The House of Favourite Newspapers

VIDEO: JPM AZINDUA JENGO ‘TERMINAL 3’ UWANJA WA NYERERE


RAIS John Magufuli leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019, amezindua  rasmi jengo la Terminal 3 Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam  ambao upanuzi wake ulianza 2013 na kugharimu Sh788.6 bilioni

Mradi huo ulianza kujengwa 2013 na awali ulipangwa kutekelezwa kwa Sh705.3 bilioni lakini kutokana na kubadilika kwa taratibu za kikodi, mchoro wa mradi (design) na gharama ya mradi huo ziliongezeka kwa Sh85.3 bilioni.

Kampuni iliyotekeleza mradi huo ni BAM International ya Uholanzi ambayo ndiyo iliyofanya kazi za kikandarasi na Arab Consulting Engineers (ACE) ya Misri, iliyofanya kazi za ushauri.

Katika uzinduzi huo Rais Magufuli amepongeza kukamilika kwake ambako alisema  kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na fedha za serikali na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo, jambo lililoongeza nguvu ya taifa kujitegemea katika miradi yake ka kutumia fedha za ndani.

Alisisitiza Watanzania kuwa na moyo wa kujitegemea ili kumaliza matatizo yao kwa kutumia fedha na nguvu zao.

“Kuna wakati najiuliza siku moja Mungu akinichukua hawa wanaokuja watayamaliza kweli?   Hii ni kwa sababu inahitaji moyo; unafanya hivi huku unatukanwa lakini inabidi ufanye tu, inahitaji kujitoa kwelikweli, ” alisema rais na kuongeza kwamba hivi sasa Tanzania inaogopewa na watu wengi kwa kuweza kusimama na kutumia fedha zake.

Alimshukuru rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kwa kuanzisha ujenzi huo ambao yeye ameuendeleza.  Pia alikumbusha kwamba ujenzi wa uwanja huo ulikuwa umetolewa chini ya usimamizi wa shirika la usimamizi wa viwanja vya ndege nchini (TAA) lakini walishindwa na hivyo jukumu hilo kutolewa kwa wakala wa mabarabara (Tanroads).

Alielezea furaha yake pia kwamba ufunguzi wa uwanja huo umefanywa siku chache kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi za jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) ambao utafanyfika jijini Dar es Salaam karibuni.

“Kuanzia juma lijalo kutakuwa na ugeni mzito kabisa wa SADC, naomba tuwapokee kwa shangwe na niwaombe changamkieni fursa zote… narudia changamkieni fursa zote  za kimaendeleo zitakazojitokeza wakati wa mkutano huo,” alisema.

 

Comments are closed.