Nilimpa kilema mtoto wa tajiri!-3

Ilipoishia wiki iliyopita

“Walinihimiza sana kutofanya mchezo na kibarua changu, walinitaka kuwa mvumilivu na mwenye nidhamu. Kila nilipowaambia kuhusu manyanyaso niliyoanza kufanyiwa, waliniambia ni mambo ya kawaida na yataisha, kwani kama yule mama angekuwa na tabia hiyo angeionesha tangu mwanzoni.

Sasa endelea…

Ndani ya mwaka mmoja, binti huyo anasema alijikuta ameshazoea manyanyaso, kwani kwa kadiri alivyokuwa akiwasiliana na wazazi wake na kuwasimulia na wao kumhimiza kuwa mvumilivu, akaamua kuyafanya maisha yake kuwa ya aina hiyo, ya kusimangwa, kutukanwa na kunyanyaswa.

“Nilifanya kazi katika mazingira hayo kwa miaka mitatu zaidi ambapo mama huyo alijifungua tena mtoto wake wa tatu, ambaye alikuwa mvulana na alipewa jina la Kei. Nikaendelea na kazi yangu ya kumlea Kei kama kawaida.

“Mtoto alipofikisha umri wa miezi kumi na moja, yule mama akaanza tena safari zake za kutoka usiku na kurejea alfajiri na maneno yake ya kunidhalilisha yaliongezeka. Nilishindwa hata mtu wa kumweleza na kunipa ushauri kwa sababu nyumba tuliyokuwa tunakaa haikuwa na mpangaji mwingine zaidi yetu na kwa sababu hiyo sikuwa na marafiki.

“Siku moja nakumbuka yule mama alirudi nyumbani mapema, kama saa nne hivi usiku. Haikuwa kawaida yake maana alikuwa akiondoka saa moja anarudi alfajiri au asubuhi kabisa ya siku inayofuata. Alionekana kutokuwa sawa, maana alikuja na pombe, akaniita sebuleni.

“Akazungumza mambo mengi, lakini kilichoniuma ni pale aliposema eti amechoshwa na tabia za wazazi wangu kumpigia simu na kumuomba hela kila siku, hivyo kuanzia siku hiyo hatanilipa mshahara, kwa sababu hela anazowapa wazazi wangu ni zaidi ya mshahara, hivyo kama siwezi niondoke.

“Nilishangaa sana, wazazi wangu hawakuwahi kuniambia kama walikuwa wanampigia simu kumuomba hela, maana siku zote nilipopewa mshahara wangu mimi ndiyo niliwatumia wao ili waendelee na maisha.

“Nilikubali kufanya kazi bila mshahara, lakini kwa kweli haikutoka moyoni. Nilikuwa na uhakika kwa wakati ule, mtaji wa baba na mama ulikuwa mkubwa, hivyo ningeweza kurudi nyumbani na kuendelea na maisha kama kawaida, lakini sijui kitu gani kilichoniambia nibaki.

“Nilimuona yule mama kama mtu anayejiona sana, akanipa hasira, siku hiyo nililala nalia, yaani umaskini wa wazazi wangu ndiyo unitese kiasi hicho? Kesho yake jioni mama alipoondoka, nikawapigia wazazi wangu na kuwauliza kama kweli huwa wanapiga simu na kuomba hela.

“Mama yangu alisema aliwahi kumuomba mara moja tu, tena zaidi ya miezi sita iliyopita. Akaniambia kama amefikia hatua hiyo ni bora nirudi nyumbani, kwani kwa wakati huo maisha yao kidogo yalikuwa afadhali. Hata hivyo, akanikataza nisitoroke, bali niage vizuri.

“Nikamkubalia, lakini sikuona jinsi gani nitamwambia huyu mama kuwa naondoka akubali kirahisi. Ila nilidhamiria nimfanyie kitu kibaya ili kumkomesha. Siku kama tatu hivi baadaye nikafanya kitendo ambacho nakijutia hadi leo, kwa sababu nilimuadhibu mtu ambaye hakustahili.

“Baada tu ya yule mama kuondoka, nikaenda kumwamsha mtoto wake yule mdogo, Kei. Nikambeba mgongoni, nikaenda naye sebuleni, nikatazama huku na huku, nikalegeza khanga niliyomfunga, nikafumba macho nikamwachia mtoto akaanguka.

“Kishindo chake kilikuwa kikubwa sana hadi nikaogopa. Nikamchukua na kumbeba tena, akawa analia sana, lakini hakutoa damu. Nikambeba tena na kuanza kumbembeleza. Alilia usiku kucha. Mama yake alipokuja asubuhi akamkuta amelala.

“Lakini alivyoamshwa tu, akaanza kulia tena. Aliponiuliza ana tatizo gani, nikamwambia sijui. Siku mbili baadaye akamchukua na kwenda naye zahanati moja jirani, akaandikiwa dawa akawa anakunywa.

“Mimi nilikaa wiki mbili tu baada ya tukio hilo nikaondoka zangu kurudi nyumbani Mbagala. Nilikaa huko nikiendelea na shughuli zangu, miaka kama saba hivi baadaye nilikutana na yule mama akiwa na yule mtoto, mitaa ya Kariakoo.

“Kimuonekano, alionekana hakuwa na maisha mazuri kama zamani, baada ya kusalimiana nikamuona Kei akiwa na kichwa kikubwa sana, nilipouliza kulikoni, nikaambiwa akiwa mdogo, mshipa ndani ya kichwa chake ulipasuka na kwa kuwa hakutibiwa, ikasababisha kuziba na hivyo kutokua ipasavyo.

“Kei alionekana kama taahira hivi. Nilisikitika sana kwa sababu nilijua ni mimi ndiye niliyefanya ukatili ule, lakini zaidi nilimlaumu mama yake. Kila siku naomba sana kwa Mungu anisamehe, ninawaogopa sana wadada wa kazi, siwaamini kabisa, kama mimi niliweza kufanya vile, hata wao wanaweza.”

Mwisho.


Loading...

Toa comment