The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-11

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA…
“Kumbe huyu hanijui, sasa subiri….” alisema Edson huku akiwa na hasira kali kama mbogo. Akawasha gari na kuanza kuelekea nyumbani kwa Elizabeth aliyekuwa akiishi hukohuko Mbezi Beach.
SONGA NAYO…

Simu ya Edson ilipokuwa ikiita, Elizabeth aliiona sana, alikuwa akiiangalia simu yake tu pasipo kuipokea. Moyo wake ulijawa na hofu kubwa, hakujua kama upigaji wa simu ile ulikuwa ni wa amani au kulikuwa na tatizo.

Kila alipotaka kuipokea, mapigo yake ya moyo yalimdunda mno, alitetemeka mwili huku uso wake ukionekana kama mtu aliyekosa amani, akabaki akiiangalia mpaka simu ilipokatika.

Alikwishajua kwamba mwanaume huyo alikuwa amepata kile alichomwachia sekretari, hakujua kama alifurahia au alichukia, hakujua maana ya kumpigia simu wakati ule, akabaki akitetemeka tu.
“Vipi tena?” aliuliza Candy aliyekuwa amefika nyumbani hapo asubuhi hiyo.
“Hakuna kitu.”

“Nani anakupigia simu?”
“Edson!”
“Sasa mbona hupokei?”
“Naogopa!”
“Kwa nini?”
“Mmmh! Wewe acha tu!’

Walibaki wakizungumza mengi, bado Elizabeth aliendelea kumwambia Candy juu ya hisia zake za kimapenzi kwa Edson kwamba alikuwa hali, halali, alichokuwa akikihitaji ni penzi la dhati kutoka kwa mwanaume huyo tu.
“Candy! Nikwambie kitu?”

“Niambie.”
“Nilikwenda ofisini kwa Edson!”
“Lini?”
“Leo hiihii.”
“Kufanya nini?”

“Nilimpelekea vitu ambavyo vilionesha ni kwa namna gani ninampenda, jamaniii, hivi yule mwanaume kaniwekea dawa gani? Mbona nimedata hivi?” aliuliza Elizabeth huku tabasamu pana likionekana usoni mwake.

Wakati wanazungumza mengi kuhusu Edson, mara wakasikia mlio wa honi kutoka nje ya nyumba hiyo, kitu cha kwanza alichokifanya Elizabeth ni kuchungulia dirishani, mlinzi alikwenda na kufungua geti, hakufungua geti kubwa, akafungua dogo.
“Candy!” aliita Elizabeth kwa mshtuko.
“Nini?”

“Edson!” alijibu Elizabeth huku akionekana kuwa na wasiwasi mahali hapo.
Edson hakutaka kuzungumza chochote na mlinzi, ndiyo kwanza akamsukumia pembeni na kisha kuelekea ndani ya nyumba hiyo ya kifahari.
Alipoufikia mlango, akakishika kitasa na kukifungua, akaingia ndani, macho yake yakatua kwa wasichana wawili, Elizabeth na Candy.

Alichokifanya ni kumtupia Elizabeth ule mfuko aliokuwa amemletea ambao ndani yake ulikuwa na vile vitu alivyokuwa amempa. Alipofanya hivyo, akageuka na kuanza kupiga hatua kutoka nje, alipoufikia mlango wa sebule hiyo, hata kabla hajaufungua akageuka nyuma.

“Nisikilize wewe malaya!” alisema Edson, alionekana kufura kwa hasira, Elizabeth akawa anatetemeka tu.

“Kuanzia leo, sitaki unizoee kabisa, yaani sitaki unizoee hata mara moja. Siyo unajiona wewe ni malaya basi unafikiri dunia nzima wapo kama wewe. Ukinifuatilia tena, nitakupiga risasi mpumbavu weee…” alisema Edson huku akionekana kuwa na hasira mno, alipomaliza, akaufungua mlango na kuondoka zake.

Elizabeth alibaki akiwa amesimama kama nguzo ya umeme, hakuamini kile kilichotokea, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, hakutingishika, alibaki vilevile na ghafla machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.

Je nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo

 

Leave A Reply