The House of Favourite Newspapers

Ofisa Habari Chadema Afikishwa Mahakamani Kisutu

0

OFISA Habari Msaidizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dominic Mgaya (37) leo Septemba 18, 2020 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka  la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

 

Akisoma hati ya mashtaka, wakili wa Serikali, Adolf Ulaya, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 127/2020.

 

Amedai kuwa Mgaya alidaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Oktoba 14, 2017 na Septemba Mosi, 2020 katika maeneo ya mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kurusha maudhui katika mtandao, kupitia channel ya CHADEMA MEDIA TV.

 

Amedai kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kurusha maaudhui hayo bila kuwa na leseni ya TCRA.

 

Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka linalomkabili, amekana kutenda kosa.

 

Upande wa mashtaka ulidai  upelelezi haujakamilika, hivyo uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Hakimu Kabate ametoa masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika watakaosaini bondi ya Sh 500,000 kila mmoja.

 

Mshtakiwa amefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana, hivyo ameachiwa kwa dhamana.

 

Hakimu Kabate ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 20, 2020 itakapotajwa.

 

Habari na Salim Abdurahmani, Global TV

SHOO KONKI ya ALIKIBA Mbele ya MAGUFULI KIGOMA, Apigiwa SHANGWE BALAA…

Leave A Reply