The House of Favourite Newspapers

OLA Afunguka Kilichowapoteza Pah One

 

PAH One

PAH One ni kundi la Muziki wa Bongo Fleva ambalo lilijipatia jina zaidi mwishoni mwa miaka ya 2000 ambalo linaundwa na watu watatu ambao ni ndugu wa damu, Ola, Ingwe na Tobanako na miongoni mwa kazi za mwanzo zilizowatambulisha vyema kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva ni Kizubaneta, I Run Dar es Salaam na I Wanna Get Paid.

 

Baada ya kujulikana vijana hawa, wenye asili ya Kigoma, walianza kusafiri sehemu tofautitofauti nje ya nchi kwa ajili ya kufanya shoo pamoja na kolabo mbalimbali. Lakini hata hivyo baada ya kusumbua kwa muda wa miaka kadhaa kundi hilo liliweza kupotea kwenye gemu.

Takribani mwaka na miezi kadhaa wakakaa bila kuachia ngoma na miezi miwili hivi kama iliyopita ndiyo kundi hili lilirudi tena kwenye gemu kwa kuachia ngoma iitwayo Hatuna Habari! Unaweza kujiuliza nini kilisababisha kundi hili lililokuwa linakua vizuri kupotea, changamoto wanazokutana nazo kwa sasa kwenye gemu na mengine mengi, huyu hapa Ola, kaka anayewaongoza kwenye kundi wadogo zake anafunguka kila kitu, teremka naye katika mahojiano na Risasi Mchanganyiko.

Risasi: Ola mmepotea sana, nini tatizo?

Ola: Hatujapotea mbona tupo, kazi yetu ya Hatuna Habari   imesogea na imefanya vizuri kwenye media mbalimbali.

Risasi: Lakini si kwa kiasi kile ambacho mmezoeleka huko nyuma, huoni kwamba kuna sehemu mnayumba?

Ola: Ni kweli. Hii ni kutokana na baadhi ya changamoto tunazokutana nazo kwenye muziki.

Risasi: Ni changamoto gani hizo?

Ola: Pesa. Muziki umebadilika. Mziki kwa sasa unahitaji pesa. Sasa wakati mwingine unajiuliza uwekeze milioni mbili kwenye video au ufanye mambo mengine ya kimaisha. Ukipima unaona hiyo pesa ya video bora ufanye jambo fulani la kimaisha alafu muziki ufuate baadaye, ndiyo kinachotokea mpaka unaona tunakaa kimya wakati mwingine bila kutoa kazi.

Risasi: Pole sana, Ingwe naye yupo wapi, mmekaa kimya mwaka na miezi kadhaa na mmeibuka wawili tu, wewe na Tobanako?

Ola: Ingwe yupo nyumbani Kigoma. Kuna masuala la kifamilia alikwenda kushughulikia. Sasa amekaa muda na sisi hapa tukaona muda unazidi kwenda bila kufanya lolote ndiyo maana tukaona ni bora tutoke kwanza sisi alafu akija kwenye kazi zinazofuata na yeye atakuwa pamoja. Bado ni kazi ya kundi hata kama hajaonekana na si solo.

Risasi: Kuna jitihada zozote ambazo mnajaribu kuzifanya ili kuhakikisha mnapata menejimenti ya kuwasapoti kwenye kazi zenu?

Ola: Jitihada zipo, lakini tatizo ni kwamba unakuta mameneja wengi wanaotaka kufanya kazi na sisi ni wale wa maneno na siyo vitendo. Wanaahidi mambo mengi lakini hawatimizi hata kimoja. Tupo tayari kufanya kazi na mtu yeyote lakini asiwe meneja maneno.

Risasi: Wakati mpo kimya kipi mlikuwa mnashughulika nacho zaidi?

Ola: Ni muziki. Tumeweza kufanikiwa kurekodi albamu mbili za audio, kwa hiyo hata meneja atakayekuja atagharamika kwenye video na mambo ya promosheni tu.

Risasi: Mkiwa kimya nini zaidi mlimisi kwenye gemu?

Ola: Hakuna, kwani bado kuna vitu tulikuwa tunafanya kulingana na muziki. Kwa hiyo hatuna tunachomis, kikubwa tunamuomba Mungu atujalie meneja ili turudi tulipokuwa kwani suala hili ndilo lililotupoteza.

Risasi: Kwa sasa mna mipango gani ya kimuziki?

Ola: Mwezi ujao tunatarajia kutoa kazi mpya.

Risasi: Asante kwa ushirikiano.

Ola: Karibu sana.

 

MAKALA: Boniphace Ngumije

Comments are closed.