The House of Favourite Newspapers

Nilivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi -10

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA

Akili yangu ilifanya kazi haraka na kujiuliza, ‘huyu panya anaishije kwenye shimo hilo refu? Je, inawezekana hutoka nje kupitia lile tundu lililotumika kutushushia sisi humu?”
Jibu sikupata kwa sababu panya mwenyewe hayupo kaingia shimoni lakini hata kama angekuwepo nisingeweza kumuuliza kwa kuwa ni panya.
Nilisimama na kwenda kuangalia lile tundu aliloingia panya, akili zikanituma kwamba utafiti wangu uanzie pale.

SASA ENDELEA:
Nilisimama kwenye lile tundu kwa dakika tano hivi, wenzangu wakawa wananiangalia wasijue nilikuwa nawaza nini.

“Mbona kaka Namakoto unaangalia tundu la panya kisha huseni lolote?” alinihoji Kwiimuka.
“Nadhani wote au baadhi yenu mmemuona panya hapa.”
“Ndiyoo,” waliitikia baadhi ya vijana niliotupwa nao kwenye shimo lile la kifo.
“Nani ana wazo kuhusu panya huyu?”
Kimyaa. Ukimya wao ulinifanya nigundue kuwa hakuna mtu mwenye mawazo, walimuona kama walivyokuwa wanamuona tukiwa nje ya pango lile.
“Hamuoni kuwa panya huyu anaweza kutuokoa?”
“Kivipi?” aliuliza tena Kwiimuka.
“Huyu panya kwa mawazo yangu naamini anatoka nje ya shimo hili na inawezekana huwa anakwenda kujitafutia chakula nje ya pango hili.”
Baada ya kusema hayo kuna baadhi ya wenzangu walikasirika, bila shaka waliona wazo langu ni la kipuuzi na nawapotezea muda.
Lakini nilijiuliza kupoteza muda ili wafanye nini kwa sababu sikuona hata mmoja ambaye alikuwa na wazo lolote la kuweza kujiokoa.
“Sasa kaka Namakoto unafikiri panya huyu kachimba shimo hadi bustani ya Nangose?”
Kabla sijajibu mwingine akadakia:
“Sasa hata kama huyu panya kachimba shimo kutoka bustani ya Nangose, sisi tunaweza kupita katika tundu lake?”
Huyu wa swali la pili nilimuona kama alitaka kuelekea kule nilipokuwa nawaza, lakini akashindwa kufikiri zaidi.
“Niwaambieni jambo?” nilianza kuongea nao, nikanyamaza kidogo ili kumeza mate.
“Huyu panya inawezekana ni Mungu ameamua kutuonesha ili kutuokoa, mnasemaje?”
“Atatuokoaje?” aliuliza msichana mmoja.
“Sikiliza. Ni lazima tutumie mifupa ya watu waliotangulia waliotupwa humu ili kujinasua. Wazo langu ni kwamba tuchimbue kufuata njia hii ya panya. Tuchimbe taratibu na kwa bidii naamini tutatoka nje ya pango hili. Kuna mwenye swali?”
Wote nikawaona wanakunjuka sura zao na kuonesha nyuso za matumaini.
“Ni wazo zuri na hiyo kazi tuianze sasa hivi,” alichombeza kijana mmoja aliyekwenda moja kwa moja kuchukua mfupa wa maiti na kuja pale kwenye shimo la panya.
Kazi ya kuchimbua haikuwa ngumu sana kwa sababu udongo ulikuwa tifutifu na hali hiyo ilitushangaza.
“Hapa inavyoelekea shimo hili lilikuwa likitumika zamani kwa kazi fulani na hii ilikuwa njia ya watu kufika shimoni,” nilisema.
“Lakini sasa kwa nini walifukia?” mwingine alihoji.
“Huwezi kujua labda walikuwa na sababu maalum, labda za kivita enzi hizo. Inawezekana walikuwa wakijificha watu hapa wakiona maadui enzi hizo za ujima,” akadakia kijana mwingine.
“Msifurahie jamani, huwezi kujua, panya anaweza kupita katikati ya miamba iliyoungana, hivyo, tutafurahi kama tutatoboa juu ya ardhi,” nilisema na baada ya kutamka hivyo nyuso za watu niliona zimekunjamana.
“Sisemi hivyo ili kuwakatisha tamaa, la hasha. Nataka tuzidi kumuomba Mungu ili tusikutane na mwamba ambao utatuzuia kuendelea na kuchimba njia,” niliona niwape moyo.
Kazi ilikuwa ngumu kwa sababu ilikuwa ni kufa na kupona. Kwamba tukifanikiwa kutoboa ardhi itakuwa ndiyo kupona kwetu na tusipofanikiwa itakuwa ndiyo kifo chetu.
Kubwa kuliko yote ni kwamba nilitaka tufanye kazi kwa bidii kabla ya chakula tulichopewa hakijaisha.
Siyo chakula tu, bali hata maji tulipewa kidogo ili tufe haraka na kwa kazi nzito tuliyokuwa tukifanya huku tukivuja jasho, ilikuwa ni hatari sana kama tungeishiwa maji.
Ni kwamba kuishiwa maji maana yake tungeshindwa kazi ya kuchimba mtaro wa kutuwezesha kutoka ndani ya lile shimo la kifo.
Tatizo lingine ambalo tulikumbana nalo ndani ya shimo lile ni vitendea kazi. Ile mifupa ambayo tulikuwa tukiitumia kuchimbulia ardhi ilikuwa ikilika.
Hilo lilinitia hofu sana na nilipoichunguza baadhi ya mifupa niligundua kuwa ni ya watu wa zamani sana hivyo haikuwa na uwezo wa kuhimili ardhi ambayo licha ya baadhi ya sehemu kuwa tifutifu, kuna sehemu zilikuwa ngumu.
Changamoto nyingine ni baadhi ya vijana kuchubuka viganja, yaani kuota mafindofindo kutokana na kutozoea kazi ngumu kama ile tuliyokuwa tukiifanya kwa vifaa duni, mifupa ya watu.
Lakini changamoto nyingine ni vifaa vya kusombea mchanga kwani tulikuwa tumeshachimba umbali wa hatua ishirini za mtu mzima.
Hatukuwa na makarai au ndoo badala yake tukawa tunatumia mafuvu ya watu ambayo kwa kweli yalitusaidia.
Wakati naanza kuwahimiza kutumia mavufu hayo baadhi ya wasichana walikwa waoga.
“Mnaogopa nini? Haya mafuvu hayadhuru, tumieni kusombea mchanga,” niliwaambia.
“Lakini mimi naogopa sana,” alisema msichana mmoja. Ni wazi kwamba wasichana karibu wote tuliokuwa nao ndani ya shimo lile la kifo ilikuwa mara yao ya kwanza kuona mifupa ya watu waliokufa.
Baada ya kuwapa somo kuhusu mifupa ile, wengi walipata ujasiri na wakawa wanatumia kama vitendea kazi. Niliwaambia wazi kwamba bila kufanya hivyo, tutafia kwenye shimo hilo kama walivyokuwa hao ambao mifupa yao sasa tunaitumia kama vifaa vya kuchimbia njia yetu ya kujinasua.
Je, watafanikiwa kujiokoa? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply