The House of Favourite Newspapers

Nilivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi – 9

0

ILIPOISHIA

 

Tuliamriwa  kusimama na kuanza safari na kuelekea kwenye shimo ambalo limeandaliwa kwa shughuli hiyo.

Yule msichana aliyekuwa mjamzito alikuwa akilia kwa sauti huku akipunga mikono ishara ya kutuaga.

 Kilio chake kilifanya hata sisi wanaume tuanze kulia, mimi huwa mgumu sana kulia lakini yowe za yule dada zilinifanya nitokwe na machozi.

Nini kilifuata?

 

SONGA NAYO…

Dereva Limbende na utingo wake ambao nao walisalimika kutupwa kwenye shimo la kifo, niliwaona wakibubujikwa na machozi kutulilia.

Vijana wenzangu tuliokuwa tumepangwa kwenye mstari wote walishindwa kusema chochote kwa kujua kwamba sasa tunakwenda kufa.

Wasichana tuliohukumiwa nao ambao walikuwa watano wote walikuwa wakilia. Mmoja aliishiwa nguvu kabisa za kutembea tukaamriwa tumbeba.

Kazi hiyo niliifanya mimi nikisaidiwa na kijana Kwiimukaga.

Hata hivyo, kazi ya kumbeba msichana ambaye alizimia wakati tunakwenda kutupwa shimoni ilikuwa ngumu ilibidi kupokezana kwa sababu msichana huyo alikuwa pandikizi la mtu.

Lakini pia kazi hiyo ilikuwa ngumu kwa kuwa tuliishiwa nguvu hasa kwa kuwa usiku uliopita hatukuweza kula chakula kutokana na hofu ya kifo ambacho sasa tunakwenda kukabiliana nacho.

Wakati wa msafara huo, kulikuwa na kikundi cha wapiga ngoma waliokuwa wamezifunga viunoni mwao.

Mwendo kutoka pale kwenye kiwanja cha mikutano hadi kwenye shimo ilichukua saa nzima ni mbali kutoka makazi ya watu na ni kwenye msitu mnene.

Tulipofika pale ajabu ya kwanza tuliyoiona ni kwamba shimo lile ni pango kubwa ambalo sijajua lilitokana na nini lakini lilikuwa na mfuniko mkubwa wa jiwe.

Kwa wale wasoma maandishi ya vitabu vya dini, niwakumbushe kuwa jiwe lile linafanana na lile ambalo lilitumika kufunikia kaburi la Yesu.

Tofauti na zama hizo ambapo jiwe hilo kubwa lilivingirishwa na askari, lile la pale lilitolewa na winji maalum ya kunyanyulia vitu vizito.

Ajabu ya pili ni kwamba kulikuwa na kiti maalum cha chuma ambacho kilikuwa na minyororo ambacho kilikuwa pale, kando kidogo na ile winji.

Nilijiuliza, kiti kile cha chuma, tunauawa kwanza kwa umeme baada ya kukikalia kisha tunatupwa shimoni?

Hilo lilikuwa swali langu kichwani na sikuwa na uwezo wa kupata jibu wakati ule.

Ajabu ya tatu ni kwamba karibu na kile kiti kulikuwa na askari wanne ‘walioshiba’ ambao nilikuwa sijajua walikuwa pale kwa kazi gani.

Baadaye aliitwa kijana wa kwanza aanze kutekeleza adhabu yetu, alichukuliwa na askari walioshiba na kukalishwa kwenye kile kitu cha chuma.

 Baadaye alinyanyuliwa huku akimwaga machozi na kuwekwa kwenye mlango wa lile pango.

Alishushwa taratibu kwa ile winji. Ilielekea kuwa shimo lile ni refu sana kwa sababu minyororo iliyokuwa imeshikilia kiti ilikuwa mirefu na iliisha yote.

Baadaye nilishuhudia ile minyororo minne ikirudi ardhini na kipande kimoja kimoja cha kile kiti cha chuma kilichoshuka chini na kijana wetu.

Zoezi hilo liliendelea mpaka wote wakaisha nami nikawa mtu wa mwisho kushushwa chini ya shimo.

“Wewe Issa Namakoto tumekufanya kuwa wa mwisho kushushwa kwenye hili shimo la kifo ili utoe neno lako la mwisho kwetu,” alisema Kamanda Ben Mtwanga aliyeoongoza zoezi hilo la kututumbukiza shimoni.

Nilifikiria haraka japokuwa akili ilikuwa siyo yangu lakini niliamua kuwatisha tu.

“Mimi naitwa Namakoto au ukienda kijijini kwetu huwa naitwa Maharage ya Zambia. Nawaahidi kwamba sisi hatutakufa na tutakuja kutokea tena katika nchi hii. Mtashangaa lakini hiyo ndiyo ahadi yangu.”

Baada ya kusema hayo niliona watu waliokuwa pale wakishangazwa na kile nilichokisema.

“Anasemaje? Watakuja tena? Wangapi wametumbukizwa kwenye shimo hilo na hawajawahi kurudi duniani?” nilisikia mtu mmoja akiuliza.

Hapohapo nikajua kuwa kumbe lile shimo limewahi kutumika kufunika watu wengine tofauti na tulivyokuwa tukidhani kwamba tungefukiwa kwenye shimo kwa mchanga.

Mimi tofauti na wenzangu ambao walikuwa wakiishiwa nguvu na kubebwa kuketishwa kwenye kile kiti cha chuma, nilikwenda na kukaa mwenyewe.

“Kwa kawaida kila anayetupwa ndani ya chimo hili hupewa chakula cha siku saba na maji ili atumie muda huo kumuomba Mola wake kabla ya kifo, hivyo, baada ya wewe kutiwa shimoni kuna chakula na maji tutawaletea, muwe tayari kuvipokea,” alisema Kamanda Mtwanga.

Sikuwa na la kusema zaidi ya kumuitikia “Sawa.” Winji iliwashwa na nikaanza kuteremshwa shimoni na kwa kuwa nilikuwa mtu wa mwisho, ngoma ambazo zilitulia wakati wa zoezi zima, zikaanza kupigwa tena.

Nilifika chini ya shimo na kukuta wenzangu wakiwa wamejikunyata huku wengi wakilia na baadhi yao wakiwa wamezimia.

Kwa kuwa jiwe lilikuwa halijafunikwa, tuliweza kuonana vizuri kwa sababu mwanga ulikuwa ukiingia.

 Niliweza kuona kando ya pale tulipokuwa tumeketi kuna mifupa ya watu, hiyo iliashiria kuwa watu waliotupwa ndani ya shimo hilo walifariki dunia na kwamba siyo utani.

Baada ya dakika kadhaa niliona kile kiti kikishuka, kilikuwa na maboksi kumi ya maji. Nilishusha, yakaletwa tena mara saba baadaye ililetwa mikate mingi, sikuwa na sababu ya kujua ilikuwa mingapi kwa sababu nilijua walaji watakosekana.

Wasichana ambao walikuwa wakilia tukiwa mle shimoni waliruka ghafla:“ Nini?” nilihoji.

“Kuna panya,” alijibu msichana mmoja.

Akili yangu ilifanya kazi haraka na kujiuliza, ‘huyu panya anaishije kwenye shimo hilo refu? Je, inawezekana hutoka nje kupitia lile tundu lililotumika kutushushia sisi humu?”

Jibu sikupata kwa sababu panya mwenyewe hakuwepo aliingia shimoni lakini hata kama angekuwepo nisingeweza kumuuliza kwa kuwa ni panya.

Nilisimama na kwenda kuangalia lile tundu aliloingia panya, akili zikanituma kwamba utafiti wangu uanzie pale.

Je, nini kiliendelea? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply