Penzi Lisiloisha  048

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kufanya chochote kumsaidia msichana huyo. Licha ya tofauti kubwa ya hali zao kiuchumi, Anna akitokea kwenye familia ya kitajiri na kijana huyo akitokea kwenye familia ya kifukara, mapenzi yao yanashamiri kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Awali, Jafet alikuwa akisomeshwa na kanisa kwa makubaliano kwamba akimaliza masomo atajiunga na mafunzo ya upadri kwa ajili ya kulitumikia kanisa, lakini baadaye anabadilisha uamuzi na kukataa kwenda kusomea tena upadri kutokana na jinsi alivyokuwa anampenda Anna.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Baada ya Jafet na Anna kuhitimu kidato cha nne, Anna anaanza maandalizi ya kutafuta shule ili wakasome pamoja kidato cha tano na sita, gharama zote zikiwa ni juu yake kwani wazazi wa Jafet hawakuwa na uwezo wa kumsomesha.

Msichana huyo anafanya kila kinachowezekana na hatimaye wawili hao wanajiunga kidato cha tano kwenye shule moja, bila wazazi wa Jafet kujua chochote. Baadaye Anna anaanza kuumwa figo, baada ya kuhangaika sana Jafet anaamua kumtolea figo moja, wanasafiri hadi India ambako wanafanyiwa upasuaji na msichana huyo kuwekewa figo nyingine kutoka kwa Jafet.

Zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa kisha wanarejea Tanzania. Wiki kadhaa baadaye, wazazi wa Anna wanamshinikiza Jafet awapeleke nyumbani kwa wazazi wake ili wakawashukuru kwa wema wake, anakuwa mgumu lakini baadaye anakubali, wanafunga safari mpaka kijijini Rwamgasa.

Wazazi wa Anna wanamkataa Jafet baada ya kujua maisha yake halisi na kwa juhudi za mama yake, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani kisha anapelekwa bila hata kuagana na Jafet, jambo ambalo linamuumiza mno kijana huyo kutoka familia ya kimaskini.

Anna naye anajikuta akianza kuzoeana na William, Mtanzania mwenzake waliyekuwa wakisoma naye chuoni nchini Marekani na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele ndivyo wanavyozidi kuwa karibu ma hatimaye wanasafiri pamoja mpaka Tanzania.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Kesho yake asubuhi, Jafet aliianza safari ya kuelekea kijijini kwao, Rwamgasa ambako nako alipanga kukaa siku mbili tu kisha kurejea jijini Dar es Salaam. Aliamini akiwa huko akili yake itatulia kwani mazingira ya nyumbani kwao yalikuwa yakimkumbusha mambo mengi aliyowahi kufanya na Anna.

Baada ya kuwasili kijijini Rwamgasa, Jafet alikuwa amebadilika mno. Hakuwa yule aliyeondoka kuelekea jijini Mwanza, alionesha kuchoka kimwili na kiakili, uso wake ulipoteza kabisa matumaini, jambo ambalo mama yake alilitambua kwa haraka.

“Huko ulikoenda umepatwa na nini?”

“Kwa nini unaniuliza mama?”

“Sasa mimi nakuuliza swali badala ya kunijibu na wewe unaniuliza.”

“Hakuna nilichokutana nacho mama.”

“Unajua mimi ndiye niliyekuzaa na nakujua hata kabla hujazaliwa? Hebu niambie umepatwa na nini?”

Badala ya kujibu swali aliloulizwa na mama yake, Jafet alijikuta akianza kutokwa na machozi, maswali ya mama yake yalienda kuutonesha mtima wake, akajiinamia huku hisia chungu zikiendelea kupita ndani ya kichwa chake.

Mama yake alimtazama usoni, akazisoma hisia zake na kuelewa nini kilichokuwa kinamsumbua, akamkumbatia na kuanza kumpigapiga mgongoni kama ishara ya kumbembeleza.

“Sasa mwanangu, utaendelea kuwa kwenye hali hiyo mpaka lini? Yaani kila siku tutakuwa tunazungumzia mambo yaleyale? Wewe ni mwanaume mwanangu, jikaze kiume,” alisema mama yake Jafet kwa upole huku akiendelea kumkumbatia mwanaye.

“Unakumbuka kipindi kile kwa sababu ya kumuwaza huyo mwanamke wako mpaka ukapatwa na matatizo ya figo, sasa hivi umepona unataka kurudia makosa yaleyale, kwa nini mwanangu?”

“Moyo unauma mama.”

“Sawa hata kama moyo unauma, inatakiwa ufike mahali ukubaliane na ukweli. Wewe unalia na kuumia kila siku, una uhakika kama na yeye huwa anakufikiria?”

“Nimemuona akiwa na mwanaume mwingine.”

“Sasa hicho ndiyo kinakuliza? Mshukuru Mungu kwa kila jambo, huwezi kujua amekuepusha na nini, kazania elimu ili uje utusaidie sisi ndugu zako, si unaona jinsi umaskini unavyotutesa?”

Mama yake Jafet aliendelea kuzungumza na mwanaye, akawa anampa maneno ya kumpa faraja na baada ya muda, Jafet alikuwa ametulia. Siku hiyo ilipita, kesho yake akazungumza na wazazi wake kuhusu safari yake ya kurejea jijini Dar es Salaam ambapo hakuna aliyekuwa na kipingamizi.

Maandalizi yakafanyika na hatimaye akafunga safari ya kurejea masomoni jijini Dar es Salaam. Japokuwa alikuwa akijikaza kiume, kila picha ya tukio la kumuona Anna akitoka uwanja wa ndege akiwa amekumbatiwa na mwanaume mwingine ilipokuwa ikimjia, ilikuwa ikiuumiza sana moyo wake.

***

Safari ya Anna na William kuelekea jijini Dar es Salaam ilikuwa nzuri sana kwa wote wawili. Japokuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Anna kufika jijini Dar es Salaam, safari hii alikuwa huru zaidi kwani alikuwa na mtu anayeifahamu vyema mitaa ya jiji hilo ambaye naye aliahidi kumtembeza kila sehemu aliyokuwa anaitaka.

“Nataka mpaka likizo ikiisha niwe nimeshafika kila sehemu maarufu hapa Dar,” alisema Anna wakiwa wamepumzika kwenye bustani ya maua, nje ya jumba la kifahari la akina William.

“Usijali Anna, utafika hata sehemu ambazo hujawahi kuzisikia. Unakujua Mbudya wewe?”

“Mbudya? Ndiyo wapi?”

“Ni kisiwa kimoja kidogo kilichopo kwenye Bahari ya Hindi, nitakupeleka na naamini utafurahi,” alisema William, wote wakacheka na kugongesheana mikono.

“Nataka unipeleke kwanza Coco Beach, napasikiaga tu wala sijawahi kufika.”

“Wala usijali Anna, leoleo nakupeleka, nataka ufurahi.”

“Nitafurahi kiukweli.”

Jioni ya siku hiyo, wawili hao walienda mpaka Ufukwe wa Coco ambapo William alitumia nafasi hiyo kujaribu kumshawishi tena Anna akubali kufanya naye mapenzi.

“Anna.”

“Mmh!”

“Unajua huu ndiyo muda muafaka wa kufungua ukurasa mpya wa mapenzi yetu. Unajua kwa kipindi kirefu nimekuwa nikitamani sana kupata nafasi kama hii, ya kukaa mimi na wewe tu na nadhani sasa imetimia.”

“Unamaanisha nini William.”

“Nataka mimi na wewe leo tulale kitanda kimoja, tujifunike shuka moja usiku kucha.”

“Bado sikuelewi, hebu nenda kwenye pointi moja kwa moja.”

“Anna, nakupenda mwenzio! Nimeshasubiri vya kutosha mpenzi wangu, naomba ukubali kufanya mapenzi na mimi.”

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye gazeti la Risasi Mchanganyiko.


Loading...

Toa comment