The House of Favourite Newspapers

NEC Yatangaza Uchaguzi Jimbo la Kuchauka Aliyetimkia CCM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Jimbo la Liwale Mkoa wa Lindi, kufutia kujiuzulu kwa alieyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Zuberi Mohamed Kuchauka aliyetimkia CCM hivi karibuni.

 

Kujiuzulu kwa Mbunge huyo ambaye alijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kunamfanya apoteze sifa ya kuwa mbunge na hivyo kulifanya jimbo hilo kuwa wazi.

Akitangaza uchaguzi huo Jijini Dar es Salaam leo Agosti 25, 2018, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage amesema tangazo la uchaguzi linakuja baada ya Tume kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza juu ya ratiba ya uchaguzi huo mdogo, jaji Kaijage alisema, kutoa fomu za uteuzi itakuwa kati ya tarehe 07 hadi 13 Septemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 13 Septemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 14 Septemba na kumalizika tarehe 12 Oktoba mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe 13 Oktoba mwaka huu.

 

“Tume inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, miongozo, na maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi huo mdogo,” Jaji Kaijage amesema.

Comments are closed.