The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-8

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA…

“Naombeni niende uani kwanza,” alisema Candy, Elizabeth akashtuka.

“Ooh! Hakuna tatizo, mwambie dada hapo akuelekeze,” alisema Edson.

ENDELEA NAYO..  

Candy akasimama na kutoka ndani ya ofisi hiyo. Kitendo cha kubaki wawili ndani ya ofisi ile, hapo ndipo Elizabeth akagundua kwamba Candy alifanya vile ili kuwaacha wawili hao peke yao, yaani Elizabeth atupe ndoano yake na hatimaye kumnasa Edson.

Akabaki kimya kwa muda, alikuwa akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kumwambia Edson. Alikumbuka kwamba usiku uliopita hakulala kwa raha kwa kuwa tu mawazo juu ya mwanaume huyo yalimsumbua mno. Siku hiyo, Edson alikuwa mbele yake, kwa muonekano wake tu, ulionesha kwamba alikuwa tayari kusikia chochote kutoka kwake.

“Edson…” aliita Elizabeth.

“Niambie.”

“Unajitahidi sana kwenye ufanyaji wako wa kazi, nimekufuatilia kwa kipindi kirefu, hakika wewe ni mchapakazi,” alisema Elizabeth.

“Asante sana Elizabeth! Hata wewe pia, una jina kubwa, pia unajitoa sana, hakika unastahili kuwa hapo ulipo,” alisema Edson.

Mpaka Candy anarudi ndani ya ofisi hiyo, hakukuwa na cha maana kilichoendelea zaidi ya mazungumzo ya kawaida tu. Elizabeth aliumia kwani alipewa muda wa dakika kumi nzima lakini hakuzigusia hisia zake kwa Edson.

Mpaka wanaaga na kuondoka huku wakiwa wamebadilishana namba za simu, Elizabeth hakuamini kama mikwara yake yote aliyokuwa nayo kabla angeweza kunywea mara atakapokutana na Edson.

“Vipi? Ulimwambia?”

“Hapana!”

“Eeeh! Hukumwambia tena?”

“Niliogopa, yaani mapigo ya moyo yalinidunda sana,” alisema Elizabeth.

“Jamani! Yaani presha yote ile ya jana na leo umeibuka kapa?”

“Yaani wewe acha tu shoga yangu! Sijui kwa nini.”

Waliendelea kuzungumza mpaka wakaingia ndani ya gari, Elizabeth alitamani arudi ofisini mle na kumwambia Edson namna alivyojisikia moyoni mwake lakini hakukuwa na nafasi hiyo tena.

“Ila namba ya simu si umeipata, sasa maliza kila kitu huko,” alisema Candy.

Kuwa na namba ya Edson kulimpa moyo kwamba angeweza kumpata mwanaume huyo. Kila wakati alikuwa mtu wa kuiangalia namba ile, alitamani kupiga na kuzungumza naye, japo aisikie sauti yake tu aridhike lakini aliona kwamba jioni ndiyo ungekuwa muda mzuri wa kuzungumza naye.

Saa ziliendelea kukatika, ilipofika saa 12 jioni, akachukua simu yake na kuiangalia namba ile, hakutaka kukubali, alichokifanya ni kuanza kumpigia Edson. Simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya Edson kusikika.

“Hallo!”

“Hallo Edson, u mzima?”

“Nipo poa Eliza. Mlifika salama?”

“Yeah! Nimefurahia mapokezi yako! Mungu akubariki,” alisema Elizabeth.

“Amen!”

“Sawa. Bye bye!”

“Bye!”

Alikuwa akipanga mistari mingi ya kumwambia Edson lakini kitu cha ajabu alipompigia simu, maneno yale yote yalifutika kichwani mwake jambo lililomfanya wakati mwingine kujiona mjinga.

Siku hiyo ikakatika hivyohivyo, alikuwa na mawazo mengi juu ya mwanaume huyo. Kesho yake, asubuhi, muda ambao alijua kwamba Edson alikuwa kazini akampigia simu na kuanza kuzungumza naye, akaomba miadi ya kuonana naye kwa mara nyingine ili amgawie kitabu kilichokuwa na mitindo ya nguo mbalimbali ambazo aliona kwamba staili moja ingemvutia hivyo kushonewa mke wake.

“Sawa! Njoo ofisini, ila wahi, saa sita nitaingia kikaoni,” alisema Edson.

“Nipe nusu saa.”

Hakutaka kuchelewa, hata hakutaka kumpa taarifa Candy, kwa kuwa alikuwa amekwishaoga asubuhi hiyo, alichokifanya ni kuanza kuelekea huko Ubungo kwa ajili ya kuonana na Edson tu.

Je nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply