The House of Favourite Newspapers

Baba wa Kindoki Afariki, Akacha Msiba, Kucheza leo

MZEE Kindoki Nkinzi ambaye ni baba wa kipa wa Yanga, Mkongomani, Klaus Kindoki amefariki dunia huko nyumbani kwao DR Congo huku yeye akikacha mazishi kwa ajili ya kuipambania timu yake inayojiandaa kujitupa uwanjani leo.

 

Yanga inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Kambarage huko mkoani Shinyanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United unaotarajiwa kuwa mgumu.

 

Kindoki ndiye anayetarajiwa kuanza katika kikosi hicho baada ya kipa, Ramadhani Kabwili kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja na nusu akisumbuliwa na maumivu ya nyonga.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari Msaidizi wa Yanga, Godlisten Anderson ‘Chicharito’, alisema baba wa kipa huyo alifariki wiki moja iliyopita lakini alishindwa kuzipata taarifa za kifo hicho kutokana na matatizo ya kimtandao yaliyokuwepo DR Congo.

 

“Baba yake ana wiki moja na siku kadhaa tangu afariki dunia, yeye taarifa alizipata juzi za kifo hicho kutokana na matatizo ya kimtandao yaliyokuwepo nchini kwao. “Kama unavyofahamu hivi sasa DR Congo hakuna amani, hivyo mtandao unasumbua na mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumapili (kesho).

 

“Licha ya msiba huo, lakini Kindoki anatarajiwa kukaa golini katika mchezo wetu na Stand na baada ya mchezo ndiyo ataanza mipango ya kurejea kwao kwa ajili ya kumalizia msiba,” alisema Chicharito.

Comments are closed.