The House of Favourite Newspapers

Simba Yatenga Sh Milioni 600 Za Usajili

0
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe.

KATIKA kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara na bora kitakacholeta ushindani kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika watakaloshiriki mwakani, uongozi wa timu ya Simba umetenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya usajili.

Kauli hiyo, ameitoa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe wakati timu hiyo ikifanya usajili wake wa kimyakimya kunasa nyota wenye uwezo mkubwa watakaoisaidia kwenye michuano ya kimataifa.

Timu hiyo, hivi sasa inadaiwa kufanya mazungumzo ya kimyakimya na mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco na beki wa pembeni wa timu hiyo, Shomari Kapombe. Akizungumza na Championi Jumatano, Hans Poppe alisema bajeti ya usajili ya msimu ujao wa ligi kuu ni lazima ziwe tofauti na msimu uliopita kutokana na kushiriki michuano ya kimataifa.

Alisema gharama za usajili zitaongezeka na kufikia milioni 600. Msimu uliopita zilikuwa ni ndogo zaidi ya hizo. Aliongeza kuwa, Kamati ya Utendaji ya Simba ilikutana jana (juzi) na kujadiliana masuala mbalimbali ya usajili huku wakifanya tathmini ya kila mchezaji.

“Kamati ya Utendaji ya Simba tulikutana jana (juzi) na kikubwa tulijadili masuala mbalimbali ya timu yetu ikiwemo kufanya tathimini ya kila mchezaji kwa maana ya kiwango na mchango alioutoa kwenye timu katika msimu huu. “Hivyo, tunashukuru kuna baadhi ya wachezaji tuliopendekeza tuwasajili na kuwaacha katika msimu huu wa ligi kuu na bajeti tuliyoipanga kuitumia kwa ajili ya kuwasajili wachezaji.

“Kama unavyojua mwakani tunashiriki michuano ya kimataifa, hivyo ni lazima gharama za usajili ziongezeke ziwe tofauti na msimu uliopita na tulichopanga ni kuongeza bajeti yetu na kufikia milioni 600,” alisema Hans Poppe.

Leave A Reply