The House of Favourite Newspapers

Njia 2 za Kuongeza Kipato Chako!

KARIBU msomaji wangu, ni Jumatatu nyingine murua! Hivi umewahi kujiuliza utawezaje kuongeza pesa ambazo unazipata katika maisha yako? Watu wengi sana wanatamani kuongeza vipato vyao ila huwa wanatumia njia ambazo siyo sahihi.

Ndugu zangu ambao tupo kwenye vita hii ya kutafuta utajiri, leo ningependa tujifunze njia rahisi ambazo tunaweza kuzitumia mara moja na kuanza kuongeza vipato vyetu kwa haraka zaidi.

 

1: UPO TAYARI KUTATUA MATATIZO YA WATU?

Jambo la kwanza la kujiuliza unapotaka kuongeza kipato chako ni kuwa, je, upo tayari kutatua matatizo ya watu? Ndugu yangu, kama ulikuwa hujui ni kwamba sehemu mojawapo kubwa ambayo pesa imejificha ni kwenye matatizo ambayo yanawakabili watu mbalimbali na leo utajifunza mbinu za kuchukua pesa zilizojificha huko.

 

Tafsiri kubwa ninayopenda kuitumia kuhusu pesa ni ile inayosema; ’Pesa ni zawadi unayopata baada ya kutatua tatizo la mtu fulani’. Huu ndiyo ukweli ambao hauwezi kupingika. Ukitaka kujua tafsiri hii imebeba uzito mkubwa kwenye maisha yako, jiulize swali hili; ‘Je, tangu umeamka leo umetumia pesa zako kufanya mambo gani?’

 

Jaribu kuorodhesha kila matumizi uliyoyafanya, utagundua kuwa kuna mtu umemlipa ambaye amekutatulia tatizo lako ambalo huna uwezo wa kulitatua au huna muda wa kutosha kulitatua hivyo umeruhusu mtu afanye kwa niaba yako.

Hii ina maana kuwa njia kubwa ya kwanza ya kupata pesa ni kutatua tatizo au matatizo ambayo yanawakabili watu fulani kwenye eneo lako. Kadiri unavyotatua matatizo mengi zaidi, ndivyo utakavyokuwa unazidi kuvutia pesa nyingi kwa upande wako.

Kadiri unavyotatua matatizo makubwa ndivyo pia utakavyokuwa unavutia pesa kubwakubwa kwenye maisha yako. Hii ina maana ukijigundua kuwa unaingiza pesa kiasi kidogo, uwezekano mkubwa ni kuwa hujatatua matatizo ya kutosha.

 

Kila unapopita, kuna matatizo yanayowakabili watu na kazi yako ni kuchagua aina ya tatizo ambalo unaona lipo ndani ya uwezo wako kulitatua na kuanza kulifanyia kazi mara moja.

Kwa hiyo kabla hujaendelea kusoma zaidi, jaribu kujiuliza swali hili; ’Hivi kwenye mazingira yangu kuna tatizo gani ambalo ninaweza kulitatua?”

 

Hii haijalishi kama uko eneo la shule, kazini au uko eneo la biashara. Jaribu kuorodhesha kila tatizo ambalo watu wanakabiliana nalo katika eneo lako na jiulize; ‘Je, ninaweza kulifanyia kazi lipi kati ya hayo? Wakati mwingine unaweza kuamua kuuliza watu wanaokuzunguka kuhusiana na changamoto zinazowakabili na watakuambia, kumbuka kuwa wazo bora kabisa la biashara ni lile linalolenga kutatua matatizo yanayowakabili watu wa eneo husika.

 

Je, umeshapata tatizo ambalo unaweza kulitatua? Wengi huwa wanasema wanakwamishwa na mtaji ila katika kuchagua tatizo, hakikisha unaanza na lile ambalo unaweza kuanza nalo kwa kile ulichonacho. Hakikisha wiki hii haiishi kabla hujaanza kulifanyia kazi wazo lako ambalo umelipata, ukichelewa sana utakuta mtu mwingine ameshalifanyia kazi haraka.

 

2: ONGEZA THAMANI

Njia ya pili ya kuongeza kiwango cha pesa ambazo unazipata ni kuhakikisha kuwa unaongeza thamani yako katika kile unachokifanya. Unachotakiwa kujua ni kuwa watu hukulipa pesa kulingana na thamani ambayo unaitoa. Hii inamaanisha kuwa unaweza kufanya kazi kwa bidii, lakini kama huongezi thamani yako, basi malipo yako yanaweza yasiongezeke kabisa.

 

Kuna tofauti kubwa ya kufanya kazi kwa nguvu na bidii (working hard) na kufanya kazi wa werevu na maarifa (working smart). Hii ya pili hutoa matokeo makubwa sana na ya haraka kwa mtu anayetumia muda wake vizuri wakati ile ya kwanza hutoa jasho jingi ila matokeo huwa ni machache sana au ni yaleyale jana, leo na kesho.

 

Hebu jaribu kujichunguza kwenye maisha yako, wewe ni mtu ambaye unafanya kazi sana, lakini matokeo ya kipesa ni madogo? Je, ni mtu ambaye si mvivu, unaamka mapema asubuhi na unachelewa kulala ila ukiangalia muda uliofanya kazi na mafanikio ya kipesa uliyoyapata hayalingani kabisa? Kama wewe ni mmojawapo inamaanisha inawezekana upo kwenye kundi hili. Hata hivyo, kuna njia kadhaa ambazo unaweza kuzitumia kuongeza thamani yako.

 

Moja ni kuongeza ujuzi wa kile unachokifanya. Hivi umewahi kujiuliza kwa nini wachezaji wanaocheza timu moja ndani ya dakika tisini, lakini kuna mwingine analipwa zaidi ya mwingine kama ilivyo kwa akina Cristiano Ronaldo, Paul Pogba, Alexis Sanchez na Lionel Messi?

 

Jibu ni kuwa anayelipwa zaidi ingawa anatumia muda uleule ila ana ujuzi ambao wengine bado hawana kwenye maisha yao. Moja ya changamoto za watu wengi katika mambo wanayofanya ni kuwa hawaongezi ujuzi kabisa, matokeo yake hawaongezi kipato kabisa.

Hebu jaribu kujiuliza; ‘Katika unachofanya leo, ni lini mara ya mwisho uliongeza ujuzi? Lini ulijifunza kitu kipya mtandaoni? Lini ulihudhuria kozi? Lini ulipata mafunzo fulani?’

 

Kama ujuzi wako ni uleule uliokuwa nao mwaka jana, uwe na uhakika pia malipo yako ya kipesa yatabakia vilevile. Kumbuka kuwa tumeshahama kwenye ulimwengu wa watu kutumia UZOEFU pekee, tupo kwenye ulimwengu wa watu kutumia UJUZI bila kujali wanafanya kazi au biashara gani na wana muda mrefu kiasi gani. Leo jiulize; ‘Je, kuna ujuzi gani ambao ninatakiwa kuuongeza katika maisha yangu ambao nikiwa nao utaniongezea kasi ya matokeo? Jaribu kutafakari kabla hujaendelea.

 

Ukishaujua ujuzi huo, jipangie mkakati wa namna ya kuuongeza haraka. Inawezakena ikakulazimu kusoma kozi rasmi, kwenda kwa mtu kujifunza au kutumia mtandao. Kwa vyovyote vile, hakikisha unajiwekea mkakati wa kuongeza ujuzi kwa haraka. Ningependa kusikia kutoka kwako pia aina ya ujuzi ambao umekusudia kuuongeza.

 

Mbili, ili kuongeza thamani yako upate kipato zaidi, hakikisha kuwa unajenga sifa ya kuaminika kwa kila jambo. Kati ya vitu ambavyo vinakata mifereji ya kipesa kwenye maisha ya watu wengi ni hali ya kushindwa kuaminika. Watu wakishasema wewe ni mtu usiyeaminika, inamaanisha ni moja kwa moja hawatakuwa tayari kukupa pesa au fursa zaidi.

 

Kumbuka kuwa, kuna watu wanaweza kukuamini na kukuazima pesa hata bila kuandikishana kwa sababu tu wanajua utawarudishia, ila ukivunja uaminifu ni ngumu kuurudisha. Jitahidi kila wakati kujenga sifa ya kuaminika. Kama unafanya biashara, wafanye wateja wako wakuamini kwa kutimiza ahadi unazowapa, kwa kuwapelekea bidhaa kama mlivyokubaliana na kwa ubora uliowaambia.

 

Kama wewe umeajiriwa, jitahidi kuwa na sifa ya kuaminika kwa kufanya kazi yako kwa wakati, kutotumia uongo na mambo yanayofanana na hayo ambayo mwisho wa siku yatakuondolea uaminifu.

Leo jiulize; ‘Ninawezaje kujenga uaminifu katika kile ninachokifanya ili nivutie pesa zaidi?’

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyinginemoto!

 

Mwandishi wa makala haya ni Joel Nanauka (pichani juu) ambaye ni Mwalimu, Mhamasishaji wa Mafanikio na Mwandishi wa Vitabu. Anapatikana kupitia; YouTube: Joel Nanauka Facebook: Joel Nanauka Instagram: joel_ Nanauka,

E-mail: jnanauka@ gmail.com

Simu: 0655 720 197

Comments are closed.