The House of Favourite Newspapers

Paka Mtu Awakeshesha Watu Dar, Shuhuda Asimulia – Video

0

 

AMA kweli duniani kuna mambo! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia paka aliyefananishwa binadamu na kuitwa ‘paka mtu’ kuwasababishia hofu iliyowakeshesha wakazi wa Mwenge- Mlalakuwa jijini Dar kutokana na vitimbi alivyokuwa akiwafanyia.

 

Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa, paka huyo alitokea kusikojulikana na kuanza kuwafanyia vitimbi mtaani hapo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Baada ya kufanya vitimbi vya kutosha, aliingia uani kwenye nyumba ya mkazi mmoja wa eneo hilo aliyekuwa amelala na kumkurupusha usingizini.

 

Akiwa kwenye nyumba hiyo, paka huyo alianza kulia kama binadamu mwenye ulemavu wa kuongea (bubu) ndipo umati uliokusanyika ukaanza kusema huyo atakuwa ni paka mtu na si paka wa kawaida.

 

Paka huyo alianza kubadilisha milio ambapo licha ya kulia kama bubu aliyekuwa akilalamika, wakati mwingine alilia kama mtoto mchanga huku akichana nyavu za dirisha la nyumba hiyo na kutaka kuingia chumbani, vitimbi vyake vilidumu kwa saa tatu.

 

Sakata la paka huyo lilisababisha wananchi wapige simu ofisi za gazeti hili ambapo mwanahabari wetu alifika eneo la tukio na kukuta paka huyo ameshakufa.

Akiwa eneo la tukio, mwanahabari wetu alizungumza na mama mwenye nyumba hiyo aliyejitambulisha kwa jina Judith Lungato Stambuli na kueleza jinsi paka huyo alivyowakeshesha.

 

“Ilikuwa ni muda wa saa saba usiku, huyu paka baada ya kufanya vurugu kwa majirani zangu ndipo akahamia kwangu.

“Akiwa hapa nyumbani, akaanza kupiga makelele kwa sauti za ajabuajabu akilia kama binadamu aliyekuwa akitaka kuongea, wakati mwingine alikuwa kama bubu anayeongea.

 

“Tulipata hofu kubwa na kuamshana nyumba nzima, ndipo mwenzetu mmoja alitaka kumpiga kwa manati, lakini mimi nilimzuia na nikachukua maji ya baraka, hapo alijitutumua na kutoa macho yaliyokuwa yakitisha kama mnyama wa ajabu.

 

“Aliendelea kutufanyia vitimbi ndipo niliyakumbuka maji ya baraka niliyopewa na mchungaji fulani nilipokuwa mkoani Tanga (jina linahifadhiwa) nikammwagia, akaanza kuzunguka moja ya nguzo hapo uani.

 

“Kuona hivyo, nikampigia simu mchungaji wa Korogwe (Tanga) na alipopokea aliniambia niendelee kummwagia maji hayo ya baraka huku nikifuatisha maneno ya mchungaji huyo bila kumuogopa ambapo nami nilifanya hivyo.

 

“Nikiendelea kummwagia kiujasiri nikiwa mbali naye, alianza kubadilika rangi na kubadilisha milio huku akiendelea kuzunguka nguzo hii (akimuonesha mwandishi).

 

“Kwa kuwa nilishakuwa na ujasiri niliendelea kummwagia hayo maji ya baraka huku nikimkemea nikiwa na familia yangu, ghafla nikamuona akiishiwa nguvu, akalala jirani na nguzo hiyo, hatimaye alinyamaza kulia, lakini alikuwa bado anapumua.

 

“Mchungaji tulimfahamisha akasema tuingie ndani kulala tusiwe na wasiwasi kwani paka mtu huyo, huo utakuwa ndiyo mwisho wake.

“Tuliingia ndani, lakini kila mara tulikuwa tunamchungulia dirishani na kilichotushangaza ni kwanza ulalaji wake pale alipokuwa.

 

“Asubuhi tuliamka na kumkuta amekufa huku miguu yake ya mbele ikiwa imejitanua kama binadamu aliyelalia kifua, ajabu ni kwamba tangu afe kama saa kumi na moja alfajiri tulipoona hapumui hadi sasa hivi ni saa mbili na nusu zimepita, lakini ameoza na kutokwa na wadudu kama vile alikufa juzi.

 

“Kwa kweli hatujamuelewa huyu paka kabisa na ndiyo ndiyo maana watu wanasema huyu atakuwa ni paka mtu, tunamshukuru Mungu kwa kutulinda na hili, ” alimaliza kusema Judith almaarufu kama Anti Judy.

 

Mwanahabari wetu alifika kwenye ofisi ya serikali ya mtaa huo ili kusikia neno kutoka kwa viongozi wa mtaani hapo, lakini mpaka mwanahabari wetu anaondoka eneo hilo ofisi hiyo ilikuwa haijafunguliwa.

Mzoga wa paka huyo ulichukuliwa na kupelekwa kwenye kanisa moja maeneo hayo kwa maombezi maalum kisha kuzikwa.

 

Leave A Reply