The House of Favourite Newspapers

Niyonzima aandaliwa mkataba mpya Simba

Haruna Niyonzima

UONGOZI wa Simba umeanza mazungumzo na kiungo wake mchezeshaji Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kwa ajili ya kumuongezea mkataba mpya wa kuendelea kuichezea timu hiyo kwenye msimu ujao.

 

Mnyarwanda huyo ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, wengine ni Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei na Nicholaus Gyan.

 

Niyonzima aliyejiunga na Simba msimu uliopita akitokea Yanga, anaruhusiwa kuzungumza na klabu yoyote kwa kuwa muda wa mkataba wake wa sasa ni chini ya miezi sita.

 

Taarifa za uhakika zinadai kuwa benchi la ufundi la Simba chini ya kocha mkuu, Patrick Aussems ndiyo waliopendekeza kiungo huyo aongezewe mkataba mwingine wa miaka miwili.

 

“Kwa kiwango anachoonyesha Niyonzima, hivi kuna kocha atakayependekeza kumuacha katika usajili wa
msimu? Ni ngumu hivyo kiungo huyo ataendelea kubakia kuichezea Simba,” alisema mtoa taarifa.

 

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi kuhusu hilo, alisema: “Muda wa usajili bado, hivyo tumepanga kukutana na kocha hivi karibuni kabla ya ligi kumalizika kwa ajili ya kujadili usajili.”

 

Alipotafutwa Niyonzima alisema: “Mimi soka ndiyo kazi yangu inayoendelesha maisha yangu, hivyo nitakuwa tayari kubaki kuichezea Simba kama tutafikia makubaliano mazuri katika maslahi yangu.”

Comments are closed.