The House of Favourite Newspapers

OFM yanusa jipu kivuko …

0

DAR ES SALAAM: Kikosi Maalum cha Global Publishers cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ limenusa jipu katika Kivuko cha Kigamboni, Dar, jinsi baadhi ya abiria wa vivuko wanavyozamia kwenye ‘pantoni’ bila kulipa nauli, jambo linalotajwa kuikosesha serikali mapato.

Dawati la OFM lilipokea malalamiko kutoka kwa raia wema, wakieleza jinsi ofisi za kivuko, upande wa Kigamboni zilivyo na mianya mingi ya watu kuingia bila kupitia getini na kupanda kwenye kivuko bila kulipa nauli, hali inayopoteza mapato ya serikali lakini pia kuhatarisha usalama wa abiria.

“Kuna njia watu wanapita bila kuwa na tiketi, hawalipi nauli ya shilingi 200 wanayopaswa kulipa na pia kama mtu ana lengo baya, anaweza kuingia na silaha kama bunduki au bomu kwenye hivi vivuko viwili vya Mv Kigamboni na Mv Magogoni, akiamua kuwadhuru abiria hakuna kipingamizi, nyie fuatilieni mtaujua ukweli,” kilisema chanzo chetu.

Baada ya kupata habari hizo, waandishi wetu walifunga safari mpaka Kivukoni na kujionea utaratibu ulivyo ambapo kwa upande wa Posta, mambo yalionekana kuwa shwari huku abiria wote wakifuata utaratibu wa kujipanga kwenye mistari na kulipa nauli kama inavyotakiwa.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti upande wa Kigamboni ambapo waandishi wetu walishuhudia watu kadhaa wakipenya kutokea ufukweni na kupanda kwenye pantoni bila kulipa nauli.

OFM ilibaini kwamba wanaozamia kwenye pantoni, hujificha mwisho wa uzio wa kivuko upande wa Chuo cha Mwalimu Nyerere, jirani na sehemu zinapoegeshwa boti na mitumbwi ya wavuvi na husubiri mpaka pantoni ishushe abiria.

Abiria wanaotaka kuvuka wanapofunguliwa geti, watu hao nao hujichanganya wakitokea upande wa ndani, hivyo kupita bila kulipa nauli na kwenda kupanda kiulaini.

Baada ya kujionea hali hiyo, waandishi wetu walimtafuta msemaji wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano ambaye hakupatikana, lakini afisa mmoja aliyekataa kutajwa jina, alifafanua kwamba wahusika wa vivuko ni Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA).

Juhudi za kumpata msemaji wa TEMESA hazikuzaa matunda mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni.

Siku chache baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alifanya ziara kivukoni na kuwapa miezi mitatu TEMESA kuhakikisha wanafunga mfumo kamili wa elekroniki katika Kivuko cha Magogoni ili kudhibiti mapato yanayopotea kiholela ambapo ilibainika kwamba zaidi ya asilimia 20 ya abiria wanaotumia vivuko, hupanda bila kulipa nauli.

Imeandaliwa na Chande Abdallah, Gladness Mallya na Hamida Hassan.

Leave A Reply