The House of Favourite Newspapers

Vilio Kuagwa Wanafunzi Waliokufa kwa Moto Kagera

0

MIILI ya wanafunzi 10 waliokufa kwa ajali ya moto uliounguza bweni la wavulana katika shule ya msingi Byamungu  wilayani Kyerwa mkoani Kagera imeagwa leo na kukabidhiwa kwa wanafamilia tayari kwa mazishi.

 

Zoezi hilo limefanyika leo Septemba 18, mwaka huu, katika viwanja vya shule hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa kwa niaba ya Rais John Magufuli  na umati mkubwa wa waombolezaji.

 

Akiongea katika hadhara hiyo, Bashiru amewapa pole wafiwa na jamii nzima iliyoguswa na msiba huo ambapo amewasihi wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo huku akiitaka serikali pamoja na vyombo vya usalama kuendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

 

Ameitaka serikali na viongozi wa Mkoa wa Kagera kusimamia maagizo aliyoyatoa Rais Magufuli alipokuwa Bukoba na kuwataka wamiliki wa shule kuendelea kutoa ushirikiano pale watakapohitajika.

 

‘’Rais magufuli ameniagiza nije hapa kuwapa pole kwa msiba huu mkubwa lakini ameniagiza pia kuweka msisitizo wa maagizo yake aliyoyatoa ya kuhakikisha mazingira ya watoto wetu wanapokuwa shuleni yanakuwa salama.,’ amesema.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema kuwa serikali imekuwa bega kwa began na watu wa Kyerwa na hasa wafiwa kwa kuhakikisha marehemu wanahifadhiwa vizuri pamoja na majeruhi wanatibiwa ambapo amesema kuwa tayari zimeundwa kamati za uchunguzi kwenye shule zote za mabweni mkoani humo kwa ajili ya kuangalia miundombinu.

 

Naye Wilbroud Mutabuzi ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM (NEC) awewasihi wananchi wa Kyerwa na wafiwa kutokutumia nafasi hii ya msiba kuanza kuzushiana na kuleta maneno ambayo kwayo yanaweza kulta uvunjifu wa amani.

 

Pia, Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Alhaj Kharuna Kichwabuta, amesema katika  hali hii wanadamu wanatakiwa kuipokea kwa kuwa mpangaji wa kila ajali na tatizo kwa mwanandamu ni Mwenyezi Mungu na hivyo wafiwa wanatakiwa kuwa na subira.

 

Wakati huohuo, mmiliki wa shule hiyo, Abdu Bushagama, amemshukuru Rais Magufuli kwa huruma zake kwa kuamuru aachiwe ili kushiriki kuwaombea watoto aliowalea kwa upendo na kuongeza kuwa miongoni mwa waliokufa yumo pia mjukuu wake.

 

Usiku wa kuamkia septemba 14 mwaka huu ilitokea ajali ya moto katika shule hiyo ambapo bweni la wavulana kwenye shule hiyo liliungua na kusababisha vifo vya watoto 10 na wengine kujeruhiwa.

Na Allawi Kaboyo Kyerwa.

Leave A Reply