The House of Favourite Newspapers

Pacome Atuma Salamu Simba Atamba kuendelea na Mwendelezo wa Kufunga

0
Mshambuliaji wa Yanga raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua (kushoto) akiwa na Kouassi Attohoula Yao

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua, amesema hatabweteka na mabao matatu aliyoyafunga katika Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akipanga kuendelea na mwendelezo mzuri wa kufunga kwenye michezo ijayo.

Kauli hiyo huenda ikawa salamu kwa mshambuliaji wa Simba Mkongomani, Jean Baleke ambaye ni kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara akifunga mabao 5, akifuatiwa na Feisal Salum wa Azam mwenye nne, huku Pacome, Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli na Matheo Anthony wakifunga matatu kila mmoja.

Kiungo huyo kwa sasa ni kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Muargentina, Miguel Gamondi.

Akizungumza na Spoti Xtra, Pacome alisema anafurahia mwanzo mzuri aliouanza katika ligi wa kufunga mabao matatu kwenye michezo mitano, huku akipanga kufunga idadi kubwa ya mabao.

Pacome alisema lengo la kufunga idadi kubwa ya mabao, ni kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki pamoja na ubingwa wa ligi msimu wake wa kwanza akiwa na timu hiyo.

Aliongeza kuwa, tayari ameizoea ligi, sasa alichobakisha ni kuthibiitisha ubora wake kwa kuifanyia makubwa Yanga ikiwemo kufunga na kutengeneza nafasi za mabao kwa wachezaji wenzake.

“Kila siku nafikiria kitu kipya cha kukifanya ninapokuwepo uwanjani, lengo ni kuona ninaendeleza mwendelezo mzuri niliouanza wa kufunga mabao matatu katika ligi.

“Haitakuwa kazi nyepesi kwangu kufunga mabao, kutokana na ubora wa wapinzani wetu tunaokutana nao, lakini kwa kushirikiana kwa wachezaji wenzangu nitafanya mengi makubwa.

“Ninataka kuthibitisha ubora wangu msimu huu ukiwa wa kwanza kwangu, lengo ni kuhakikisha tunatetea ubingwa wa ligi na kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Pacome.

STORI NA WILBERT MOLANDI

MFANYABIASHARA MAARUFU ARUSHA AFIA NDANI ya GARI- AKUTWA na MABURUNGUTU ya PESA SIKU ya 5..

Leave A Reply