The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani – 6

0

ILIPOISHIA:

Siku moja usiku ilikuwa majira ya saa nne tukiwa tunajiandaa kulala na kipenzi changu Bantu. Mara nilipigiwa simu ambayo ilikuwa ya bwana yangu mmoja wa Kiarabu Abdul akinijulisha kuwa ameingia jijini usiku ule na ndege na hakuwa tayari kulala peke yake kwa hiyo alinitaka niende tukalale pamoja.

SASA ENDELEA…

Kwa kweli katika wanaume zangu ambao hunipa pesa nyingi ni Abdul ambaye hata lile gari la kifahari ninalotembelea amenipa yeye na alikuwa na mpango wa kuninunulia nyumba kubwa ambayo amesema ndiyo inalingana na hadhi yangu.

Sikuwa na jinsi kuondoka usiku ile japo tangu niwe na Bantu nimeshalala nje mara nyingi kwa kisingizio cha kazi nyingi. Bantu hakuwa na neno lakini nilikuwa sijawahi kuondoka nyumbani usiku tukiwa tumelala, wanaume wote wanaonipigia simu usiku niliwakatalia kwa kumheshimu Bantu.

Sikuwa na shaka nilinyanyuka na kwenda bafuni kuoga kisha kujipamba na kujipulizia manukato aliyoninunulia Abdul aliyokuwa akiyapenda. Wakati huo Bantu alikuwa bado amelala.

Nilipanga kama ataamka nitamuaga lakini akikuta sipo tutaongea asubuhi dawa yake ni kurudi na zawadi ambayo itamziba mdomo. Baada ya kujiandaa kila kitu wakati naweka mkoba wangu kwapani Bantu alishtuka usingizini na kunikuta nikiwa katika hali ya kutoka.

“Vipi mwenzangu mbona hivyo?” aliniuliza huku akinishangaa.
“Aa…aah, kuna simu nimepigiwa sasa hivi kuna mzigo umeingia unatakiwa kupakuliwa usiku huu,” nilitengeneza uongo.
“Mmh!” Bantu aliguna.

“Kweli Bantu usinifikirie vibaya, siwezi kukusaliti,” bila kujielewa nilijikuta nikijiingiza kizimbani mwenyewe.
“Siyo sikuamini bali muda mbaya kwa nini usiende kesho alfajiri?”
“Yaani muda huu ndiyo wameanza kupakua kibaya nimewaeleza kuwa naenda.”

“Basi acha nikusindikize usiku mkubwa huu, si vizuri uende peke yako,” Bantu alisema huku akinyanyuka kitandani ili anisindikize niliona mambo yameharibika kuongozana na Bantu. Hiyo mizigo nitamuonesha ipi na kweli Abdul atanielewa nisipokwenda wakati nilimuhakikishia nipo peke yangu na kumwambia tutakuwa wote muda wowote. Nilijikuta njia panda bila kutegemea nilipata wazo.

“Unajua nini Bantu?”
“Hata sijui.”
“Hizi dili zetu ni za magendo kwa hiyo huwa hatuendi na watu kwa kuogopa polisi.”
“Kwa maana hiyo unaniambiaje?”

“Acha niende peke yangu hakuna tatizo nitafika salama na kurudi salama.”
“Haya kama umesema mwenyewe mimi sina neno.”

Nilimshukuru Mungu kwa kuweza kumdanganya Bantu wakati huo simu ya Abdul ililia niliipokea na kuongea kwa sauti bila kuhofu kwa kujua lazima Bantu atajua ndiyo ninaofanya nao dili.
“Nakuja sasa hivi.”

“Wahi usijechelewa au kukuta vitu nusu si unajua raha ya kitu kipakuliwe ukiwepo,” Bantu alinihimiza niwahi bila kujua alikuwa anamtupia fisi mzoga.
“Acha niwahi,” nilimpiga busu Bantu na kumuwahi Abdul, nilikuwa nimempiga changa la macho kama wasemavyo watoto wa mjini.

Nilikwenda hadi nje kwenye gari langu na kwenda katika hoteli aliyofikia Abdul. Nilipofika alifurahi kuniona, akanikumbatia kwa furaha.
“Ndiyo maana nakuamini Konso kwa mtindo huu siwezi kukunyima chochote ukitakacho.”

“Nilikueleza ukweli kuwa nipo kwa ajili yako,” nilimpaka mafuta kwa mgongo wa chupa.
“Basi nikuoe kabisa.”
“Haiwezekani labda ubadili dini wewe.”
“Ulisikia wapi mwanaume anabadili dini?”

“Mara nyingi tu, kama kweli unanipenda badili dini unioe.”
“Mmh! Kwa mtindo huo itakuwa ngumu.”
“Basi tuendelee kila mmoja na dini yake.”

“Lakini Konso ungekubali nikuoe nitakupa zawadi kubwa sana ambayo ni zaidi ya kile ukifikiriacho kukipata maishani mwako.”
“Nipe muda.”

Siku hiyo tulilala mpaka asubuhi huku tukifurahia maisha, kwa kweli siyo siri uwezo wa Bantu kimapenzi aliwazidi wanaume wote niliokutananao. Wengi niliwapendea pesa zao wala si mapenzi. Ila Abdul yeye nilimpendea mapenzi ya moyoni mwake na kunipa chochote nikitakacho pia alikuwa mwanaume muelewa hakuwa tofauti sana na Bantu.
Tofauti yao ni pesa, Abdul anazo na Bantu hana kitu, kingine Bantu ana uwezo mkubwa kitandani, Abdul huwahi kuchoka.

Siku ya pili nilimuacha Abdul na kumuwahi Bantu ambaye nilimkuta amelala. Siku hiyo usiku tulipanga kukutana tena na Abdul mapema. Sikuwa na wasi nilijua nitamdanganya vipi Bantu. Alikuwa kama ndondocha asiyejua kitu kila kitu kwake sawa .
Kama kawaida nilimueleza Bantu kuwa jioni nitakuwa kwenye biashara kwa hiyo naweza kurudi kesho, kwa kujua hata kama Abdul hataondoka bado Bantu nitamdanganya. Kikubwa nilipanga kumnunulia gari dogo ambalo nilimuahidi pale anapoweka vizingiti vya mimi kutoka.

Japo mara nyingi huwa hanizuii lakini lazima niweke taadhari siku zote kuti la mazoea ndilo linalomuangusha mkwezi. Kama kawaida ilipofika majira ya mchana wakati huo tulikuwa tumelala nilimjulisha Bantu kuhusu mtoko wangu wa usiku.

“Mpenzi leo jioni ndiyo siku ya kufanya biashara ile ya jana usiku.”
“Mmh! Mbona hii imekuwa ya usiku?”
“Unakuwa kama mgeni, cha usiku mara nyingi huuzwa usiku ukiona mchana ujue hapa kupatikana kwa mchana.”

“Lakini mpenzi mbona kuna biashara uliishawahi kufanya usiku na kuiuza mchana?” Bantu alionesha machale kumcheza.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Jumatano siku ya Jumatano.

Leave A Reply