The House of Favourite Newspapers

OFM Yabaini Utapeli Daraja la Kigamboni!

0
Mlinzi wa Suma JKT akikagua kamera ya mwandishi baada ya kuikamata.

 

Wakati Watanzania wakifurahia kukamilika na kuanza kutumika kwa daraja la kisasa la Kigamboni ambalo linaitwa Nyerere Bridge, mambo ya aibu yameibuka baada ya kudaiwa kuwepo kwa watu wanaofanya vitendo vya kitapeli dhidi ya wananchi wanaolitumia, Risasi Mchanganyiko linaweza kuripoti.

 

Chanzo cha kuaminika kililidokeza Risasi Mchanganyiko kuwa vipo vitendo vya kitapeli vinavyofanyika darajani hapo, kwa watu kujifanya askari na kuwaomba hongo wananchi wanaopita hapo na kujaribu kujipiga picha kwa kutumia kamera au simu zao za mikononi.

Nyerere Bridge

 

“Watu hao wana kawaida ya kuwakamata wanaopiga picha eneo hilo la daraja na kuwalazimisha kutoa pesa, huku wakitishiwa kunyang’anywa simu au kamera na wakati mwingine kutishiwa kufikishwa katika jengo la utawala kwa adhabu kali zaidi,” kilidai chanzo hicho.

 

Kufuatia madai hayo, Kitengo Maalum cha Global Publishers cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) kiliamriwa kuingia kazini mara moja ili kubaini ukweli wa vitendo hivyo kufanyika katika daraja hilo la umma linalomilikiwa na serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF.

 

Mmoja wa wafanyakazi wa daraja hilo alipokutwa na makamanda hao na kutakiwa kutoa ufafanuzi wa suala zima la upigaji picha, alisema NSSF wameweka utaratibu maalumu wa kufotoa picha katika daraja hilo, lakini matapeli wametumia fursa hiyo kuwapiga pesa watu wanaoonekana kutojua vizuri juu ya suala hilo.

 

 

Mwandishi (kushoto) akimbembeleza mlinzi huyo ampatie kamera.

 

Baada ya kupata majibu hayo, makamanda hao walijipanga na kuanza kurandaranda huku wakijipiga picha katikati ya daraja mchana wa saa saba, lakini dakika 20 tu baadaye wakakutana na matapeli hao waliojifanya ni wahusika wa daraja hilo.

 

Hata hivyo Kamanda wa OFM aliyekuwa akijipiga picha kwa makusudi aliwakomalia watu hao na matapeli hao walipobaini wamekutana na mjanja mwenzao, waliamua kuachana naye na kutokomea kusikojulikana.

 

Kamanda huyo akiwa na mwenzake, alikwenda tena kujipiga picha katika eneo lingine na ndipo alipojikuta mikononi mwa walinzi ambao ni wa Suma JKT, wakachukua kamera ndogo aliyokuwa akiitumia kupiga picha huku wakimchimba mkwara.

 

Walinzi hao wawili waliokuwa wamevaa ‘unifomu’ waliwahenyesha makamanda hao wa OFM kwa muda wa saa tatu kisha baadaye wakaamua kuwaachia.

 

Wakijadiliana

 

Akizungumza kwa njia ya simu, Ofisa Habari wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Khalfani Abdallah alisema suala la kuwepo kwa matapeli darajani hawalifahamu, lakini kwa vile limefikishwa mezani kwake, ataliwakilisha sehemu husika.

 

“Sina taarifa kama kuna vitendo vya namna hiyo katika daraja la Nyerere, lakini kwa kuwa umelileta mezani kwetu sisi pia tutalipeleka katika mamlaka husika ili lishughulikiwe,” alisema.

 

Kadhalika Abdallah aliongeza kuwa siyo ruhusa kupiga picha katika daraja hilo hasa eneo la utawala bila kufuata utara tibu uliowekwa huku akisisitiza hakuna sheria ya faini kwa mtu anayekamatwa akifotoa picha zaidi ya kutakiwa kuzifuta na kuelekezwa utaratibu.

 

STORI: ALLY KATALAMBULA NA BONIPHACE NGUMIJE | RISASI JUMATANO |DAR ES SALAAM

Leave A Reply