The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani -01

0

Nayainua macho juu, nautazama ulimwengu ambapo namuona kila mtu anatembea akiwa na yake mazito moyoni. Wengi aibu imetutawala kutoa yaliyo mioyoni kwa kuhofia aibu tutakayoipata, kwa watu kujua mambo ya aibu yaliyomo mioyoni mwetu.

Wengi tumeanzisha mahusiano na shetani bila kujua na mwisho wake kufunga naye ndoa kabisa na kuamini yote atuelekezayo ndiyo sahihi na kusahau kuna Mungu mwenye nguvu na wivu ambaye anatupenda na alituleta duniani kwa kusudi maalumu la kumuabudu yeye.

Hivyo, tunatakiwa kumsikiliza na kumfuata yeye na si kitu kingine kinyume na maamrisho yake ni makosa makubwa. Asikudanganye mtu, kuivunja ndoa na shetani yataka nguvu za ziada kwani si rahisi kutoka ndani ya ndoa ya shetani kwa vile huwezi kuona kitu chochote mbele yako, atakuwa amekupofua macho na kuiona taswira yake peke yake.

Dunia imekuwa ikiangamia kwa watu kufunga ndoa na shetani kwa tamaa ya kidunia kwa kuyatumia maneno ya Mungu kwa faida ya matumbo yao na si faida ya kuwakomboa wana kondoo. Neno la Mungu linatumika kama kisu kikali cha kujikatia nyama unayoitaka na si ukombozi kwa waliopotea.

Wengi tunawaamini viongozi wa kiimani lakini wamekuwa wakigeuza Neno la Mungu kama mradi kuliko kuwajenga waumini kiimani ndiyo kufia watu kumuona kiongozi fulani kama Mungu na kusahau yupo anayemuongoza yeye bila yeye yeye si kitu.

Kila kukicha makanisa yanaongezeka kila kona kwa dini kugeuzwa biashara baada kuvamiwa na watu wenye tamaa za kidunia. Walio kidunia huligeuza Neno la Mungu mtaji ukimuona mtu huyo jua tayari wameshafunga ndoa na shetani na kutoka yataka nguvu ya Mungu peke yake.

Pamoja na umri wangu mdogo nimeshuhudia mambo makubwa kila nikiyakumbuka moyo wangu hutetemeka kwa hofu. Hupiga magoti kumuomba Mungu anisamehe kwa kila ovu nililomtendea. Nimeshuhudia viongozi matapeli wakiwapotosha watu ambao wamekuwa wakiwaamini kwa kutumia kitabu kitakatifu kuponya lakini nyuma yake kuna uchawi mzito na kiini macho. Sisemi kwa kusikia bali nami nilikuwa mshiriki mkubwa kufurahia ndoa yangu na shetani.

Nakiri kuanza kupotea tangu nikiwa binti mdogo kutokana na kiburi huku nikiyadharau malezi na mafunzo mema toka kwa wazazi wangu ya kuwa niwe na tabia njema kwa kuwaheshimu wakubwa na wadogo huku msisitizo mkubwa ukiwa kumcha Mungu.

Heshima kwangu sikuona kazi kubwa lakini suala la kumcha Mungu na kuacha starehe za ujana niliona kazi kubwa. Siku zote niliamini ukimwona mtu anamfuata sana Mungu ujue maisha ya kidunia yamemshinda, hasa wazee ambao wakiona wamekaribia kufa hapo ndipo humrudia Mungu kwa nguvu kubwa tofauti na walipokuwa vijana.

Kiburi changu ndicho kilichosababisha kuanzisha uhusiano na shetani na hatimaye kufunga naye ndoa kabisa na kuwa wakala wake niliyetumika kupoteza watu ili kuongeza wafuasi aliokuwa akiwatafuta kila kukicha huku Mwenyezi Mungu akitumia kila awezalo kuwarudisha kundini wana kondoo walipotea kwa kutuletea mitume ambao walikuwa wokovu kwetu.

Kiburi cha kibinadamu ndicho kinachotuponza watu wengi, kama ilivyokuwa kwa Nabii Nuhu kuangamizwa na gharika. Kinachoendelea katika ulimwengu wa leo, moyo wangu umekuwa ukitikisika kwa hofu ya kuteremka gharika nyingine. Kwa umri wangu mdogo nimeona mambo mengi ambayo nataka niyatoe kama ushuhuda kwa wenzangu ili nanyi mvunje ndoa zenu na shetani. Huenda huijui ndoa hiyo, basi ungana nami ili kuijua ndoa yako na shetani na jinsi ya kuivunja.

Kwa jina naitwa Konsolata nimezaliwa miaka 28 iliyopita ni mtoto wa nne katika familia ya watu watano nikiwa ni mmoja wa watoto wa kike wa famili ya mzee Joseph na mama yangu Mary.

Kwanza lazima nimshukuru Mungu kwa kuzaliwa katika familia iliyompokea Bwana kama mlinzi na mwokozi. Wazazi wetu walikuwa wacha Mungu wazuri sana, lakini ilikuwa tofauti na sisi watoto wao. Kwenda kanisani ilikuwa mbinde au kusingizia tunakwenda kanisani kumbe kwenye mambo yetu.

Pamoja na wazazi wetu kuwa wacha Mungu wazuri watoto wao tulikuwa hatukosi kwenye matamasha hata kumbi za starehe majira ya usiku kwa kutoroka.
* * *
Baada ya kumaliza kidato cha sita nilibahatika kwenda chuo kikuu, kwa kweli kwa upande wangu nilikuwa kama mfungwa aliyefunguliwa kifungoni. Kwa kupata muda wa kufanya mambo yangu ambayo wazazi wangu walikuwa wakinibana.

Nilikutana na shoga yangu ambaye tulikuwa tunakaa naye chumba kimoja, kwa kweli mwanzo mavazi yake yalinishinda yalikuwa ya nusu utupu na kumuona akitembea uchi. Lakini na yeye alinishangaa mimi kuvaa nguo ndefu kama mtawa.
“Konso utakatifu gani huo?”

“Kwa nini unasema hivyo?” nilimuuliza nikiwa simuelewi.
“Mavazi gani hayo, yaani umbile kama lako ningekuwa nalo mimi kila mtu angenisoma namba. Mungu amekupendelea ili uutangaze uwezo wake wa uumbaji ukilificha, usije shangaa siku moja ukasikia umekuwa mlemavu kwa kushindwa kuvitangaza…kwanza unajijua wewe mzuri?” niliuliza huku akinitazama.

“Nitajijuaje mwenyewe?”
“Ina maana kote ulikosoma hukuwahi kusifiwa?”
Je, kilifuatia nini? Usikose katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave A Reply