The House of Favourite Newspapers

Omog Kutumia Kombe la SportPesa Kuijenga Simba

0

Omary Mdose, Championi Jumatano, Habari

KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, raia wa Cameroon, amepanga kuitumia michuano ya Kombe la SportPesa kwa ajili ya kukijenga zaidi kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Simba ambayo imemaliza msimu huu ikinyakua Kombe la FA huku ikiukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara uliotua kwa watani zao wa jadi, Yanga, inatarajiwa kuwa na mapumziko ya takriban siku tano kabla ya kuanza kujiandaa na michuano hiyo.

Michuano hiyo itakayozishirikisha timu nane ambazo ni Simba, Yanga, Singida United na Jang’ombe Boys kutoka Tanzania na Tusker, Gor Mahia, Nakuru All Stars na AFC Leopards za Kenya, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 5, mpaka 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Omog amesema: “Tunashukuru tumemaliza msimu salama licha ya kuukosa ubingwa wa ligi kuu, lakini kitendo cha kuchukua Kombe la FA ni faraja kubwa kwetu hali ambayo itatufanya msimu ujao tujipange zaidi. “Baada ya ligi kumalizika, kinafuata kipindi cha usajili ambapo hatutakiwi kufanya makosa kwa hilo na hii michuano midogo ambayo tunakwenda kushiriki, inaweza kutusaidia kuangalia wapi tunatakiwa kujiweka imara zaidi kabla ya kuanza kwa msimu ujao, lakini pia wale wachezaji waliokuwa wanakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, wataanza kuonekana.”

Leave A Reply