The House of Favourite Newspapers

PAKA WA AJABU AZUA BALAA!

MOROGORO: Ukistaajabu ya Musa utayaona ya firahuni. Khadija Ramadhan (67), mkazi wa Mtaa wa Mwigole, Kata ya Mwembesongo mkoani Morogoro, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kutokewa na paka akamfanyia vitu vya kushangaza kisha kumng’ata mguuni.  

 

Tukio hilo la kushangaza lililojaza umati mkubwa wa watu limetokea hivi karibuni, majira ya asubuhi nyumbani kwa bibi huyo wakati alipokuwa akipiga mswaki.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mjukuu wa bibi huyo, Asha Ramadhan alikuwa na haya ya kusema: “Majira ya saa 2 asubuhi bibi alikuwa akipiga mswaki hapa nje ghafla akaja paka na kumzunguka mara saba na kumvamia bibi na kumng’ata mguu wa kulia.

 

“Mimi nilikuwa ndani bibi akapiga kelele huku akitikisa mguu kwa lengo la kumtoa paka huyo lakini aligoma kutoka na kuendelea kung’ang’ania mguu wa bibi. Nikamuweka mwanangu chini nikachukua fimbo na kumtandika paka huyo mgongoni ndipo alipomuachia bibi na kukimbilia kwao, nyumba kadhaa kutoka hapa kwetu,” alisema mjukuu huyo na kuongeza:

 

“Niliamua kuzunguka nyuma ya nyumba yetu, nikawaambia masela tukamtoa kwenye ile nyumba na kumtoa nje yule paka wakamuua na baadaye wakamkata mkia kisha tukamchoma moto.”Kwa upande wa bibi Khadija alipohojiwa na mwandishi wetu alisema:

 

“Huyu paka sielewi ni wa aina gani ila mimi nina imani namuamini Allah, nilikuwa napiga mswaki hapa nje paka akaja akanizunguka kama mara saba hivi akanivamia na kuning’ata mguu nashukuru majirani wamenipa huduma ya kwanza kwa kunifunga kamba juu ya goti ili kama paka huyu ana sumu isisambae mwilini kisha wakanipaka masizi kwenye jeraha kuidhibiti damu isitoke nyingi baada ya kuzungumza na wewe napakia bodaboda wanikimbize hospitali,” alisema bibi huyo huku akionekana mwenye hofu kubwa.

 

Kaimu mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo ambaye pia ni mjumbe wa mtaa, Asha Ng’aka amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye mtaa wake. “Ni kweli tukio hilo limetokea kama unavyoshuhudia mimi kiongozi wa serikali ya mtaa huo kwa kushirikiana na wananchi wangu tumeamua kumuua kisha kumchoma moto paka huyo,” alisema kaimu mwenyekiti huyo.

STORI: Dunstan Shekidele, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.