The House of Favourite Newspapers

Okwi, Chama Waipeleka Nusu Fainali Simba

Kikosi cha Simba kilichoanza dhidi ya AFC Leopards ya Kenya.

SIMBA jana Jumatano iliwapooza mashabiki wao ndani ya Uwanja wa Taifa, kwa kuitupa nje AFC Leopards ya Kenya na kufuzu hatua ya nusu fainali ya SportPesa Supercup baada ya kushinda mabao 2-1.

 

Hiyo inamaanisha kwamba Simba itacheza na Bandari FC ya Mombasa kesho Ijumaa saa 8 mchana. Bandari ambayo iliwatoa Singida United iko chini ya Kocha Benard Mwalala ambaye ni straika Mkenya aliyefuta uteja wa Yanga kwa Simba miaka ya 2000.

Emmanuel Okwi (katikati) katikati akifanya yake.

Mabao ya Simba jana yalifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 13 na Claytos Chama dk 48 huku lile la Leopards likifungwa na Vincent Oburu dk 61.

 

Matokeo hayo yanamaanisha timu mbili kongwe za Kenya, ziliaga mashindano hayo jana baada ya Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi kufungwa penati 4-3 na Mbao kwenye mchezo uliochezwa majira ya saa nane mchana.

Kenya ambao mashabiki wao walitarajiwa kuja kwa wingi kwa usafiri wa mabasi jijini Dar es Salaam leo, imesaliwa na timu mbili kwenye michuano hiyo ambayo bingwa anabeba Sh69milioni.

Katika mechi ya jana, Leopards walionekana kutawala umiliki wa mpira kipindi cha kwanza lakini Simba ndio waliokuwa wakifika langoni kwao mara nyingi zaidi huku Okwi na Chama wakikosa nafasi nyingi za wazi.

Leopards walikuwa wakicheza kwa tahadhari kubwa huku wakishangiliwa na mashabiki wachache wa Yanga waliojitokeza uwanjani hapo. Yanga ilitolewa juzi na Kariobangi Sharks kwa jumla ya mabao 3-2.

Katika mchezo huo ambao Chama alikuwa mchezaji bora, Simba iliwajaribu wachezaji wake wa kigeni na takwimu zao zilikuwa hivi;

 

MTOGO-KISSIMBO

Huyu ni straika anaitwa Hunlede Kissimbo, mpaka alipotolewa dakika ya 45 alipiga pasi 7, pasi tatu ziliharibika na nne ndizo zilifika.

Hakufanyiwa faulo yoyote.

Alikosa shambulio moja kwa kichwa, mpira wa krosi aliopigiwa na Emmanuel Okwi. Aliporwa mipira mitatu na mabeki wa AFC Leopards kutokana na kukosa utulivu.

MGHANA MORO

Ni beki jina lake ni Lamine Moro.

Pasi alizopiga mpaka dakika 45 ni 15 zote zilifika kwa walengwa ingawa takolini hakufanya hata moja ndani ya muda huo.

Hatari alizotoa ni nne, alifanya faulo moja na yeye hakufanyiwa ndani ya dakika 45 za kwanza.

Kipindi cha pili, alipiga pasi 12, akafanyiwa faulo moja na yeye akafanya mbili. Aliokoa hatari tatu lakini akacheza kwa kiwango cha kati, kipindi cha kwanza alicheza na Paschal Wawa cha pili akacheza na Juuko Murshid.

Kiujumla dakika 45 wachezaji wote wawili hawakuwa na makali kwa kiwango cha kutisha kama wengi walivyotarajia.

Simba iliyoanza; Aishi Manula, Rashid Juma, Zana Coulibaly, Lamine Moro, Paschal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Kissimbo, Okwi na Chama.

MBAO WANATISHA

Mbao inayoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara jana Jumatano ilifanya maajabu kwa kuwaondosha Gor Mahia ya Kenya ambao ni mabingwa watetezi wa michuano ya SportPesa Super Cup.

Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1 yaliyofungwa na Denis Oliech wa Gor Mahia dakika ya 52 na Aboubakary Ngalema wa Mbao dakika ya 76.

Zilipokwenda kwenye penalti Mbao ilishinda 4-3 na kuwaacha Wakenya hao wenye mastaa kama Francis Kahata, Jacques Tuyisenge wakiwa hawana la kufanya.

Kocha wa Mbao, Ally Bushiri alisema; “Kwanza tuliwaheshimu sana Gor Mahia, tukaamua kukaa na mpira muda mwingi, lakini vilevile kipigo cha Yanga cha jana (juzi) kilitufanya tuongeze umakini ili kutunza heshima ya nchi.”

Kwa matokeo hayo, Mbao anakwenda kucheza nusu fainali na Kariobangi Sharks kesho Ijumaa saa 10:15 jioni.

PICHA: MUSA MATEJA | STORI:  SAID ALLY NA ISSA LIPONDA

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.