hadi 72,000. Katika kundi hili watanzania 6000 wanapata maambukizo mpaya kwa mwezi na kwa siku ni 200,” alisema.

Aidha, alisema sababu za vijana kupata maambukizo zaidi ni kutoka kwenye utoto kwenda kwenye ujana.

“Hawajapata elimu sawasawa hivyo inakuwa rahisi kwake kufanya maamuzi ambayo hana taarifa za kutosha. Lakini pia vijana wa kike kutaka kupata vitu kwa haraka. Ndio maana tuna miradi ambayo inagusa kaya maskini kwa kuwasaidia kupata elimu ya ujasiriamali katika mikoa mitatu,” alisema.

 

Kutokana na tatizo hilo Makamu wa rais miradi endelevu wa kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo alisema kwa mwaka huu katika kampeni hiyo ya kuchangia afua za UKIMWI wamelenga kukusanya Sh bilioni mbili.

Hata hivyo, alisema hadi sasa tayari wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 1.5 sawa na asilimia 67 ya lengo la kampeni hiyo ya mwaka huu ambayo sasa inatimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake.

 

Alisema tangu kuanzishwa kwa Kilimanjaro Challenge, zimekusanywa zaidi ya Sh bilioni 13 ambazo zimenufaisha asasi na taasisi mbalimbali 50 zinazoshughulikia masuala ya UKIMWI.

“Lengo kuhakikisha maambukizi mapya yanatokomea na kufikia lile lengo la sifuri tatu,” alisema.

 

Alisema tangu kampeni hiyo ianzishwe watu zaidi ya 800 wamepanda Mlima Kilimanjaro, na mwaka huu wanategemea zaidi ya watu 80 wakiwamo waendesha baiskeli.

 

Aidha, Mkurugenzi wa Makao ya Watoto Moyo wa Huruma – Geita, Sr. Adalbera Mukure alisema tangu kituo hicho kifunguliwe mwaka 2006 kwa kuwezeshwa na GGM, kimeweza kuboresha maisha ya watoto mbalimbali.

Alisema kituo kimesomesha watoto 18 wa chekechea, shule za msingi, 70, sekondari 29, kidato cha tano na sita 8, vyuo vikuu wawili, mmoja chuo cha walimu, wawili wameajiriwa kwenye sekta binafsi na wawili bado hawajapata ajira.

Makamu Rais wa Mgodi wa dhahabu Geita (GGM), Simon Shayo (wa pili kulia) akikabidhi hundi ya Sh milioni 150 kwa Dkt. Ndungulile na Mkurugenzi Mtenda wa Tacaids, Dk. Maboko. Mchango huo unalenga kudhibiti maambukizi ya VVU.

“Tunaomba michango yenu ili kuwezesha ujenzi wa shule ya English medium ili kuwezesha watoto kusoma na hata watoto wa nje ya kituo kusoma na fedha zitakazopatikana kutumika kuendesha kituo,” alisema.

 

Meneja wa Kili Challenge Manace Ndoroma alisema bodi ilikaa na kuamua kuwa mwaka huu zitatolewa Sh milioni 800 ambazo kati yake Sh milioni 550 zitabakia kusubiri maombi ya asasi mbalimbali zitakazowasilisha maombi yao.

 

“Sh Milioni 150 zitaenda Tacaids kujenga vituo vyta huduma za ukimwi. Sh Milioni 50 moyo wa huruma kuwezesha kituo kiuchumi Sh milioni 50 zitakwenda kwa mfuko waUKIMWI (ATF) wakati Sh bilioni 1.173 zilizotolewa na GGM zitaenda Kili Trust Fund,” alisema.

 

NA MWANDISHI WETU

 

JPM Atoa BODABODA kwa Maafisa TARAFA – “Zitumike kwa Kazi tu”

Comments are closed.