Pacman: Niko Fiti, Nitashusha Ndonga za Ukweli Dar Live
BAADA ya miaka sita kupita bila ya Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala Zakhem, Dar kutumika katika mchezo wa Msamsumbwi, bondia Nasibu Ramadhan ‘Pacman’ atakuwa ni miongoni wa mwa mabondia watatu wa Tanzania watakaouwasha moto katika mapambano ya Kimataifa la kugombania ubingwa wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati kwenye ukumbi huo.
Video: Nasib Ramadhani Nitampiga vibaya Mzimbabwe Njooni Dar Live
Pacman mwenye rekodi ya kucheza mapambano 33, ameshinda 22, kati ya hayo 11 ni KO, amepoteza tisa, matatu ni KO huku akitoa sare mawili wakati mpinzani wake, The Chairman akiwa na rekodi ya kucheza mapambano 24, akishinda 12, sita kwa KO na amepigwa 12, moja kwa KO huku akitoka sare moja.
Championi Ijumaa limefanya mahojiano maalum na Pacman ambaye ana uwezo wa kurusha ngumi nyingi kwa mfululizo ‘cherehani’ kuelekea katika pambano hilo la kukata na shoka ambapo ameanza kufunguka alivyoweza kujiandaa:
“ Nimejiandaa vizuri na kocha wangu Christopher Mzazi ‘Mzazi Respect’ ananisimamia vizuri kwa sababu hili ni pambano la kimataifa, hivyo natakiwa kufanya vizuri.
“Hili si pambano la kwanza la kimataifa kucheza, nimeshacheza mengi nje ya nchi na ndani ya nchi, hivyo sina hofu hata kidogo.
“Naendelea kujifua vikali katika gym yetu ya No Talking Gym iliyopo Mabibo jijini Dar.
UNAMZUNGUMZIAJE MPINZANI WAKO?
“Mpinzani wangu ni mzuri ila naamini mimi ni mzuri zaidi kuliko yeye, kwa jinsi nilivyojiandaa tuombe uzima hizi siku zilizobaki tuwe na afya njema na nguvu ili tuweze kufanya kazi tuliyotumwa na Watanzania.
USHAWAHI KUCHEZA PAMBANO LA UBINGWA NDANI YA TANZANIA?
“Sijawahi, hili ni la kwanza kwangu, licha ya kuwa ni la kwanza la kugombania ubingwa, Watanzania wasiwe na wasiwasi.
“Si kwangu tu hata kwa wenzangu wote tunaiwakilisha Tanzania tupo vizuri, wasituone wa kawaida, bali ni mabondia ambao ni wakali kwa hapa Tanzania na hao mabondia wanaokuja kutoka nje ya nchi wanakuja kupigwa tu na si kingine.
“Huko kwao wanaonekana wazuri lakini hapa kwetu ni wa kawaida tu kwa sababu tushakutana na mabondia wakali kushinda wao na tukawashinda.
MAPAMBANO YAKO YA NJE, NI LIPI LILIKUWA GUMU?
“Ni lile nililopigana mwaka jana dhidi ya bondia wa Uingereza, Thomas Ward. Huyu bondia alinisumbua sana japo nilimaliza
mpaka mwisho pambano la raundi kumi, lakini nilipigwa. Pambano hilo lilifanyika Birmingham, Uingereza.
ILIKUWAJE?
“Mpinzani wangu kila nilipokuwa napanga mikakati ya kumpiga nikawa nashindwa basi akawa ananipiga tu, unajua mpinzani wangu alikuwa yupo fasta sana yaani kabla sijapiga yeye tayari keshapiga, nilipigwa kihalali siwezi kulalamika.
KWA NINI WANAKUITA PACMAN WA BONGO?
“Hilo jina wamenipa Watanzania kwa sababu wakati tunafundishwa na kocha wetu, tulikuwa tunaambiwa tufuate nyayo za yule Mfilipino, Manny Pacquiao ‘Pacman’ jinsi anavyocheza.
“Kwa kifupi Pacman ndiye aliyenifanya mpaka leo hii nimekuwa hapa, tulikuwa tukionyeshwa CD zake wakati anapigana, hivyo kocha akaniambia anataka nicheze kama yeye, kuanzia hapo akaanza kunifundisha niweze kuwa kama Pacman na Watanzania wenyewe ndiyo wakanipa hilo jina mpaka leo naitwa Pacman wa Bongo.
KWA TANZANIA, PAMBANO LIPI LILIKUWA GUMU KWAKO?
“Ni moja ambalo nilicheza nikiwa nachipukia , nilicheza dhidi ya Juma Fundi katika pambano la raundi 12. Wakati napambana naye, hapo ilikuwa ni baada ya awali kunipiga, kisha nikaomba turudiane, akanipiga tena.
NINI SIRI YA MAFANIKIO YAKO?
“Ukiwa na nidhamu kuanzia ndani ya ringi mpaka nje, moja kwa moja kiwango chako kinakuwa juu kwa sababu siku zote nidhamu matokeo yake ni mafanikio. Nimefundishwa kuwa na nidhamu tangu naanza mchezo huu, kocha wangu amekuwa akinisisitiza kila siku na nimekuwa nikifuata kile ninachoambiwa.
UNAWAAMBIA NINI MASHABIKI WAKO?
“Nawasisitiza kuwa karibu na Global TV kushuhudia mapambano haya kwani kupitia simu zao za mkononi, wanaweza kushuhudia live hata kama wakikosa fursa ya kufika ukumbini.
“Yaani Global TV imerahisisha mambo, mtu unaweza kukaa kwako ukaangalia kupitia simu yako, unaingia YouTube, unatafuta chaneli ya Global TV, basi unaangalia kila kitu moja kwa moja kutoka Dar Live. Mimi na wenzangu tutapambana kuhakikisha tunashinda katika ardhi ya nyumbani,” anasema Pacman.
Idd Pialali: Njooni Dar Live Mshuhudie Nitakavyomuua Mkongo
Ili kulishuhudia pambano hilo kwa njia ya simu tena bure, hakikisha unajiunga (subscribe) na YouTube Chanel ya Global TV Online sasa hivi ili usipitwe. Ingia You Tube, tafuta GLOBAL TV ONLINE, kisha bonyeza neno subscribe pia bonyeza kikengele kidogo kilichopo pembeni yake ambacho kitakukumbusha kuangalia pambano hilo mara tu litakapoanza.
Kama wewe umeshajiunga, basi hakikisha pia umebonyeza kikengele ili usipitwe na kila kinachoendelea Global TV. Pia unaweza kutupata kupitia mtandao wetu wa www. globaltvtz.com. Usisubiri, jiunge sasa na Global TV ili uwe wa kwanza kuona ndondi za kimataifa.
JIUNGE SASA kwa kubonyeza HAPA: www.youtube.com/ user/uwazi.
IBRAHIM MUSSA | CHAMPIONI | Dar es Salaam