The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 70

1

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna, wote wakiwa ni wanafunzi wa sekondari mbili tofauti jijini Mwanza. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, anatoa figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa mpaka jijini Dar es Salaam anakoenda kulazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini hali inazidi kuwa mbaya, anapelekwa nchini India.

Akiwa hospitalini hapo, Anna anaanza kuwasumbua wazazi wake akishinikiza Jafet akaletwe. Baadaye, baba yake Jafet anafunga safari mpaka Tanzania na kumchukua Jafet, anafunga naye safari mpaka nchini India na hatimaye Jafet na Anna wanakutanishwa tena hospitalini hapo. Ndani ya muda mfupi tu, Anna anaanza kuonesha mabadiliko makubwa kwenye afya yake.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Taratibu wawili hao wakawa wanatembea kwenye bustani za maua, wakipiga stori za hapa na pale na kukumbushana mambo waliyowahi kuyafanya pamoja siku za nyuma, furaha kubwa ikatawala kwenye mioyo ya wote wawili.
“Unaona mwanao alivyochangamka ghafla?”

“Mh! Yaani huyu Jafet sijui anampa nini maskini! Huwezi kuamini kama ndiyo yule Anna wa saa kadhaa zilizopita. Nimeamini wanapendana sana lakini makosa niliyoyafanya mimi ndiyo yametufikisha hapa tulipo,” alisema mama yake Anna wakati wakiwatazama Jafet na Anna waliokuwa wakipiga stori na kufurahi pamoja.

“Umemkosesha mwanao nafasi ya kufurahi maishani mwake, hivi hata sijui ulikuwa unafikiria nini. Hujui kwamba furaha maishani ni muhimu kuliko hata fedha?”
“Jamani mume wangu, utaacha lini kunilaumu? Si nilishakubali makosa?”

“Basi tuachane na hayo mambo,” ilibidi baba yake Anna akatishe mazungumzo kwani kila walipokuwa wakizungumzia habari hizo, hawakuwa wakifikia mwisho mzuri.

Ukimya ukatawala kati yao wakati wakiwaangalia Jafet na binti yao, Anna wakiendelea kupiga stori za hapa na pale na kufurahi kwenye bustani za maua hospitalini hapo. Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye Anna akatakiwa kurudi wodini na wauguzi kutokana na hali ya hewa ya baridi iliyokuwepo nje.

Jafet akarudi naye wakiwa wameshikana mikono kwa furaha mpaka kitandani kwa msichana huyo. Akamsaidia kupanda kisha akamfunika vizuri, akakaa pembeni yake na kuendelea kumpigisha stori za hapa na pale wakati manesi wakimpa dawa za kutibu maradhi yake.

Mpaka saa nne za usiku Jafet alipokuwa anaaga kwa ajili ya kwenda hotelini alikofikia kupumzika, Anna hakuwa akitaka kumruhusu. Kama sheria zingekuwa zinaruhusu, alitamani walale wote wodini lakini hilo halikuwa likiwezekana. Jafet akaondoka na baba yake Anna mpaka kwenye hoteli waliyofikia.

“Nakushukuru sana kwa jinsi ulivyoweza kucheza na akili za Anna, huo ndiyo uanaume wenyewe, nakuomba uendelee hivyohivyo,” alisema baba yake Anna, wote wawili wakacheka na kugongesheana mikono kwa furaha, wakaendelea kuzungumza mambo mbalimbali.

Muda mfupi baadaye, walitoka na kwenda kwenye mgahawa uliokuwa ndani ya hoteli hiyo waliyofikia ambapo walipata chakula cha usiku pamoja huku mzee huyo akimueleza Jafet mambo mengi ya kuzingatia maishani.

Baadaye waliagana, Jafet akarudi kwenye chumba chake, mzee huyo naye akaelekea kwenye chumba chake kupumzika. Siku hiyo ilipita vizuri, kesho yake asubuhi wakawahi kuamka na kuongozana mpaka hospitalini ambako walimkuta Anna akiwa ameshaamka na ameanza kumsumbua mama yake akitaka Jafet akaitwe.

Kama ilivyokuwa jana yake, Anna alifurahi sana kumuona tena Jafet. Japokuwa siku za nyuma alikuwa akisumbua kutokana na kukataa kula, siku hiyo hakusumbua kabisa. Kifungua kinywa kilipoletwa, alikula na Jafet mpaka wazazi wake wakafurahi.

Walishinda pamoja kutwa nzima, wakala chakula cha mchana na kushinda mpaka jioni huku muda mwingi Anna akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

aisha yaliendelea hivyo na siku chache baadaye, madaktari waliokuwa wakimtibu msichana huyo, waliitana katika kikao cha dharura kujadiliana kuhusu maendeleo ya mgonjwa wao.

“She is recovering in a way that is difficult to explain, i have never seen such a condition.”
(Anapona haraka katika namna ambayo ni ngumu kuielezea, sijawahi kuona hali kama hii.)
“Even destroyed cells of a transplated organ seems to start to recover in a high speed. If this will continue like this, there will be no any need of another transplant or dialysis,” (Hata seli zilizoharibika kwenye figo aliyopandikizwa zinaonesha kurudi kwenye hali yake kwa kasi kubwa. Kama hali itandelea namna hii, hakutakuwa na haja ya kubadilishiwa tena figo wala kuendelea na Dialysis) alisema Dokta Priyanka na kuungwa mkono na wenzake.

Kila mmoja alishangazwa sana na kilichokuwa kikitokea kwenye figo za Anna, ndani ya siku chache sana tayari alikuwa na ahueni kubwa kuliko hata madaktari walivyofikiria. Wazazi wa Anna walipopewa taarifa hizo, walishindwa kuficha furaha kubwa waliyokuwa nayo. Hakuna aliyetegemea kama anaweza kupata ahueni haraka kiasi hicho.

“Kwa hiyo inawezekana pia kuwa maradhi yake yanasababishwa sana na matatizo ya kisaikolojia?”
“Hata mimi mwenyewe nahisi hivyo kwa sababu hakuna dawa yoyote ya tofauti aliyopewa ambayo tunaweza kusema ndiyo imesababisha apate ahueni kubwa namna hii. Uwepo wa Jafet ndiyo uliosaidia,” baba na mama yake Anna walikuwa wakijadiliana baada ya kupelekewa majibu hayo.

Madaktari nao hawakuishia hapo, kwa jinsi msichana huyo alivyopata ahueni kubwa ndani ya kipindi kifupi, waliamini lazima kuna jambo wanalopaswa kujifunza ili kuwasaidia watu wengine wenye matatizo kama ya Anna waliokuwa wakiteseka kwa kutumia dozi kubwa za madawa bila mafanikio yoyote.

Kwa kushirikiana na wataalamu wa mambo ya saikolojia, walianza kumfuatilia Anna kwa karibu, wakati mwingine wakimuuliza maswali mbalimbali huku pia wakiendelea kufuatilia afya yake kwa karibu.

Katika uchunguzi wao, walibaini kwamba uwepo wa Jafet ndiyo uliochochea sana maendeleo mazuri ya afya ya Anna na wakatoa ushauri kwamba ili afya yake iendelee kuimarika, lazima aendelee kuwa naye karibu.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

1 Comment
  1. hanifa mwinyi says

    Ya kale hayanuki

Leave A Reply