The House of Favourite Newspapers

Pigo: Wanne Familia Moja Wafariki Katika Mazingira Tofauti

0

FAMILIA ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa Delphina Mamiro, imepata pigo ndani siku 28 kwa kupoteza watu wanne, akiwamo profesa huyo.

 

 

Awali, wazazi wa profesa huyo walifariki dunia wakipishana siku tatu, baada ya kuanza mama yake, Franciska Kyessi, aliyefariki dunia Januari 13, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mfupi na kufuatiwa na baba yake.

 

 

Hata hivyo, wakati machungu hayo hayajapoa, Profesa Delphina alianza kujisikia vibaya mwanzoni mwa mwezi huu na kufariki dunia akipatiwa matibabu hospitali na siku chache baadaye mumewe alifariki dunia.

 

 

Anna Mamiro, ambaye ni mtoto wa Profesa Delphina, alisema vifo vya wazazi wao ni pigo kwa familia. Wakati wakiombeleza kifo cha bibi yao, Januari 16, mwaka huu wakapata pigo jingine la kifo cha babu yao, Mchungaji Lucas Kyessi, ambaye alifariki ghafla.

 

“Mama na baba walitoka Morogoro na kwenda Moshi kwa ajili ya kuzika na baada ya hapo walirejea Morogoro na kuendelea na majukumu yao. Baada ya siku chache mama akawa analalamika hajisikii vizuri. Baadaye akaugua na ikabidi kumpeleka hospitali ya mkoa kwa matibabu zaidi, alifariki Jumamosi iliyopita, Februari 6, baada ya kuzidiwa.

 

 

“Wakati tukiendeleza maandalizi ya mazishi na kusafirisha mwili wa mama kwenda mkoani Kilimanjaro, usiku wa kuamkia Februari 9, mwaka huu, tukapata msiba mwingine mzito wa baba yetu, Dkt. Peter Mamiro, ambaye alifariki dunia nyumbani maeneo ya Veta Kihonda baada ya kuugua kwa muda mfupi,” alisimulia Anna.

 

 

 

 

Akizungumzia msiba huo, Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Paphael Chibuda, alisema kama wanajumuiya wa chuo wamepoteza sehemu ya wanafamilia, ambapo  wamempoteza Profesa Delphina ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Mimea Vipando na Bustani (Department of Crop Science and Horticulture).

 

 

 

Profesa Delphina pamoja na kuwa mhadhiri wa SUA, pia alikuwa anatumika katika masuala ya ushauri kwenye taasisi mbalimbali za umma.

 

 

Dkt. Peter alistaafu kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sokoine, kabla yake alikuwa mhadhiri wa Kitivo cha Chakula na Lishe katika Chuo Kikuu cha Sokoine.

Leave A Reply