The House of Favourite Newspapers

POLISI AMJARIBU LUGOLA KWA MENO YA TEMBO

DAR ES SALAAM: SIKU moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba, Kitengo cha Kufichua Maovu cha Global Publishers (OFM) kimenasa siri nzito kwenye jeshi la polisi baada ya kunyetishiwa juu ya askari aliyefahamika kwa jina moja la Ruben akidaiwa kukutwa na meno ya tembo.

NI MBEYA

 

Tukio la kukamatwa kwa askari huyo linadaiwa kutokea Juni 23 mwaka huu, maeneo ya Sheli ya Esso mkoani Mbeya baada ya makachero wa polisi kumuwekea mtego.

OFM YATONYWA

Awali, OFM ilitonywa na vyanzo vyake juu ya uwepo wa tukio hilo lililokuwa linafuatiliwa kwa karibu na makachero wa jeshi la polisi.

 

MTEGONI WASUKWA NA POLISI

Ilielezwa kuwa, Ruben akiwa na wenzake wawili, mmoja akitajwa kwa jina la Fundi na mwingine akifahamika kwa jina la Jafari kwa pamoja walishiriki katika kufanya biashara hiyo haramu.

“Hawa walikuwa watatu, wakasakwa kuingizwa kwenye kumi na nane kwa muda mrefu.

“Hawa jamaa ni miongoni mwa watu ambao wanadaiwa kuwa kwenye mtandao huu wa biashara ya meno ya tembo sasa makachero wa jeshi la polisi walitumia mbinu zao mbalimbali kuhakikisha wanawadaka,” kilidai chanzo makini.

 

Chanzo hicho kilizidi kueleza kuwa, awali Ruben na wenzake walikuwa wazito kidogo kuingia kwenye mtego wa jeshi la polisi lakini siku hiyo waliweza kuingia na kujikuta wamekamatwa.

“Unajua kuna mbinu mbalimbali ambazo polisi wanazitumia sasa hawa mwanzoni walikuwa wanaruka vihunzi mara kwa mara.

“Kuna wakati walipokuwa wanaulizwa dili bila kujua na makachero wa polisi walikuwa wanaelekeza eneo la mbali na hapa Mbeya mjini, lakini kama unavyojua za mwizi siku zote ni arobaini wakajikuta wameuvaa mkenge na kukamatwa,” kilidai chanzo hicho.

Makachero wa OFM kupitia vyanzo vyake, walifanikiwa kunasa picha za baadhi ya watuhumiwa hao akiwemo askari huyo pamoja na Jafari wakiwa mikononi mwa polisi.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya na kuwekwa mahabusu wakisubiria taratibu zaidi za kiuchunguzi kabla ya kufikishwa mahakamani.

 

WASIWASI WA ISHU KUZIMWA WAIBUKA

Hata hivyo, wakati OFM ikifuatilia sakata hilo, ilielezwa kuwepo na wasiwasi wa tukio hilo kutotiliwa mkazo na jeshi na polisi hivyo kuzua hofu ya kuzimwa pasipo watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

“Hebu nyinyi OFM kwa kuwa mnafukua maovu fuatilieni kwa undani maana jinsi sakata hili linavyoenda linaweza lisijulikane kabisa katika jamii,” OFM ilitonywa na chanzo makini.

LUGOLA ATUPIWA ZIGO

Chanzo hicho kilizidi kwenda mbele zaidi kwa kulielekeza suala hilo kwa waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kwani ni miongoni mwa changamoto kubwa anazotakiwa kupambana nazo.

“Hili suala Lugola kwa kuwa ndio kwanza amekabidhiwa ofisi, anabidi asimame imara kweli maana ukiacha yale aliyoambiwa na Rais Dk John Magufuli wakati anaapishwa, meno ya tembo nayo ni tatizo kubwa.

“Unaweza kuuona ukubwa wa tatizo hususan pale unapoona hadi polisi nao wanatajwa kuhusika katika biashara hii haramu,” kilieleza chanzo hicho.

KAMANDA MBEYA AZUNGUMZA

Mara baada ya kuelezwa madai hayo, juzi Jumanne, OFM ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mbeya, Ulrich Matei ambapo alipopatikana aliomba apewe muda kwa kuwa ndio kwanza amekabidhiwa ofisi kutoka kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mbeya, ACP Mussa Taibu aliyehamishiwa makao makuu ya jeshi hilo hivi karibuni.

“Hilo tukio nimesikia lipo lakini kama unavyojua mimi ni mgeni hapa, hata hii simu nimekabidhiwa hapa na wewe (mwandishi) unanipigia, subiri nilifuatilie kwa ukaribu zaidi ili niweze kuwa na majibu mazuri kuhusiana na tukio hilo,” alisema Kamanda Matei.

LUGOLA HAPATIKANI

Amani lilifanya jitihada za kumtafuta waziri Lugola ili kumsikia anazungumziaje changamoto hiyo na namna alivyojipanga kuikabili lakini bahati mbaya hakuweza kupatikana hewani.

Comments are closed.