The House of Favourite Newspapers

Penzi Lenye Maumivu-4

0

ILIPOISHIA IJUMAA:

Hakuwa na akili nyingi darasani, alikuwa na uwezo wa kawaida, upole wake ukawafanya wengi kupenda kuongea naye, lakini muonekano wake tu haukuwa wa kuwakaribisha watu hao kuzungumza nao, hasa wanafunzi wenzake. SONGA NAYO…

SIKU ziliendelea kukatika mpaka alipomaliza shule na hatimaye kukaa nyumbani kusubiri matokeo. Alichokifanya baba yake, Mzee Hawadhi ni kumchukua Halima na kumpeleka Mombasa walipokuwa shangazi na wajomba zake katika Mtaa wa Kilindini kwa ajili ya kipindi kifupi cha likizo.

Huko Mombasa alipofikia, Halima alikuwa gumzo kila sehemu, kila aliyemuona, alimpenda. Binti huyo alivutia, sura nzuri na umbo lake matata viliwachanganya wanaume wengi wa Mombasa.

Wengi walimsimamisha na kuzungumza naye, Halima hakuwa muongeaji, muda mwingi alikuwa kimya, wavulana walisumbuka naye, hawakuelewa kile kilichokuwa kwa msichana huyo mpaka kuamua kuwa kimya na kutopenda wanaume namna hiyo.

Hakufikiria mapenzi, hakuwahi kumpenda mvulana yeyote yule kwani aliamini kwamba hata kama angependa asingeweza kufanya mapenzi kwa sababu ya jinsi mbili alizokuwa nazo, hakutaka kabisa zionekane na mtu yeyote.

Uzuri wake haukupungua, uliendelea kuwa gumzo mahali hapo, wavulana kutoka Lamu, Bamburi na sehemu nyingine hapo Mombasa walifika Kilindini kumuona msichana wa Kitanzania ambaye alisifika kwa uzuri na walipofika hapo na kumuona, walithubutu kusema kwamba Halima alikuwa msichana mrembo mno.

Halima alikaa kwa mwezi mzima ndipo akarudi nchini Tanzania. Alitulia nyumbani, hakutaka kutoka, uzuri wake uliendelea kuwa gumzo mitaani na wengi walitamani kumuona, lakini walishindwa kwani muda mwingi alikuwa ndani na alipotoka kwenda kuswali, aliongozana na mama yake, jambo ambalo liliwapa ugumu wanaume wakware kumuingiza kwenye kumi na nane zao.

Siku zikakatika, hatimaye matokeo ya darasa la saba yakatoka na kufaulu. Baba yake alikuwa mfanyabiashara mkubwa, mwenye pesa hivyo hakutaka kumuona Halima akipata taabu ya aina yoyote, alichokifanya ni kumtafutia shule nyingine ya matajiri ya Liberty iliyokuwa Mikocheni B na kuanza masomo huko.

Alikutana na watoto wa kitajiri, watoto wa viongozi ambao kila siku waliletwa na magari ya kifahari. Hilo halikumtisha, kila alipowaangalia na kujiangalia, alijiona wakiwa wamefanana kwani hata baba yake, Mzee Hawadhi hakuwa mtu wa kawaida, alikuwa tajiri mkubwa aliyeingiza kiasi kikubwa cha fedha kila siku.

Kama ilivyokuwa sehemu nyingine, hata hapo shuleni wavulana wengi walivutiwa na msichana huyo mrembo. Wakajitahidi kuweka mawasiliano naye, kumzoea na mwisho wa siku kumtongoza, lakini Halima hakuwa msichana wa kuingilika.

Hakuwapenda wavulana kwa sababu alijijua jinsi alivyokuwa. Hakutaka vile alivyo kuonekana na mtu yeyote yule, alipanga kubaki peke yake katika maisha yake yote.

“Siwezi kupenda, sitaki kuwa na mwanaume yeyote,” alisema Halima kila alipokuwa chumbani akijiangalia kwenye kioo.

Uwezo wake shuleni uliendelea kuwa wa kawaida kama wengine, hakuwa mzungumzaji kama kipindi cha nyuma, hakuwa akichanganyika na wasichana chooni, alipokwenda huko kujisaidia, aliufungua mlango na kuufunga, hakutaka mtu yeyote yule amuone jinsi alivyokuwa.

Hiyo ilikuwa siri kubwa, siri iliyotesa maisha yake, iliyoutesa moyo wake usiku na mchana. Alipofika kidato cha tatu ndipo mwili wake ukawa na matamanio makubwa, mwili ukawaka na alikuwa na uhakika kwamba mwili wake huo ulihitaji mwanaume kuliko kitu chochote kile.

Hali hiyo ilimpa mawazo mno, hakujua angefanya nini, hakujua ni mwanaume gani ambaye alistahili kuwa naye, kumpa penzi bila kumwangalia kwamba alikuwa mtu wa aina gani. Huo ulikuwa mtihani mkubwa, shule nzima walijua kwamba alikuwa mkimya, hakuzoea kuzungumza na wanaume, jambo lililowapa wanaume hao wakati mgumu wa kujenga mazoea naye.

Wanaume wakamkwepa kwa sababu walimuogopa, hata pale alipohitaji mwanaume wa kuwa naye, hakufanikiwa kumpata na hata kama angempata hakuhisi kama angeweza kuwa naye kitandani, hakuona kama angeweza kufanya naye mapenzi kama wapenzi wengine walivyofanya.

Siku ziliendelea kukatika, mwili wake ulichachamaa, uliendelea kuwaka moto. Kila alipokaa, alifikiria ngono, alipolala, aliota ndoto za ngono, kila kitu alichokifanya wakati huo alikuwa akiwaza ngono tu.

“Nitakufa! Nitaweza kweli kuvumilia?” Alijiuliza, lakini akakosa jibu, wakati akiwa kwenye hali ya mawazo, hali ya kutamani kuwa na mvulana, ndipo alipopokea ujumbe wa maandishi, ulioandikwa kwenye kikaratasi kutoka kwa mvulana aliyeitwa Wilbert Kinyambi, kijana mwenye sura nzuri aliyekuwa akisoma naye hapo shuleni.

Halima alibaki akiuangalia ujumbe ule mfupi uliotoka kwa kijana huyo ambaye alimwandikia na kutaka kuonana naye. Mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu, hakuamini kama kijana huyo angediriki kuomba kuonana naye katika kipindi kama hicho, kipindi alichokuwa akihitaji mwanaume kwa nguvu zake zote.

Alikuwa radhi kuonana na Wilbert, ila jambo alililokuwa akilifikiria lilikuwa ni kufanya naye mapenzi. Hakuwa radhi, hakutaka kuona mwanaume yeyote yule akizitoa nguo mwilini mwake na kufanya naye mapenzi.

Moyo wake ulimuuma mno, kila siku alimlaumu Mungu kwa kile alichokuwa amekifanya katika mwili wake kwani kwa uzuri aliokuwa nao, hakustahili kuwa na jinsi mbili kama alivyokuwa.

“Nionane naye au?” Alijiuliza, baada ya kukaa kwenye mawazo kwa kipindi kirefu, akakubali kuonana naye, kwa sababu kwenye ujumbe ule mfupi Wilbert aliambatanisha na namba yake ya simu, akaamua kumpigia.

** *

Miongoni mwa wavulana waliokuwa wakimpenda Halima alikuwa kijana Wilbert ambaye alisoma kidato cha tatu kama msichana huyo shuleni hapo. Moyo wake uliteseka kwa penzi kubwa alilokuwa nalo kwa msichana huyo, mara kwa mara alipokuwa akimwangalia, uzuri wake uliutikisa moyo wake.

Kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa msichana huyo, alipokuwa akiwasikia wavulana wakimzungumzia Halima, moyo wake ulimuuma mno, alijua kwamba wasingeweza kumpata kutokana na maisha aliyochagua kuishi shuleni hapo, lakini hilo halikutaka kumpa uhakika kwamba wangeshindwa, kwake, alitaka kuona yeye akiwa na msichana huyo na si mtu mwingine yeyote yule.

Kutokana na uzuri wa sura yake, wasichana wengi walimfuata na kumwambia kwamba walikuwa wakimpenda, lakini Wilbert hakutaka kusikia, hakutaka kuwaelewa kwani kila alipojiangalia, moyoni mwake alimuona Halima, akiwa amevuta kiti na kukaa kabisa.

Hakuwahi kuzungumza na msichana huyo, alitamani sana kufanya hivyo. Ukimya wake ukamuogopesha na kumuona mwanamke aliyekuwa na msimamo ambaye hata kama angemfuata na nini, msichana huyo asingeweza kukubaliana naye hata mara moja.

Kila siku Halima alipelekwa kwa gari shuleni hapo, Wilbert alipokuwa akifika, kitu cha kwanza kabisa alikuwa akiangalia sehemu ambapo gari lililokuwa likimleta msichana huyo lilipokuwa likipaki, alipokuwa akiliona, moyo wake ulifurahi kwa kuona kwamba siku hiyo alikuwa na uhakika wa kumuona msichana huyo ila asipoliona, moyo wake ulikuwa na huzuni kubwa kana kwamba alikuwa mgonjwa.

Siku ziliendelea kukatika, aliendelea kuteseka moyoni mwake, kila siku alipokuwa akimwangalia Halima, uzuri wake uliongezeka maradufu. Wakati mwingine alikuwa akichelewa kulala kwa kuwa alikuwa akimfikiria msichana huyo, hata siku ambazo alikuwa akilala mapema, alipokuwa akiamka, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumfikiria Halima tu. Je, nini kitaendelea? Tukutane Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply