The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-13

0

Mwanamke bilionea mwenye kiu ya kupata mtoto, Elizabeth Marcel anajikuta akitukanwa na mume wa mtu kisa tu alikuwa akimpenda na kumtaka kimapenzi. Hilo, linamuumiza mno na kuamua kuachana naye kisha kusonga na maisha yake pasipo kujua Mungu amemuandalia kitu gani mbele yake.
SONGA NAYO…

Baada ya miezi miwili kupita, hatimaye maumivu yakawa yamepungua, hakumkumbuka tena Edson, aliamua kuachana naye na kufanya ishu zake nyingine. Safari hazikuisha, hakuwa mtu wa kutulia, leo alikuwa akienda nchi hii na siku nyingine alikwenda nchi nyingine.

Hivyo ndivyo maisha yake yalivyokuwa kwa kipindi kirefu. Katika siku ambayo alibuni mavazi ya kike aliyoyaita kwa jina la ELIZYAA, watu wengi walikusanyika ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee kulipokuwa kukifanyika uzinduzi wa mavazi hayo.
Kila mtu aliyeyaona, aliyapenda, yalikuwa mavazi yaliyobuniwa kwa ustadi mkubwa ambayo yalistahili kuvaliwa na mwanamke yeyote, sehemu yoyote ile pasipo kujali kama ilikuwa sehemu iliyotakiwa kuvaliwa mavazi ya heshima au la.

Hayo yakawa mafanikio yake makubwa, hakuamini pale alipohitajika kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya kufanya uzinduzi wa mavazi hayo kwani kwa mara ya kwanza bilionea kutoka nchini humo, Alhamdul Rasheed alipoyaona katika mitandao mbalimbali, aliyapenda na hivyo kuwasiliana na Elizabeth.

“Nataka tufanye biashara! Upo tayari?” aliuliza Rasheed kwenye simu.
“Nipo tayari!”
“Ninataka nifanye uzinduzi wa mavazi yako huku Morocco ila kwa makubaliano fulani,” alisema Rasheed.

“Makubaliano gani?”
“Asilimia ishirini iwe kwangu, upo tayari?”
“Mbona kubwa hivyo?”
“Basi kumi na tano!”
“Sawa! Hakuna tatizo.”

Elizabeth alijifunza mambo mengi katika biashara kwamba hauwezi kufanikiwa kama kila kitu utataka ufanye peke yako. Ili ufanikiwe zaidi, ilikuwa ni lazima kuchangia vitu fulani na watu wengine, hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Alijulikana dunia nzima kutokana na bidhaa zake alizokuwa akiziuza lakini ili kujulikana zaidi alitakiwa kufanya biashara hizo na watu wengine. Hakuangalia ni kiasi gani Rasheed angepata, alichokijali ni kwamba angeweza kulitangaza jina lake zaidi na hivyo kupata kiasi kikubwa cha fedha.

Hakuwahi kumuona Rasheed, alikuwa amewasiliana naye kwenye simu tu, alipanga kwenda nchini Morocco kwa ajili ya kuonana naye na kupanga jinsi mambo yatakavyokuwa, hivyo baada ya wiki moja, kila kitu kilipokamilika, akaanza safari ya kuelekea Morocco.

Baada ya saa kadhaa, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogador uliokuwa katika Jiji la Marrakech nchini Morocco. Kwa kuwa tiketi yake ilisomeka kama mtu maalumu, VIP, akapitishwa katika mlango wanaotakiwa kupita watu hao huku akiwa na begi lake kisha kuelekezwa mahali walipokuwa wenyeji wake walipokuwa wakimsubiri.

“Karibu Morocco,” alimkaribisha mwanaume mmoja wa Kiarabu, alikuwa amevaa kanzu ndefu nyeupe na kilemba kilichokuwa na kamba fulani kichwani.
“Asante sana,” aliitikia Elizabeth na kuanza kuelekea nje na mwanaume yule wa Kiarabu.

Safari yao iliishia nje ya uwanja ule, alipoangalia huku na kule, kulikuwa na magari mengi ya kifahari ambayo yaliegeshwa mahali hapo. Mazingira mazuri ya eneo hilo yalimfurahisha kwa kuwa yalivutia mno machoni mwake, kila alipoyaangalia alijikuta akiachia tabasamu pana.

Wakafuata moja ya magari ya kifahari yaliyokuwa mahali hapo kisha kuingia. Ilikuwa gari moja kubwa aina ya Jeep lililokuwa na rangi nyeusi.
Ndani ya gari lile kulikuwa na muonekano uliomshangaza mno, alilipenda na kujikuta safari nzima akitoa tabasamu pana tu.

Ni kweli aliwahi kukutana na magari mengi ya kifahari huku yeye mwenyewe akiwa anamiliki gari lenye thamani kubwa lakini katika maisha yake hakuwahi kukutana na gari kama lile aliloingia, akabaki akiliangalia tu.
“Ni gari zuri sijawahi kuona,” alijisemea Elizabeth.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply