The House of Favourite Newspapers

NMB yauza Hati Fungani za Bil.83.3/=

Afisa Mkuu wa Fedha, Ruth Zaipuna akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza matokeo ya hati fungani ya Benki hiyo katika ofisi za NMB  jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Mkuu wateja wadogo na wakati, Filbert Mponzi na Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko ya Fedha (Head, Gladness Deogratius.
Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati Benki ya NMB, Filbert Mponzi(kushoto) akitoa ufafanuzi wa jambo.

 

 

BENKI ya NMB, imetangaza matokeo ya mauzo ya toleo la tatu la programu ya hati fungani ya benki hiyo, ambako imekusanya Sh. Bilioni 83.3 sawa na asilimia 333 ya mauzo yaliyotarajiwa awali ya Sh. Bilioni 25. Mauzo ya toleo la tatu la hati fungani ya NMB yalifunguliwa Juni 10 na
kufungwa Julai 8, mwaka huu, ambako kipindi hicho cha miezi miwili, kilikuja baada ya Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA), kutoa idhini ya mauzo hayo.

 

 

Akizungumza katika hafla ya kutangaza matokeo hayo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mkuu wa Fedha , Ruth Zaipuna, alisema wao kama benki wanajivunia kiwango hicho cha mauzo, kinachothibitisha imani ya wananchi na jamii kwa benki yake.

 

 

Zaipuna alibainisha kuwa, tayari NMB imeyapokea na kuyakubali maombi yote na kwamba waombaji wote wa manunuzi ya hati fungani wametaarifiwa na kwamba leo Agosti 2, wanaorodhesha hati fungani zote, kabla ya wanunuzi kukabidhiwa vyeti mwezi mmoja ujao.

 

 

Alifafanua ya kwamba, mauzo hayo ya kiwango cha juu kuliko walivyotarajia, yanaiongezea benki nguvu ya kiuchumi katika kufanikisha utoaji wa mikopo kwa wateja wao na kwamba mchakato mzima umeshirikisha zaidi ya matawi 200 kote nchini.

 

 

“NMB inatoa shukrani za dhati kwa taasisi zote zilizofanikisha uuzwaji wa toleo la tatu la hati fungani ya NMB, ikiwemo CMSA, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshauri Kiongozi wa NMB, Stanbic Bank Tanzania Ltd na Dalali Mfadhili wa NMB, Orbit Securities Company Ltd,” alisema Zaipuna.

 

 

Hati fungani ni aina ya uwekezaji, ambao unamuwezesha mteja kuwekeza pesa katika taasisi (hasa shirika la kibiashara au Serikali), kwa kuikopesha fedha kwa muda maalum na kwa riba isiyobadilika. Riba ya hati fungani za NMB kwa mwaka ni asilimia 10.

 

 

Mteja anaponunua Hati Fungani ya NMB, anakuwa ameikopesha benki fedha zake, ambako NMB inaahidi kurejesha fedha zake (msingi) katika kipindi maalum cha ukomavu. Kuanzia muda uliowekeza hadi muda wa ukomavu ambao unakuwa miaka mitatu.

Comments are closed.