The House of Favourite Newspapers

NGOMA 10 Zilizotazamwa Zaidi Hadi 2018, Video Zipo Hapa

YOUTUBE ni mtandao wa kijamii wa kuweka na kutazama video za vitu mbalimbali zikiwemo za matukio ya kila aina bila kusahau muziki kutoka kona mbalimbali za sayari hii ya dunia yenye zaidi ya watu bilioni 7. Makao Makuu ya YouTube yapo San Bruno, California nchini Marekani.

Uzuri wa YouTube mwanangu unakula vitu ndani ya dakika sifuri baada ya kupostiwa ilimradi tu uwe na simu janja na bando.

 

Soma hiyooo! Wenye mtandao wao wana kipengele kinachoitwa ‘the most viewed video’ (video iliyotazamwa zaidi). Hapa huwa wanaorodhesha video zote zilizopata watazamaji (views) wengi hasa zile za muziki na kuacha mshangao kutokana na mwitikio wa watu.

Hadi Desemba, 2018, kuna video ambazo ziliendelea kuweka rekodi ya kutazamwa tangu zilipowekwa kwenye mtandao huu huku zikijizolea mabilioni ya watazamaji. Zifuatazo ni video kumi (10) za muziki zilizopata watazamaji wengi zaidi duniani kwa kipindi chote tangu zilipowekwa kwenye mtandao huo na kutoa burudani ya aina yake kwa watazamaji wake;

 

1: DESPACITO

Hii ni ngoma ya karne. Inamilikiwa na mwanamuziki kutoka nchini Puerto Rico aitwaye Luis Fonsi aliyomshirikisha Daddy Yankee naye wa Puerto Rico. Ilipandishwa kwenye Mtandao wa YouTube Januari 12, 2017 ambapo hadi Desemba, 2018, imetazamwa na zaidi ya watu bilioni 5.82 duniani kote. Kumbuka dunia hii ina watu zaidi ya bilioni 7 hivyo imebakisha kutazamwa na watu bilioni mbili tu iwe imetazamwa na dunia nzima!

2: SHAPE OF YOU

Video ya wimbo huu ni ya mwanamuziki Ed Sheeran wa Uingereza ambayo ilipandishwa mtandaoni Januari 30, 2017. Imetazamwa na zaidi ya nusu ya watu wote duniani. Hadi Desemba, 2018 imefikisha watazamaji zaidi ya bilioni 3.97 duniani kote.


3: SEE YOU AGAIN

Hii ni video ya wimbo wa rapa wa Marekani, Wiz Khalifa
aliyomshirikisha mwimbaji Charlie Puth, naye kutoka Marekani. See You Again ilipostiwa kwenye mtandao huo Aprili 6, 2015. Hadi Desemba, 2018 imetazamwa na watu zaidi ya bilioni 3.92 duniani kote.


4: UPTOWN FUNK

Video ya ngoma hii inamilikiwa na mwanamuziki Mark Ronson wa Uingereza akimshirikisha Bruno Mars wa Marekani. Imetazamwa na zaidi ya watu bilioni 3.39 baada ya kupostiwa kwenye mtandao huo Novemba 19, 2014.


5: GANGNAM STYLE

Video hii ni ya rapa wa Korea Kusini aitwaye Psy. Ni moja ya video zilizotikisa dunia hii kutokana na staili ya jamaa huyo ya kucheza. Iliwekwa kwenye mtandao huo Julai 15, 2012 na mpaka sasa imetazamwa na watu zaidi ya bilioni 3.25.

 

6: SORRY

Hii ni video ya dogo kutoka Canada anayefanyia kazi zake nchini Marekani, Justin Bieber. Video hiyo ilipostiwa kwenye YouTube Oktoba 22, 2015. Imetazamwa na watu zaidi ya bilioni 3.05.


7: SUGAR

Video ya Sugar ni mali ya wanamuziki wa Pop wa Marekani waitwao Maroon 5. Ilipandishwa kwenye Mtandao wa YouTube Januari 14, 2015. Hadi Desemba, mwaka huu, Video ya Sugar imetazamwa na watu zaidi ya bilioni 2.84.


8: SHAKE IT OFF

Ni bonge moja la video kutoka kwa mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa kutoka nchini Marekani, Taylor Swift. Video hiyo ilipostiwa kwenye mtandao huo Agosti 18, 2014 na tayari imetazamwa na zaidi ya watu bilioni 2.70.


9: ROAR

Roar ni video ya ngoma ya mwanamuziki mkubwa wa Marekani, Katy Perry. Video ya Roar ilipostiwa kwenye YouTube Septemba 5, 2013 na hadi sasa imetazamwa na zaidi ya watu bilioni 2.69.

 

10: BAILANDO

Ni video ya staa wa Kihispania, Enrique Iglesias aliyowashirikisha waimbaji kutoka Cuba, Descemer Bueno na Gente De Zona. Video ya ngoma hiyo iliyopandishwa kwenye Mtandao wa YouTube Aprili 11, 2015, hadi Desemba, mwaka huu imetazamwa na zaidi ya watu bilioni 2.66.

Comments are closed.