The House of Favourite Newspapers

Namungo Yarejea, Yasubiri maamuzi ya Caf

0

 

BAADA ya kuahirishwa kwa mchezo wao wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola, kikosi cha Namungo kimeanza kurejea nchini leo kutokea jijini Luanda, Angola.

 

 

Mchezo huo uliopangwa kufanyika jana katika dimba la Estádio 11 de Novembro, Luanda nchini Angola, uliahirishwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), baada ya kutokea sintofahamu iliyotokana na wenyeji hao kusema wachezaji watatu wa kikosi cha Namungo pamoja na kiongozi mmoja kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona na kuwataka Namungo wawekwe karantini au warudi Tanzania.

 

 

Kutokana na sintofahamu hiyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Mamlaka za Kiserikali ya Tanzania viliingilia kati suala hilo na kusababisha mchezo huo kufutwa huku Caf ikiendelea kuchunguza.

 

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Namungo, Kindamba Namlia alisema: “Ni kweli kikosi chetu kinarejea kutokea Angola ambapo tulikuwa na changamoto kidogo, hatuwezi kusema mengi kwa sasa lakini kama ambavyo taarifa zimetolewa tunasubiri mamlaka za uchunguzi za Caf ili kujua nini kitaendelea.”

 

 

Kwa mujibu wa kanuni za Caf, upo uwezekano mkubwa wa Namungo kupewa ushindi katika mchezo huo.

 Joel Thomas, Dar es Salaam

 

Leave A Reply